Tuesday, March 28, 2017

SOMO: CHAKULA CHA KICHAWI


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH
[KANISA LA UFUFUO NA UZIMA]
GCTC → MOROGORO
JUMAPILI: 26 MARCH 2017

MHUBIRI: PASTOR BARAKA NJAMASI (SNP MAHENGE)

SOMO: CHAKULA CHA KICHAWI


Kwa nini leo tunaongea kwa habari ya chakula? Ni kwa sababu zipo aina nyingi za vyakula. Mathalani vipo vyakula vya kimwili, vyakula vya Kimungu na hata vyakula vya kishetani. Chakula ni kitu chochote kinachoweza kuingizwa mwilini au rohoni na kumpa mtu nguvu na uhai ili aishi. Viumbe hai vyote hula vyakula vya aina tofauti tofauti, na hivi ni vyakula vya kimwili, vingine ni vya Kimungu na vyakula vingine ni vya kishetani (Kichawi). Mifano ya Vyakula hivi ni kama ifuatavyo:-

1.      CHAKULA CHA MWILINI

Katika MAMBO YA WALAWI 11:1-8 Imeandikwa hivi (Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 2 Neneni na wana wa Israeli, mkiwaambia, Wanyama hawa ndio wanyama wenye uhai mtakaowala, katika hayawani wote walio juu ya nchi. 3 Kila mnyama mwenye kwato katika miguu yake, mwenye miguu ya kupasuka kati, mwenye kucheua, katika hayawani, hao ndio mtakaowala. 4 Pamoja na hayo, wanyama hawa hamtawala katika wale wenye kucheua, na katika wale walio na kwato; ngamia, kwa sababu yuacheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. 5 Na wibari, kwa sababu yeye hucheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. 6 Na sungura, kwa sababu hucheua, lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. 7 Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu. 8 Msiile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao; hao ni najisi kwenu.). Wana wa Israeli walipewa sheria hizi mara tu baada ya kutoka utumwani Misri. Hizi sheria za ‘kipi kiliwe na kipi kisiliwe’ ziliwekwa kwa wakati ule wa Agano la Kale.

 

Kwa nyakati hizi za Agano Jipya, Neno la Mungu linasema je kuhusu sheria za kukataza kuliwa kwa baadhi ya vyakula? Tunaposoma katika 1 TIMOTHEO 4:1-5 maandiko yanasema hivi.. (Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; 2 kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; 3 wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli. 4 Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani; 5 kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.). Kwa maandiko haya ndiyo kusema kwamba, endapo kipo chakula usichokitaka au mnyama ambaye wewe hutaki kumla, ufanye hivyo lakini siyo kwa kuwahukumu wengine wanaokula vitu hivyo. Yesu mwenyewe alikuwa akila na kunywa, kiasi kwamba baadhi ya Mafarisayo walianza kumwita MLAFI na hata kumtofautisha na Yohana Mbatizaji ambaye alikuwa akifunga mara kwa mara.

 

 

Katika chakula kuna nguvu. Ndivyo ilivvyoandikwa katika 2WAFALME 4:8-17 (Hata ikawa siku moja, Elisha alikwenda Shunemu; na huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo; naye akamshurutisha aje ale chakula. Ikawa kila alipopita njia ile, huingia kula chakula. 9 Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu. 10 Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo. 11 Ikawa siku moja akafika huko, akaingia katika chumba kile akalala. 12 Akamwambia Gehazi mtumishi wake, Mwite yule Mshunami. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mbele yake. 13 Akamwambia, Sema naye sasa, Tazama, wewe umetutunza sana namna hii; utendewe nini basi? Je! Uombewe neno kwa mfalme, au kwa amiri wa jeshi? Yule mwanamke akamjibu, Mimi ninakaa katika watu wangu mwenyewe. 14 Akasema, Basi, atendewe nini? Gehazi akajibu, Hakika hana mwana, na mumewe ni mzee. 15 Akamwambia, Kamwite. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mlangoni. 16 Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa Mungu, usiniambie mimi mjakazi wako uongo. 17 Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto mume wakati uo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia. 18 Hata yule mtoto alipokua, ikawa siku moja alitoka kwenda kwa baba yake kwenye wavunao). Tunajifunza kuwa kumbe hata chakula kinaweza kusababisha mtu kuongea kitu cha baraka. Kupitia chakula na ukarimu wa watu hawa, ni dhahiri kwamba Mungu wa Mbinguni aliongea kwa habari ya huyu mama na mumewe kupitia maneno ya unabii wa Elisha. Ingawa wote hawa ni vikongwe lakini Mungu aliwapa mtoto baada ya mwaka mmoja, sawa sawa na unabii wa Elisha. Ukitenda mema kwa watumishi wa Mungu ujue kwamba Mungu atasababisha miujiza kwako katika Jina la Yesu.

 

Imeandikwa katika 2 WAFALME 6:20-23 (Naye mfalme wa Israeli alipowaona, akamwambia Elisha, Ee baba yangu, niwapige? Niwapige? 22 Akamjibu, Usiwapige; je! Ungetaka kuwapiga watu ambao umewatwaa mateka kwa upanga wako na uta wako? Weka chakula na maji mbele yao, wapate kula na kunywa, na kwenda kwa bwana wao. 23 Basi akawaandalia chakula tele; nao walipokwisha kula na kunywa, akawaacha, wakaenda zao kwa bwana wao. Na vikosi vya Shamu havikuja tena katika nchi ya Israeli.). Tunajifunza kuwa hata ukiwa na adui yako, wewe umpe chakula tu ale. Tunapaswa kuwatendea mema maadui zetu kwa sababu tunafahamu kuwa rohoni tumeshawashinda na hawatuwezi kamwe tena kwa Jina la Yesu.

 

2.      CHAKULA CHA KIMUNGU:

Mungu huwa analisha watu wake. 1WAKORINTHO 10:1-4 (1 Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; 2 wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; 3 wote wakala chakula kile kile cha roho; 4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Mungu aliwashushia chakula wana wa Israeli kule Jangwani, kilichoitwa MANA.

 

Neno la Mungu katika YEREMIA 15:16 linasema hivi “Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi”. Kumbe maneno ya Mungu yanaweza kuonekana na hata kuliwa. Mungu anaweza kumtumia mtu yeyote. Chakula cha Kimungu kinatupa uwezo wa kusonga mbele na kumshinda shetani. Tunapoongea habari za chakula tunaongelea habari za Yesu Kristo. Imeandikwa pia katika KUTOKA 16:32 “Musa akasema, Hili ni neno Bwana aliloliamuru, Pishi moja ya kitu hicho na kiwekwe kwa ajili ya vizazi vyenu; ili kwamba wao wapate kukiona kile chakula nilichowalisha ninyi barani, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri”.

 

Pia Imeandikwa katika ZABURI 119:11 “Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi”. Ukiona mtu anafanya maovu, anaiba au anatukana ujue moyoni mwake hajaliweka neno la Mungu. Kwa hiyo ukila neno la Mungu hatutarajii uwe mzinzi au mwasherati. Ukila neno la Mungu sawasawa utakuwa unaongozwa na Neno la Mungu. Ukila Neno la Mungu utashiba. Mungu pia anatufundisha katika WALAWI 21:6… “Watakuwa watakatifu kwa Mungu wao, wala wasilinajisi jina la Mungu wao; kwa kuwa wao ndio wasongezao sadaka za Bwana kwa njia ya moto, chakula cha Mungu wao; kwa ajili ya hayo watakuwa watakatifu”.

 

Na tena Imeandikwa katika YOHANA 6:55-56 …. (Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake.). Yesu hapa alimaanisha kuwa Yeye ni Neno. Wayahudi walidhani kwamba Yesu alikuwa anaataka waule mwili wake na kunywa damu yake. Kumbe Yesu alikuwa anazungumza mambo ya rohoni zaidi. Ndiyo maana katika 1WAKORINTHO 10:31 “Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.” Kwa nini tuombe na kushukuru? Ni kwa sababu vyakula vingine ukivila vinageuka na kuwa magonjwa mwilini mwako. Vipo vyakula ambavyo wachaawi huvinuizia maneno na pale unapovila kabla ya kuviombea, ni dhahiri vitasabisha madhara na magonjwa mbalimbali mwilini mwako. Kwa nini ukubaliane na daktari anayekuambia kwamba Moyo wako Umetoboka? Swali la kumuuliza huyo daktari ni “Nani ameutoboa moyo wangu?” Endapo daktari atakuambia kuwa amekupima na kuona uvimbe tumboni. Swali la kumuuliza huyo daktaari ni “Nani aliyesababisha huo uvimbe”

 

3.      CHAKULA CHA KICHAWI (KISHETANI):

Hivi ni vyakula vinavyoletwa na yule “mungu-asiye sawa”. Kwa maana nyingine ni vyakula vinavyotokana na nguvu za “mungu wa dunia hii” (yaani shetani). Vyakula hivi ni vile vinavyotumiwa sana waganga wa kienyeji, wachawi, wasihiri, wafuga majini na wasoma nyota wa siku za leo ili kuleta uharibifu kwa watu wengine.

UKIRI
Kwa Jina la Yesu leo navitapika vyakula vyote vay kishetani nilivyowahi kulishwa. Kila vyakula vya kishetani viondoke vyote kwa Jina la Yesu. Amen

 

Imeandikwa katika MATENDO 21:25 “Lakini kwa habari za watu wa Mataifa walioamini, tuliandika na kutoa hukumu yetu ya wao kujilinda nafsi zao na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na kitu kilichosongolewa, na uasherati”. Mungu alisema tujiepushe na unajisi wa sanamu. Endapo unacho kitu unachokipa nafasi ya juu sana, labda ni gari au nyumba, ujue mashetani watependa kukaa mahali hapo kwa kuwa hiyo tayari ni sanamu!!.

 

Imeandikwa pia katika MATENDO 15:19-20 (Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; Tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika Mataifa; 20 bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu). Kuna watu wanazindika nyumba au magari yao kwa kafara za damu. Kwa kufanya hivyo ujue umeyaruhusu mashetani yatoke kuzimu na kuhamia kwenye hilo gari au nyumba. Ukeshajiepusha na sanamu za aina hii, Mungu atataka uanze mara moja kumwabudu Yeye Peke Yake. Katika maandiko haya kuna maneno yasemayo “Nyama iliyosongelewa” ambayo ni ile inayochinjwa kwa kutamkiwa maneno fulani-fulani. Kwa kawaida waganga wa Kienyeji hawapokei zawadi kama vile matembele au karanga. Haw hupokea wanyama kama mbuzi, kuku n.k na wanapowachinja hutamka maneno yao ya kiganga wakati ile damu inapokuwa inamwagika ardhini, ili kusababisha madhara yaliyokusudiwa!!.

 

Katika WALAWI 17:11 imeandikwa …“Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi”. Mungu alikataza watu wasile nyama pamoja na damu yake. Lakini damu nyingine zinapochinjwa kwa upande ule wa ibilisi, humwagika zikiwa “zina maneno” ambayo mwishowe huendelea kuongea hata ziwapo ardhini. Damu inaweza kutoa machozi, kwa kuwa damu inao uhai. Katika Ulimwengu wa Roho, waganga wa kienyeji wanafahamu haya mambo, na ndiyo maana wanapokuwa wanachinja kafara zao damu hizi huyatamka maneno ya Balaa kama vile “Asizae” / au “Achanganyikiwe”/ au “Afukuzwe kazi” n.k. Hata hivyo sisi tuliookoka, tunaitumia DAMU YA YESU ambayo hunena mema kwetu (kama ilivyoandikwa katika WAEBRANIA 12:24 “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.”). Hata kama wachawi watataja majina yao, sisi tutalitaja Jina la Yesu. Wao watataja farasi, sisi tutalitaja Jina la Yesu. Damu zingine zote zinaongea mabaya. Ni Damu ya Yesu pekee inayonena mema hata sasa.

 

Kipindi fulani walitokea watu majasiri waliogoma kula vyakula vya kichawi. DANIELI 1:5- (Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme. 6 Basi katika hao walikuwapo baadhi ya wana wa Yuda, Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria. 7 Mkuu wa matowashi akawapa majina; alimwita Danieli, Belteshaza; na Hanania akamwita Shadraka; na Mishaeli akamwita Meshaki; na Azaria akamwita Abednego. 8 Lakini Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi. 9 Basi Mungu alimjalia Danieli kupata kibali na huruma machoni pa huyo mkuu wa matowashi. 10 Mkuu wa matowashi akamwambia Danieli, Mimi namwogopa bwana wangu, mfalme, aliyewaagizia ninyi chakula chenu na kinywaji chenu; kwa nini azione nyuso zenu kuwa hazipendezi kama nyuso za vijana hirimu zenu? Basi kwa kufanya hivyo mtahatirisha kichwa changu mbele ya mfalme. 11 Ndipo Danieli akamwambia yule msimamizi, ambaye mkuu wa matowashi amemweka juu ya Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria, 12 Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi; na watupe mtama tule, na maji tunywe). Danieli na wenzake waliazimu kupewa mtama na maji tu kwa sababu kile chakula cha mfalme kabla ya kuliwa kilikuwa kinanuiziwa mambo mbalimbali na mizimu ya ufalme ule. Hicho ni chakula ambacho hakifai kwa sababu kimeunganishwa na nguvu za kuzimu.

 

Kama alivyokataa Danieli na wenzake kula vyakula vya Mfalme, ndivyo hata sisi tunapaswa kukataa kula vyakula vilivyo najisi kwa Jina la Yesu. Hata wewe utakapoletewa vyakula vya aina hiyo ndotoni, vikatae na usivile kwa Jina la Yesu. Endapo utakula vyakula vya aina hii, nguvu ya mapepo ndani yako huimarishwa. Mfano: vyakula vya majini ni ubani, udi, uji n.k. Udi ingawa utauona kidogo, unapochomwa, mashetani maelfu huhudhuria na kupata nguvu upya. Wewe unayekula chakula cha Mungu ambacho ni NENO LA MUNGU ndiye uliye sahihi, kwa sababu Yesu yu hai hata leo, na anataka kuingia kwako ili wale waliodhani umepigwa wajikute wao ndio wamepgwa, na waliodhani umepindishwa wajikute wao ndio wamepindishwa kwa Jina la Yesu.

Yapo makundi mbalimbali ya mashetani, mfano: majini, majoka, mizimu na miungu.


A.    KUNDI LA MAJINI

Ndiyo maana wapo watu wanaotumiwa matatizo ya uvimbe tumboni, ambayo kimsingi ni aina ya Majini ya Kiarabu. Unapoona unalishwa vyakula ndotoni, ujue hivyo ni vyakula vya kuimarisha viumbe vya kijini vilivyoko mwilini mwako.

UKIRI
Kwa Jina la Yesu, kila gonjwa lolote nililowekewa na ambalo si la kawaida ila ni la kishetani, naamuru teketea kwa Jina la Yesu. Ninakataa magonjwa, mimi siyo mdhaifu, mimi siyo maskini, niachieni kwa Damu ya Yesu. Kuanzia leo, nakataa vyakula vyenu vya kichawi, kwa Jina la Yesu. Amen


B.     KUNDI LA MAJOKA

Kundi la pili la mashetani ni Majoka. Kama ambavyo unawaona majoka ya mwilini, ujue kuwa yapo pia majoka ya rohoni. Endapo mtu ametupiwa majoka, anakuwa hana rafiki au mtu wa kumsaidia kwa sababu watu baadala ya kukuona wewe, watu huyaona majoka aliyokuzunguka. Yamkini wewe ni kijana au mtu mzima uliye na elimu kubwa tu ya Masters (shahada ya pili), lakini huwezi kupata kazi, kwa sababu popote utakapoomba kazi majoka haya yatakuzonga na kukufanya usionekane mtu wa maana. Ndiyo maana unaweza kumuona mwenye shahada moja akapewa kazi uliyoiomba wewe, pamoja na kwamba umemzidi kielimu. Kumbuka joka anayo sumu. Majoka yanaweza kukuachia sumu mwilini au rohoni mwako. Majoka ni mawakala wa mashetani. Dawa ya Nyoka ni Kumponda Kichwa. Leo tunatumia rungu la Bwana na kuyaponda majoka yote yaliyotumwa kwetu kwa Jina la Yesu.

C.    KUNDI LA MIZIMU

Mabibi na mababu waliokufa wakiwa na dhambi, huingia kuzimu. Lakini mambau na mabibi hawa wangekufa wakiwa wawmeokoka wanaingia Paradiso kuisubiria siku ya Bwana (). Mizimu huweza kukemewa na kuondoka. Jhata hivyo, mizimu wana tabia ya kuondoka na kurudi tena. Ni vyema kuwa karibu na Yesu ili kujitenga na mizimu.

D.    KUNDI LA MIUNGU

Haya ni mashetani yanayosimamia matatizo sugu (mfano magonjwa yasiyi na tiba n.k).

UKIRI
Leo najitenga na vyakula vya kiachwi, nawashambulkia majini,nashambulia magonjjwaa kwa Jina la Yesu. Amen Kwa wewe ambaye hujaokoka, fanya maamuzi leo kwa wewe ambaye hujaokoka ni rahisi kuvamiwa na kulishwa vyakula vya kichawi, na hivyo unapaswa kumkubali Yesu maishani mwako kwa maana ya kuokoka ili ukiwa upande wa Yesu ufanyike kiumbe kipya.

========== AMEN ========

KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godso
TEL: 0719 798778 (Sms only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/

 
Share:
Powered by Blogger.

Pages