GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH
[KANISA LA UFUFUO NA UZIMA]
GCTC → MOROGORO
JUMAPILI: 19 MARCH 2017
MHUBIRI: PASTOR STEVEN NAMPUNJU (RP)
Kuishi kwako hadi
leo ni kwa sababu lipo kusudi la Mungu
la kukufanya uwe hai. Katika ISAYA 43:2
“Upitapo
katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha;
uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.” Hivi
ni kwa nini Mungu aahidi haya yote kwa ajili yako? Ni kwa sababu ipo sababu ya
Kimungu ya kukuokoa na mabaya yote ili lile kusudi lake la Kimungu la kukuumba liweze kutimia. Mfano mwingine ni wakati ule Yesu akikamatwa ili akahukumiwe, Petro aliutoa upanga wake na
kumkata mmojawapo wa wale maaskari na
kumkata sikio.!! Hata hivyo, Yesu
alimwambia Petro aurudiishe ule upanga alani mwake kwa sababu kama ingekuwepo haja
ya kufanya hivyo, Yesu angeamuru vikosi
vya jeshi la malaika toka mbinguni kuja na kumlinda!! Ni udhihirisho kuwa, Mungu anao malaika
walio upande wetu na ambao ni wengi kuliko majeshi ya wale walio upande wa adui
zetu.
Imeandikwa katika 2WAFALME 6:8-17 (Basi, mfalme wa Shamu alikuwa
akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo
changu kitakuwapo mahali fulani. 9 Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa
mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko
wanakoshukia Washami. 10 Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale
alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si
mara moja, wala si mara mbili. 11 Basi mfalme wa Shamu moyo wake ukamfadhaika
sana kwa ajili ya jambo hili; akawaita watumishi wake, akawaambia, Je!
Hamtanionyesha, ni mtu yupi miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli?
12 Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha,
yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo
katika chumba chako cha kulala. 13 Akasema, Enendeni, mkamwangalie aliko,
nipate kupeleka watu kwenda kumchukua. Akaambiwa ya kwamba, Tazama, yuko
Dothani. 14 Kwa hiyo akapeleka huko farasi, na magari, na jeshi kubwa; wakafika
usiku, wakauzingira mji ule pande zote. 15 Hata asubuhi na mapema mtumishi wake
yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na
farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu!
Bwana wangu, tufanyeje? 16 Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi
kuliko wale walio pamoja nao. 17
Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona.
Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima
kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.). Mfalme wa Shamu alikuwa amepanga kuivamia Israeli,
na kila mara siri ya uvamizi ule ile ikawa inavuja. Hiki ndicho kilichomfanya
Mfalme wa Shamu kuhisi maofisa wake wa jeshi kuwa wanahusika. Hata hivyo,
mipango yake hii ilikuwa wazi na dhahiri kwa Elisha, hata kama angeipanga
mipango hii akiwa chumbani mwake. Mfalme
wa Shamu alipoambiwa ukweli huu, ilibidi apange jeshi lake kuizingira nyumba ya
Elisha. Mtumishi wa Elisha alipoona jeshi limejaa nje ya nyumba yao, alimwambia
Bwana wake “Ole wetu” akimaanisha
kuwa ile vita ilikuwa siyo tu ya Elisha
peke yake bali ni ya wao wote.
Neno la Mungu
linasema, “Jeshi lijapojipanga kupigana nami, sitaogopa”!!!. Mtumishi wa
Elisha macho ya mwilini mwake yalikuwa yamefungwa asione, lakini pale Mungu
alipoyafungua macho yake na kuona, ghafla alitiwa nguvu kwa sababu majeshi ya
malaika waliowazunguka walikuwa wengi sana, na adui zao walikuwa pia wamezungukwa!!
Ndiyo kusema, Mungu wetu huwatuma malaika zake ili kutulinda, na hivyo huna haja
ya kuogopa. Na ndiyo maana pia imeandikwa katika WARUMI 8:31 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo
upande wetu, ni nani aliye juu yetu?”. Ijapokuwa Israeli ilikuwa na
jeshi lake, lakini Mungu alituma jeshi la malaika wa mbinguni kwa ajili ya
kumzingira Elisha na Mtumishi wake tu.!! Kwa nini? Hii ni kwa sababu ndani ya
Elisha lilikuwepo kusudi la kimungu la kuumbwa kwake.
Imeandikwa katika 2WAFALME 2:11-12..(Ikawa, walipokuwa wakiendelea
mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto,
likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. 12 Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu,
gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi
yake mwenyewe, akayararua vipande viwili.). Hapa tunaona tukio la gari la moto na farasi wa moto kwa pamoja yakimtenga Eliya na
Elisha. Ni maombi yangu kuwa, magari haya ya moto na farasi wa moto wa Mungu
yakija yakutenge wewe na balaa zote, mikosi yote na dhiki zote zilizoelekezwa kwako
na adui zako kwa Jina la Yesu.
Mamia ya Watenda kazi na Waumini wa Ufufuo na Uzima Morogoro wakifuatilia kwa makini Mahubiri 19/3/2017 |
Imeandikwa pia
katika 2WAFALME 6:17-19 (Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi,
mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye
akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto
yaliyomzunguka Elisha pande zote. 18 Na walipomtelemkia Elisha akamwomba Bwana,
akasema, Uwapige, nakusihi, watu hawa kwa upofu. Akawapiga kwa upofu sawasawa
na neno la Elisha. 19 Elisha akawaambia, Njia hii siyo, na mji huu sio,
nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa mtu yule mnayemtafuta. Akawapeleka
Samaria.). Maombi ya Elisha yalisababisha watu hawa kupigwa na Upofu.
Hata hivyo, upofu uliopigwa kwa haya Majeshi ya Washami hapa siyo ule upofu wa kimwili.
Ni akili zao zilipofushwa na kutoweza kujua kusudi lao. Roho ya upofu ikimwingia
mtu, atashindwa kuona fursa zilizoko mbele yake. Ndiyo maana watu hawa walitoka
sehemu sahihi aliyokuwepo Elisha waliyekuwa wanamtafuta, na kuelekezwa sehemu ingine
isiyo sahihi. Hata Adamu na Eva kilichotokea kwao ni kupofushwa fikra zao baada
ya kumsikiliza shetani na kula tunda lile walilokatazwa na Mungu wasile. Ndiyo
kusema kwamba upofu wa fikra ndiyo mbaya kuliko upofu wa macho ya mwilini.
Imeandikwa katika 2WAFALME 7:3-11…(Basi walikuwapo watu wanne wenye
ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe? 4
Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa
hapa, tutakufa vile vile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami;
wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu. 5 Basi wakaondoka kabla ya
mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kimo
cha Washami, kumbe! Hapana mtu. 6 Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha
Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo
cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa
Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi. 7 Kwa hiyo wakaondoka,
wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao,
na kimo chao vile vile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao.
8 Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja,
wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda
wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua
vitu, wakaenda, wakavificha. 9 Ndipo wakaambiana, Mambo haya tufanyayo si mema;
leo ni siku ya habari njema, na sisi tunanyamaza; mkingoja hata
kutakapopambazuka, madhara yatatupata; basi twende tukawaambie watu wa nyumba
ya mfalme. 10 Basi wakaenda, wakawaita mabawabu wa mji; wakawaambia, Tulifika
kituo cha Washami, na tazama, hapana mtu ye yote huko, wala sauti ya mtu, ila
farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na hema zao kama walivyoziacha. 11 Na
mabawabu wakaita wakawaambia watu wa nyumba ya mfalme.). Wenye ukoma
hawa walitengwa na jamii kwa kuwekwa nje ya mji wa Samaria. Siku ya habari
njema hupaswi kunyamaza. Maajabu ni watu
leo hii, badala ya kuwaambia watu wengine kuwa wanelekea kanisani ili kuwavuta
hao nao wapate ukombozi, watu hukaa kimya (hunyamaza) na kwenda kula vyakula
vya rohoni peke yao kila wiki kanisani!
Unapoamua
kujihatarisha kwa wakati mwingine ndiyo njia iliyo sahihi ya kuokoa maisha
yako. Nje ya lango walikuwepo wakoma wengi sana, lakini ni wale wakoma wanne tu
walioamua kujihatarisha, na kupitia ujasiri wao habari zao zimeandikwa hadi
leo. Wakati mwingine shida huwa haiishi hadi pale utakapochukua hatua. Mungu
huwa anamsaidia mtu aliyeamua kuchukua hatua. Meshaki, Shedraki na Abednego
walipochukua hatua kwa kukataa kuiabudu miungu mingine ingawa walihatarisha
uhai wao kwa imani waliyokuwa nayo kwa Mungu wao, lakini hata ndani ya tanuru
la moto Mungu aliingia pamoja nao na kuwaepusha na madhara ya ule moto kwa Jina
la Yesu.
Ndani ya Ngome za Jeshi
la Washami zipo baraka na nyara zako. Kama huwezi kulivamia Jeshi la Washami
hutaweza kujipatia chakula wala kuupata wokovu kwa Taifa lako. Ukichukua hatua,
Mungu huweka ulinzi kwako. Danieli naye
alichukua hatua, na kwa kuwa alimjua Mungu anayemtumikia, hata mfalme alimtia
moyo kwa kusema “Mungu wako unayemtumikia atakuepusha na simba hao wakali”, na
ikawa hivyo.
UKIRI
Kwa Jina la
Yesu, kuanzia leo na kuanzia sasa, Nazilazimsha kazi zote za mashetani ziharibiwe
zote leo kwa Damu ya Yesu. Naifungua nafsi na roho yangu kwa Jina la Yesu.
|
Mungu kwetu (Ufufuo na Uzima Morogoro) huabudiwa katika ROHO na KWELI, na ndivyo ilivyokuwa Jumapili 19/3/2017 |
Katika 1YOHANA 4:4 imeandikwa “Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu
nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye
katika dunia”. Tunajifunza kuwa,
kumbe yapo makundi mawili yafanyayo kazi tofauti, kundi la aliye ndani yetu na linguine
la aliye katika dunia hii. Kwa watoto wadogo wanaweza kushinda kwa sababu aliye
ndani yao ni mkuu kuliko wa aliye katika ulimwengu huu.
Katika YOHANA 12:19 imeandikwa “Basi
Mafarisayo wakasemezana wao kwa wao, Mwaona kwamba hamfai neno lo lote;
tazameni, ulimwengu umekwenda nyuma yake”. Kwa upande wa Mafarisayo,
hawakupenda kuona ulimwengu wote unamwendea Yesu Kristo. Ulimwengu wote ulikuwa
upande wa Yesu. Kuna watu leo wanakuchukia wewe tu eti kwa sababu kiongozi wako
kazini anakuwa upande wako.!! Na katika YOHANA
12:31 imeandikwa “Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu
wa ulimwengu huu atatupwa nje.” Yesu
alijua kuwa mkuu wa ulimwengu huu
yupo, kwa sababu yeye Yesu alitokea mbinguni na duniani hapa siyo mahali pake.
Tena imeandikwa pia katika YOHANA 14:30
(Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja
mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.). Hivi ni kwa nini Yesu aliyasema haya? Ni kwa sababu Yesu
anajua kuwa mkuu wa ulimwengu huu hana kitu kwake na kwamba wapo malaika
waliokuwa upande wake.
Imeandikwa katika 2NYAKATI 32:7-8 (Iweni hodari, na wa moyo mkuu,
msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi
yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja
naye; 8 kwake upo
mkono wa mwili; ila kwetu yupo Bwana, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania
mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda.). Biblia inatuambia tusiogope, tuwe hodari na kuwa na
moyo mkuu. Wako watu ambao ili waupate msaada, wanao mkono wa mwilini (pengine
serikali yao, wachawi, mizimu n.k.). Tukumbuke kuwa Bahari ya Shamu ilifanyika
kikwazo kwa Musa na wana wa Israeli kutojua njia ya kuelekea nchi ya ahadi. Usipokuwa
hodari na kuwa na moyo mkuu utajikuta unageuka na kutaka kurudi nyuma. Ipo nchi
ya ahadi mbele zako, lakini shetani hataki uifikie hiyo nchi, na ndiyo maana anakuwekea
Bahari ya Shamu kukuzuia. Mungu naye ameachilia watumishi wake ili kukusaidia
tena kwa Jina la Yesu. Hata hivyo ili ufanikiwe, na malaika hawa kukusaidia ni lazima uwe hodari
na kuwa na moyo mkuu. Ni vizuri kusimama imara ili kuuona wokovu wa Mungu wako kwa Jina la Yesu. Ukiwa na
shida suluhisho siyo kurudi nyuma. Ukiwa
na moyo mkuu, hutaogopa matukio makubwa yatakayotokea maishani mwako. Mungu anayo miujiza yake kwako, lakini na kwa
wale wenye moyo mkuu hawajiulizi maswali kwa sababu wanamwamini Mungu.
Platform wa Ufufuo na Uzima Morogoro wakimwimbia Bwana wanaimba kwelikweli, na wakiwa katika Kuabudu, vivyo hivyo! |
Chanzo cha taabu
au dhiki uliyo nayo inatokana na mashetani kukiwinda kile kitu alichokiweka
Mungu rohoni mwako. Mungu kwa wakati mwingine anaruhusu matatizo yakupate ili
kuwafanya wengine waokoke. Usiogope! Uwe na Moyo Mkuu!! Daudi alipoona Goliathi
anatukana majeshi ya Bwana, aliuliza “Ni kitu gani ambacho atakayemuua huyu
mfilisti atapatiwa?” Ni kwa sababu Daudi alijua kuwa baada ya kumuua Goliathi
Mtukanaji (adui zako, mashetani, wachawi, majini n.k) kutakuwepo na malipo
ambayo wewe uliyemuua utapatiwa katika Jina la Yesu.
Jeshi la Washami
waliizingira nyumba ya Elisha katika ulimwengu wa mwili. Leo hii katika
ulimwengu wa roho, yapo majeshi ya rohoni yanayoweza kukuzingira, lakini kama
ilivyotokea kwa mtumishi wa Elisha, siyo rahisi kuyaona majeshi ya rohoni.
Ndiyo maana wapo watu husema, ilikuwa je nimekaa na shida zangu hizi miaka yote
hii na sikuweza kuja hapa Kanisani Ufufuo na Uzima? Ni kwa sababu shetani
anakuwa amepofusha macho yako ya rohoni. Hawa ndiyo watu ukiwashuhudia waje
kanisani kuombewa husema wanazo dini zao!!. Watu hawa wa dini wanakuwa tayari
kwenda kwa waganga wa kienyeji ingawa
kimsingi hiyo nayo siyo dini yao.
UKIRI
Kwa Jina la
Yesu, mimi ninazingirwa na moto wa Bwana. Walioniteka watekwe wao. Walionizingira wazingirwe wao. Kuanzia leo
nageuka kuwa mwali wa moto. Kuanzia sasa ninakataa kudhulumiwa haki zangu,
kwa kuwa imeandikwa nitakuwa kichwa wala siyo mkia, katika Jina la Yesu.
|
Umati wa Watendakazi na Waumini wa Ufufuo na Uzima Morogoro wakisikiliza maelekezo ya Maombi ya Jumapili 19/3/2017 |
Ili ufanikiwe
itategemea sana ni nani aliye upande wako. Katika 1YOHANA 4:4 “Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu
nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye
katika dunia”. Kumbe ushindi wa
mtu hutokana na yule aliyeko ndani yake. Shida ulizo nazo zinatokana na wewe
kutokuwa na mwenye nguvu yaani Yesu Kristo maishani mwako. Ukimpokea Yesu ndani
mwako, atakuponya na kukufungua kutoka kwenye shida uliyo nayo, kwa sababu Yesu
atakuwa ndani yako. Hata kama uliwahi kuombewa na mamia ya wachungaji na shida
yako ikabaki pale pale, suluhisho lako siyo maombi ya wachungaji kwa sababu
wachungaji hawa hurudi majumbani mwao, ila ukimfanya Yesu awe rafiki yako na kuingia ndani mwako,
siku zote YESU atakuwa pamoja nawe. Cha
kufanya leo kwa wewe ambaye hujaokoka, ni kumkubali Yesu maishani mwako kwa
maana ya kuokoka ili ukiwa upande wa Yesu ufanyike kiumbe kipya.
========== AMEN ========
KWA MSAADA
ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow
us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: 0719 798778 (Sms
only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/
© Media and Information Ministry
GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH,
(Kanisa la Ufufuo na Uzima)
Mkundi - Morogoro
Tel: +255719612874 / +255713459545
|