GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH
[KANISA LA UFUFUO NA UZIMA]
GCTC → MOROGORO
JUMAPILI: 2 APRIL 2017
MHUBIRI: PASTOR Dr. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)
Mchungaji Kiongozi akitoa utangulizi wa somo leo, jumapili 2. April. 2017. |
Katika HESABU 13:1-33 ipo habari ya kutumwa
kwa wapelelezi 12 ambao Musa aliwatuma wakaipeleleze nchi ya ahadi waliyoahidiwa na Mungu kuiendea na
kuikalia kama urithi wao wa milele. Musa alitoa maelekezo ya jinsi ya kuipeleleza
hiyo NCHI YA AHADI waliyokuwa wakiiendea.
Kila kabila kati ya makabila yote 12 ya wana wa Israeli, aliteuliwa mtu mmoja
kuwa mpelelezi mwakilishi. Katika mstari wa 33, neno la Mungu linasema “Kisha,
huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona
nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”. Taarifa ya
wapelelezi hawa ilikuwa njema lakini ikambatana pia na taarifa mbaya (taarifa
zenye kujenga hofu kwa wengine). Kalebu na Joshua pekee ndiyo waliotoa taarifa
ya matumaini.
Wengine wote
walisema nafsi zao zilikuwa kama Panzi. Kwa nini watumie neno nafsi? Hii ni kwa
sababu Mwanadamu anazo sehemu kuu tatu: Roho Nafsi na Mwili. Imeandikwa katika MWANZO 2:7 “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi
ya uhai; mtu akawa nafsi hai”. Mungu alimfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi
ambayo tunayaita ni MWILI, na baada ya Mungu kuipulizia hili lisanamu
pumzi,ilifanyika NAFSI hai. Kwa hiyo nafsi ni muunganiko kati ya Roho iliyotoka
mbinguni, na mwili ambao ni mavumbi ya nchi. Nafsi haina umbile la kuonekana,
huwezi kuishika kama tushikavyo mwili. Pasipokuwepo mwili na aroho, hauwezi
kuiona nafsi. Ndiyo maana tunasema Mwanadamu ni Roho yenye
nafsi inayokaa ndani ya nyumba na hiyo nyumba ni mwili. Endapo jmtu akifa,
ni roho yake inakuwa imetengana na mwili.
Majeshi ya Bwana wakisikiliza kwa umakini somo la Kuishinda roho ya wapanzi, Ufufuo na Uzima Morogoro. |
Katika LUKA 9:24 imeandikwa “Kwa
kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza
nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha”. Kumbe nasi Nafsi
inaweza kuangamaia. Siku ya “Nafsi kuangamia”
ni pale roho ya mtu inapotengana na mwili wake. Utambulisho wa mwanadamu upo
katika nafsi. Huwezi kwenda mahali popote na kujitambuilisha kwa kusema “mimi
ni ile roho ya fulani”!!!. Kwa wazungu wanasema wanaenda kuvuna nafsi
zilizopotea (Soul winning). Hata katika ushuhudiaji ili watu waokoke,
tunachoenda kukihubiria ni ule muunganiko
wa mwili na roho ambao ni NAFSI. Ndiyo maana kifungo cha nafsi ndicho kibaya
kuliko vyote. Mashuleni kinachofundishwa ni nafsi siyo roho au mwili. Ndiyo
maana mtu akisoma sana na kubobea, ujuzi wa huyo mtu unakuwa umepandwa katika
nafsi yake. Na endapo mtu wa aina hii akifariki dunia, elimu na ujuzi wake
hauwezi kuhamishiwa au kuurithishwa kwa watoto wake.!!
Nafsi inazo idara
za Aina tatu: Nia (Mind), Utashi (Will),
na Hisia (Emotion).
1.
IDARA YA NIA
Ni idara ya kumfanya mtu kufikiria afanye nini!!.
Ili uweze kuishi maisha mazuri inabidi uwe mtu kufikiria. Kupitia idara hii,
mtu anaweza kufikiria na kufanya maamuzi fulani. WARUMI 12:2 imeandikwa hivi “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali
mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo
mema, ya kumpendeza, na ukamilifu”. Ili uweze kugeuzwa unapaswa kusikiliza
na kulisoma neno la Mungu kwa bidii
2.
IDARA YA UTASHI
Ni idara ya
kufanya maamuzi. Kupitia utashi, nafsi ya mtu hufanyya maamuzi magumu. Nyuma ya
utashi kunakuwepo na ile idara ya nia. Ukiona mtu anafanya mambo mabaya, ujue
shetani ameitega idara hii ya utashi.
3.
IDARA YA HISIA
Ni idara ndani ya
nafsi, ambapo mtu akeshafikiria na kuamua, hatimae huweza kuingiwa ama na ujasiri,
au woga, jazba, hasira n.k, na vyote hivi vimejaa katika idara hii.
Ndiyo maana katika
HESABU 13 mstari wa 33 “Kisha, huko tuliwaona Wanefili,
wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama
mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”. Kwa andiko hili ni dhahiri
kuwa, pamoja na kwamba ushuhuda wa ile nchi walikuwa nao kwa kubeba lile tawi
lenye kishada cha zabibu, lakini woga wa kuwaona wenyeji wa ile nchi uliwafanya
“wajione kama mapanzi”. Isingewezekana
kwa hao Wanefili wawaachilie wapelelezi hawa 12 (wanaojihisi ni mapanzi) eti waondoke
bila kudhurika.!! Katka HESABU 13 Mstari
wa 27 na 28 imeandikwa hivi “Wakamwambia
wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa
maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake. 28 Lakini watu wanaokaa katika
nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na
hayo tuliwaona wana wa Anaki huko.” Kuna watu wanaweza kukuletea
taarifa mbaya kwako, leo tuungane na Kalebu na kukataa taarifa zote mbaya juu
yetu kwa Jina la Yesu. Usikubali kutishwa kamwe na taarifa za madaktari
waliopima afya yako. Usitishwe na taarifa mbaya zenye kusema kwamba ukoo wako
ni wa watu wasiosoma zaidi ya darasa la 7. Wewe Unaye Bwana wa Mabwana - Yesu
Kristo, ambaye unakuwa naye siku zote akitembea na wewe, hivyo haipo sababu ya
mtu yeyote kukutisha tena, na usimhofu mtu yeyote kamwe kwa Jina la Yesu.
Mmojawapo wa watu wenye Roho ya Mapanzi akifunguliwa kwa mkono wa masihi wa Bwana, Ufufuo na Uzima Morogoro. |
Endapo kati ya
wapelelezi 12 ni wawili tu waliokuwa na ujasiri, ni udhihirisho kuwa wingi wa
taarifa siyo hoja ya msingi. Ndiyo kusema kwamba usitishwe na wingi watu
wanaotoa taarifa mbaya kwako. Tunasoma katika HESABU 13 Mstari wa 30 “Kalebu
akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana
twaweza kushinda bila shaka”. Wachawi wanaokutisha lakini nao watageuka
na kuwa chakula chako kwa Jina la Yesu. Hata Mfalme Ahabu alitabiriwa na
manabii zaidi ya 400, lakini taarifa zao zilikuwa potofu (fake news). Ni taarifa ya Mikaya pekee, Nabii wa Bwana wa
Mabwana ambaye alitabiri ukweli, na hakika kile alichokisema ndicho kilichotokea, kudhihirisha kuwa wingi wa
wanaotoa taarifa kwako au kukutabiria
siyo hoja bali uangalie kile asemacho Bwana wa Mabwana - Yesu Kristo juju ya maisha yako.
MTU ANAIPATA JE ROHO YA MAPANZI?
Roho ya mapanzi ni
roho inayopandwa na mashetani ndani ya mtu. Endapo roho ya panzi ikiingia ndani
yako, hata kile ulichokuwa unakiwaza kitabadilishwa nia yake. Mifano ya roho za
mapooza ni kama hii:-
·
Kile kitu
ulichokuwa unaweza kufanya, unaanza kusema huwezi kukifanya tena.
·
Pengine yupo mtu
ambaye Mumewe amemnunulia gari, lakini hata kuliendesha hataki au hawezi, na anaendelea
kupanda daladala na bodaboda,na anaweza kupata ajali humo.
·
Pengine Unakuwa
unavyo vyeti vya kitaaluma lakini kuomba kazi hutaki au unaogopa kuvitumia,
kwa kufikiria kuwa hauna sifa au
hautafanikiwa!!.
·
Pengine ni katika
Familia yenu, na mmejaliwa watoto, lakini kuwapelekea shule hutaki, na
unasubiri bibi yao aliyeko kijijini atoe ruhusa au ushauri wa nini kifanyike.!!
·
Pengine yupo Kijana
anayetaka kuoa, lakini anakuwa muoga kuelezea nia yake kwa mchumba anayelenga kumuoa.
Kila siku anakuwa na visingizio vipya vya kumfanya asifanye maamuzi hayo ya
kuchumbia.!!
Yote haya ni maroho ya mapanzi. Hofu ni roho ya mapanzi iliyoanza kupandwa kwa wale wapelelezi 10 wa Israeli ili kuwafanya wasikubali kuingia katika nchi ya Ahadi waliyopewa na Mungu.
UKIRI
Nakataa kwa Jina
la Yesu kuendelea na roho ya mapanzi ndani yangu. Ninakataa mimi siyo mdudu tena,
kwa Jina la Yesu.
|
Majeshi wakiziondoa Roho ya Mapanzi, Ufufuo na Uzima Morogoro. leo jumapili 2. April. 2017 |
Leo hii wapo wakristo wanaofanya maombi mbele za Mungu wakidhani ndiyo njia ya kunyenyekea wakisema “Mungu nisaidie, mimi ni kama funza tu, mimi ni takataka mbele zako, sina lolote baba.!!” Haya siyo maombi sahihi, kwa sababu ni mojawapo ya roho ya mapanzi. Leo tutayafukuza mashetani na majini yanayosababisha watu kujaa hofu na roho za mapanzi kwa Jina la Yesu. Kumbuka kuwa katika ZABURI 82:6 imeandikwa “Mimi nimesema, Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye juu, nyote pia.”. Kwamba Mungu anakuita wewe kuwa “sawa na Mungu”. Kwamba unapokuwa na Mungu ndani mwako, popote unapoenda ni Mungu ameenda na unakuwa sawa na Mungu. Kwamba ukiona kitu ni Bwana ameona, na ukisema kitu ni Bwana amesema.
Katika HESABU 14:1-9 imeandikwa (Mkutano
wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. 2 Kisha wana
wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia,
Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama
tungalikufa katika jangwa hili. 3 Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili
tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali
turudi Misri? 4 Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri. 5
Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la
wana wa Israeli. 6 Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune,
waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; 7 wakanena na
mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili
kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. 8
Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni
nchi yenye wingi wa maziwa na asali. 9 Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope
wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao
umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope.). Maisha haya ambayo Mungu anakupitisha sasa, ni mazuri mno na wachawi wanayaona na ndiyo
maana wanatafuta mbinu za kukuzuia usifikie zile ahadi za Mungu maishani mwako.
Leo tunatangaza kwamba, uvuli wa wale waliokutisha umeondolewa na watakuwa
chakula chako kwa Jina la Yesu.
Tunaiona hatari ya
roho ya mapanzi. Ni maombi yetu kwamba Bwana aiondoe roho ya mapanzi ndani
mwako kwa Jina la Yesu. Waliokutisha kwamba hauwezi kuanza biashara, au huwezi
kusoma elimu fulani, leo ukatae na kuwa kama Joshua na Kalebu kwa Jina la Yesu.
TUFANYE JE ILI KUISHINNDA ROHO YA MAPANZI?
Shetani anaweza
kugeuka na kuwa jambo lolote. Kwa hiyo ili tumshinde shetani na roho ya mapanzi
inatubidi tufanye mambo yafuatayo:-
1. Njia mojawapo ni kubadilisha jina. Ulikuwa unaitwa ‘mwoga’,
lakini sasa ujiite ‘shujaa’. Tunaona kuwa, wapo wapelelezi ambao Musa aliwabadilisha
majina yao. Ndivyo ilivyoandikwa katika HESABU
13:16 “Hayo ndiyo majina ya hao watu waliotumwa na Musa waende kuipeleleza
nchi. Na huyo Hoshea mwana wa Nuni, Musa akamwita jina lake Yoshua”.
Unapobadilishwa Jina unakuwa na mtizamo tofauti na wengine wote.
2. Kubadilisha Mtizamo wako. Unapaswa kukataa kuitwa lile
Jina la Awali. Ulikuwa huna hela ‘(maskini)’ lakini useme wewe kuanzia sasa ni ‘tajiri’.
Ulikuwa unaitwa ‘mgonjwa’, kwa sasa useme wewe ni ‘mzima’. Yale majina ya
kujiita ‘sisi wote ni maskini’ leo tuyakatae kwa Jina la Yesu.
3. Kung’oa Mafuta au Uvuli wa Utisho uliopo mbele yako.
Kuna ofisi zingine wapo maboss ambao huwa na uvuli wa aina hii, unaowafanya
watumishi waliopo chini yao kuwaogopa sana.
Leo ng’oa huo uvulin wa utisho unaowafanya waogopwe kwa Jina la Yesu.
UKIRI
Ninahama kwenye
ulimwengu wa roho wa kishetani, ninahamia ulimwengu wa roho wan Bwana Yesu.
Kuanzia leo ninaing’oa roho ya hofu kwa Jina la Yesu. Amen
|
Huwezi kujaribu
kupambana na shetani ukiwa ni mwenye dhambi. Kama upo mtu ambaye hujaokoka, leo
mpe Yesu maisha yako, ili utengeneze upya kwa maana ya kuokoka ili ukiwa upande
wa Yesu ufanyike kiumbe kipya.
========== AMEN ========
KWA MSAADA
ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow
us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: 0719 798778 (Sms
only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/