Thursday, April 27, 2017

MILIMA YA WACHAWI YA UHARIBIFU


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)

{KANISA LA UFUFUO NA UZIMA → MOROGORO}

 

JUMAPILI: 23 APRIL 2017

 

MHUBIRI:  PASTOR Dr. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)

 

 

Kwa kawaida mlima ni mahali pa juu palipoinuka sana kuliko tambarare zote. Mahali palipoinuka pa aina hii ni rahisi kuona tambarare zingine zote, na hivyo wachawi hupendelea kutumia maeneo kama hayo ili waweze kuona mbali na kuleta uharibifu kwa waliowakusudia. Katika Kitabu cha 2WAFALME 23:13Na mahali pa juu palipokuwapo mbele ya Yerusalemu, palipokuwa upande wa kuume wa mlima wa uharibifu, alipopajenga Sulemani, mfalme wa Israeli, kwa Ashtorethi, chukizo la Wasidoni, na Kemoshi, chukizo la Moabu, na Milkomu, chukizo la wana wa Amoni, mfalme akapanajisi”. Ndiyo maana hata mchawi Balaamu alitumia mahali pa aina hii ili kutaka kuwalaani Israeli na kuleta uharibifu kwao. Ndivyo ilivyoandikwa katika HESABU 23:13Balaki akamwambia, Haya! Njoo, tafadhali, hata mahali pengine, na kutoka huko utaweza kuwaona; utaona upande wa mwisho wao tu, wala hutawaona wote, ukanilaanie hao kutoka huko”.

 

Mahali pa juu hutumiwa sana na wachawi, waganga wa kienyeji, wasoma nyota na wenzao kwa sababu ya kuinuka kwake, na pia ni sehemu ya kuweza kuwaona watu wote na nyumba zao na hivyo kuwa rahisi kufanya uharibifu. Na hata Yesu mwenyewe alipojaribiwa, shetani alimpandisha hadi kwenye kinara na kumuonesha miliki na fahari zote za hii dunia. Majeshi mbalimbali pia huweza kutumia mahali pa juu (mfano mlimani), katika kuwaona adui zao na kupanga mbinu za kupigana nao.

 

JE WACAHWI WAMETAJWA KATIKA BIBLIA.

Maandiko yanasema katika KUTOKA 22:18 “Usimwache mwanamke mchawi kuishi”. Kumbe basi ni dhahiri kuwa wachawi wapo na wameandikwa katika Biblia maeneo mbalimbali, na mifano yake ni kama ifuaatavyo:-

1.      Imeandikwa katika MATENDO 13: 6Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake BarYesu;” huyu kwa Jina lake tu “BarYesu” inaonesha alikuwa MCHAWI pamoja na kuwa analo jina la Kikristo.

 

2.      Mfano wa pili ni katika MATENDO 8:9Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. 10 Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu. 11 Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake.” Huu nao ni ushahidi mwingine kuwa, wachawi wapo, tena wenye majina ya Kikristo kama hili la “Simoni”. Mtu huyu Simoni aliwashangaza watu kwa namna alivyotumia njia za kichawi (pengine alikuwa akiruka angani kwa kutumia ungo, au kutembelea mguu mmoja n.k). Leo tutawafyeka wachawi wote kwa Jina la Yesu, wale wanaojihudhurisha makanisani lakini kumbe ni wachawi.

 

 ZIPI NI TABIA ZA KUWAFAHAMU WATU WACHAWI?

1.      Wachawi wote duniani kote wamejaa hila.  Mchawi anaweza kukulaghai kwa kukupa vitu fulani-fulani akikudanganya kuwa vitakusaidia lakini kumbe siyo chochote. Kila alicho nacho mchawi kimejaa hila: mwingine utamkuta usoni mwake kumejaa “ndita” pamoja na kuwa siyo mzee, kwa hivyo ujue kuwa mtu wa aina hiyo ni mwenye hila tu.!!

 

2.      Wachawi wote wamejaa uovu na uharibifu. Mungu amelenga mtu apate baraka, mafanikio, afya, maisha mazuri n.k. Hata hivyo mtu muovu analenga kuona uharibifu, akuone unakuwa maskini, umekuwa mgonjwa n.k. Kwa sababu wachawi ni mawakala wa mashetani, lazima watekeleze malengo ya kishetani kama ilivyoandikwa katika YOHANA 10:10Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.

 

3.      Wachawi wote kwa asili ni wana wa ibilisi.  Ndiyo maana Biblia inasema kuwa watoto wa ibilisi ni dhahiri na watoto wa Mungu ni dhahiri. Na katika YOHANA 1:12Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;

 

4.      Wachawi wote ni adui wa haki yote. Kwa kawaida, pengine mtu alitakiwa apate kazi lakini kupitia wachawi wanasababisha jambo hili lisitokee. Ilikuwa mtu aolewe lakini lakini miaka itakujja na kupita bila kuolewa kwa sababu ya wachawi kuingilia kati maisha ya mtu huyo.

 

5.      Wachawi wote hupotosha njia za Bwana zilizonyooka. Pengine kupitia njia hii mtu angeweza kufanikiwa kibiashara, lakini kupitia wachawi, mtu wa aina hii hupata hasara na kuacha biashara. Mfano mmojawapo wa Kibiblia ni wa yule mama aliyepindana mgongo kwa miaka 18. Utakumbuka kuwa watu wa dini (Masadukayo) walikasirika sana kwa kuwa Yesu aliunyoosha upya mgongo wa huyu mama siku ya Sabato.!!  Kwa kawaida watu wote wanaokasirika wakimuona mtu mwingine amefanikiwa ujue ni wachawi tu, hata kama wanaonekana ni watu wa dini sana.

 

6.      Wachawi hupindisha maisha. Pengine Mtu ulitakiwa uwe na mafanikio lakini wachawi wakayapindisha maisha yako, au wakapindisha afya na njia zako za mafanikio zilizonyooka n.k. Pengine mtu alipaswa kuwa daktari lakini leo hii wachawi wameipindisha hatima yake na matokeo yake mtu huyo anaishia kufanya kazi ya bodaboda.!! Kumbuka kuwa Mungu akikupa baraka zake anabariki kila kitu utiacho mikono yako kufanya. Hata hivyo, kama umeanza shughuli ya bodaboda na kuona miaka inasonga mbele bila ongezeko la kupata bodaboda nyingine ujue tayari ulipindishwa na hawa wachawi na hivyo lazima uhame kutoka kwenye huo mpango wa kichawi kwa Jina la Yesu.

 

Mfano mwingine ni pale ambapo wachawi wakimuona kijana anayesoma mwenye bidii sana darasani na ambaye kila mara anafaulu masomo yake huipindisha hatima yake ya kimasomo. Wachawi hawa watafanya mbinu zote, na mwishowe kijana wa aina hii taratibu huanza kufeli mitihani yake, kuwa mgonjwa au kushindwa kabisa kuona ubaoni n.k

 

7.      Kutia moyo wa kuacha. Imeandikwa katika MATENDO 13:6-12. (Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake BarYesu; 7 mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu. 8 Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. 9 Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, 10 akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? 11 Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazungukazunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza. 12 Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.). Ndivyo ilivyo hata leo. Pengine mtu alikuwa amepanga kuoa ndani ya mwaka huu lakini muda wa kufanya maamuzi ukifika mtu huyo ataahirisha kila mara. Kuna watu wanawekewa moyo wa kuacha kazi, moyo wa kuacha ndoa, moyo wa kuacha masomo, moyo wa kuacha huduma, moyo wa kuacha kilimo n.k.

 

Wapo watu wakiwekewa moyo wa kuacha, huweza kufanya maamuzi ya ghafla, bila kutafakari na kujikuta wanaandika barua ya kuacha kazi ndani ya saa 24. Hata hivyo watu wa aina hii hurudiwa na akili zao punde tu baada ya kukabidhi barua zao kwa viongozi wao makazini na kuruhusiwa kuondoka. Wakirudi kuomba msamaha, maboss wao huwaambia haiwezekani kwa sababu barua ya kuacha kazi waliyojiandikia ilishapelekwa kwa viongozi wa juu zaidi.!!

 

UKIRI
Ewe moyo wa kuacha niachie leo kwa Jina la Yesu. Moyo wa kuacha kazzi, moyo wa kuchukia vitu vyangu mwenyewe, leo naung’oa huo moyo wa kuacha kwa Jina la Yesu. Moyo  wa Jiwe ng’ooka kwa Jina la Yesu. Amen

 

Hizo tu ni baadhi ya tabia za wachawi, na zinafanana duniani kote. Hata hivyo tabia zingine za wachawi zilizosalia tutamalizia kuzijadili katika ibada zingine wiki hii.

 

Yesu Kristo mwenyewe alitupa njia nzuri sana ya kuwabaini watu wote waovu ambao kwa nje hujifanya kuwa ni wema lakini kumbe mioyoni mwao ni mbwa-mwitu. Tunasoma katika MATHAYO 7:15-18… (“Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwamwitu wakali. 16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? 17 Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. 18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri”). Ndiyo maana katika maandiko hapo juu tumeshuhudia kuwepo kwa watu wenye majina ya Kikristo lakini kumbe ni wachawi maarufu tu mitaani kwao. Unaweza kumuona mtu mwenye sura nzuri na ukampenda ukataka kuoa au kuolewa naye, lakini kumbe huyo kwa ndani ni mbwa mwitu mkali.

 

NAMNA GANI WACHAWI HUFANYA KAZI YA KUHARIBU MAISHA YA MTU?

Njia wanazotumia wachawi kuharibu maisha ya mtu, ni kama zifuatazo:-

1.      Wachawi Hupanda juu mahali palipoinuka na kutamka laana zao: Mahali palipoinuka ni vituo vya kichawi vya kufanya uharibifu kuweza kurusha laana zao. Wachawi wakiwa milimani hufanya hivyo ili waweze kurusha laana zao kwa ufanisi na huku wakiwaona walengwa wao. Ndicho alichokifanya Balaki pale alipomuajiri Balaamu, katika HESABU 23:13Balaki akamwambia, Haya! Njoo, tafadhali, hata mahali pengine, na kutoka huko utaweza kuwaona; utaona upande wa mwisho wao tu, wala hutawaona wote, ukanilaanie hao kutoka huko”. Wachawi wanaweza kutamka laana zote kwako, wakitaka usifanikiwe lakini hata hivyo Biblia inasema katika MITHALI 26: 2Kama shomoro katika kutangatanga kwake, Na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu”. Leo tutaomba ili  kila aliyepanga kutulaani, kinywa chake kibatilishe laana zao na badala yake wajikute wanatamka baraka kwetu kwa Jina la Yesu.

 

2.      Wachawi Hukutenga na hatima ya mafanikio yako: Kazi nyingine ya wachawi ni kumtenga mtu na mafanikio yake. Kwa njia hii, wachawi hutengeneza mlima kati ya mtu na njia yake ya mafanikio. Mathalani  milima hii ya rohoni huwekwa kati ya mtu anayetaka kuoa na mtu anayetaka kuolewa, kati ya anayeajiri na mwajiriwa, kati ya daktari na mgonjwa au kati ya mwenye msaada na anayeuhitaji msaada ili wawili hawa wasionane kamwe, wawe wametengana. Pengine mtu wa kukusaidia anakuwepo lakini mlima wa rohoni unapokuwepo mtu huyu hawezi kufurukuta kwa sababu hauonekani. Pengine kazini haupandishwi cheo kwa muda mrefu sasa, cha kufanya ni kusawazisha vilima vilivyowekwa mbele yako. Pengine hauoi au hauolewi lakini siri kubwa ili uweze kuondoka kwenye hiyo shida ni kusawazisha vilima vyote vilivyowekwa mbele yako. Leo tutasawazisha kila vilima vilivyoinuka mbele yetu na kufanya vyote tambarare kwa Jina la Yesu.

 

3.      Wachawi Hukuweka kwenye milima ya aibu: Kwa njia hii, wachawi humfanya mtu aliyeokoka akose chakula, aishi kama ombaomba, akose kazi, akose mapato n.k. Mtu wa aina hii, baadae huanza kusakamwa na familia yake wakimsema vibaya kwamba tokea alipookoka amekuwa hafanikiwi tena. Yesu Kristo vivyo hivyo alisulubiwa juu kilimani pale Golgotha ili watu wote wanaopita njia ile waione aibu yake na kumzomea.!! Leo tunayo habari njema kwako, kwamba pamoja na aibu hii kubwa iliyopandwa juu yako na hata kama imekomaa, tutabomoa milima yote ya kichawi inayoleta aibu kwako, na wale waliokuona haufai waanze kukuona unafaa tena kwa Jina la Yesu.

 

Endapo katikati yetu leo yupo mtu ambaye hajaokoka, ni fursa pekee kwako kumpa Yesu maisha yako, ili uwe na kibali cha kuivamia milima ya kichawi na kuisawazisha yote iwe tambarare tena kwa Jina la Yesu. 

 

========== AMEN ========

 

KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:

FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia

Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson

Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson

TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)

BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/
Share:
Powered by Blogger.

Pages