Sunday, May 14, 2017

MATUKIO YA KUTENGENEZWA NA SHETANI



GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)
{KANISA LA UFUFUO NA UZIMA → MOROGORO}

JUMAPILI: 14 MAY 2017

MHUBIRI:  PASTOR DR. GODSON ISSA ZACHARIA  (SNP)



Mch. Dr. Godson Issa Zacharia akifundisha katika ibada ya leo 14/05/2017


Unapoyaona matukio mbalimbali yakitokea hapa duniani, ujue kuwa kipo chanzo chake. Mengi  ya matukio haya ni ya kichawi.  Mathalani uonapo ajali zinazochukua uhai wa watu wengi kwa pamoja, hupaswi kukimbilia kusema eti huo ni uzembe wa dereva.!!! La hasha. Mengi ya matukio hayo ni yale ya kutengenezwa. Hata hivyo, Watu wa dunia hii husema ni matukio ya kawaida, lakini kumbe sivyo ilivyo. Dunia imekuwa kama vile imevishwa nguo, na kuipofusha macho yake, na kuwafanya watu waliomo duniani wasielewe ukweli wa kinachoendelea. Ni Bahati mbaya kuwa haya matukio yanaonekana kama ya kawaida, na hata mtu ukijaribu kuwafundisha  watu  wa dunia hii  hawaamini ukweli halisi wa haya matukio haya ya kichawi.

Ndiyo maana imeandikwa katika 2KORINTHO 4:3-4 (Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; 4 ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.).  Dunia hii ina mungu wake ambaye ni shetani, ambaye anapofusha fikra za watu ili wasiamini. Ukiwaambia watu kuwa haya ni matukio ya kutengenezwa na shetani, wanadamu wa leo hawaamini kabisa. Endapo wewe utapatwa na matukio ya ajabu ajabu, usikimbilie kuungana na watu wa dunia kuyashabikia. Mathalani pindi upwatapo na ugonjwa fulani, ingia kwanza magotini kufanya maombi kabla ya kukimbilia hospitalini. Hatusemi kuwa mtu uuguapo usiende hospitalini, la hasha.  Unapoomba kabla ya kukimbilia matibabu hospitalini inakuwa ni njia nzuri ya kulijaribu hilo tukio la ugonjwa kujua kama ni la kutengeneza au la!!!

Imeandikwa katika MATHAYO 7:15 (Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwamwitu wakali.). Kama wanadamu wanaweza kuvaa mavazi  ya uongo, ujue kuwa hata dunia nayo inao  uwezo huo huo pia. Kama dunia imevaa mavazi ya mbwa mwitu, leo lazima tuivue dunia nguo zake ili tujue ukweli wa kilichomo ndani yake katika Jina la Yesu.




Umati wa watu wakisikiliza neno la Mungu mapema leo. 14/5/2017 katika nyumba ya Ufufuo na Uzima Morogoro.




1.      MAFURIKO YA KISHETANI
Katika Biblia, yapo matukio kadhaa ya kutengenezwa, yakiwemo mafuriko. Imeandikwakatika UFUNUO  12:1- (1 Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili. 2 Naye alikuwa ana mimba, akilia, hali ana utungu na kuumwa katika kuzaa. 3 Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba. 4 Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake. 5 Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi. 6 Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambapo ana mahali palipotengenezwa na Mungu, ili wamlishe huko muda wa siku elfu na mia mbili na sitini.). Huyu  ni mwanamke aliyekuwa anajiandaa kujifungua mtoto. Joka (ambaye ni shetani) alikuwa karibu ili kummeza mtoto huyu akeshazaliwa. Ndicho kinachotokea hata leo mahospitalini. Wamama wanapoteza watoto wao, na watu wanaanza kusema, BAHATI MBAYA.!!! Hiyo siyo bahati mbaya, bali ni matukio ya majoka (mashetani) kumeza watoto wale wanaoonekana kuwa watakuwa maarufu sana duniani endapo wangezaliwa na wakawa watu wazima. Tunajifunza kuwa, mashetani wanaweza kula watoto, au kula biashara, kula ndoa, kula kazi n.k, lakini ukimtegemea Bwana atakuvusha kama alivyofanya kwa usalama wa mtoto huyu aliyezaliwa na huyu mwanamke. Hata Yesu Kristo pia wakati wa kuzaliwa, Yusufu alipewa jukumu la kumtorosha hadi Misri ili asiuliwe na Herode.

Shetani huwameza pia watoto nyakati za kuzaliwa kwao. Imeandikwa katika UFUNUO 12:13–16 (Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume. 14 Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo. 15 Nyoka akatoa katika kinywa chake, nyuma ya huyo mwanamke, maji kama mto, amfanye kuchukuliwa na mto ule. 16 Nchi ikamsaidia mwanamke; nchi ikafunua kinywa chake, ikaumeza mto ule alioutoa yule joka katika kinywa chake.). Tunamuona shetani akimuudhi mwanamke aliyemzaa mtoto, kwa sababu kilichozaliwa kina mamlaka ya kumponda shetani kichwa. Tunajifunza kuwa kumbe shetani anaweza kutapika maji ya mafuriko kama mto, na watu wakayaona ni mafuriko ya maji, kumbe ni mpango wa kishetani. Hata leo hii, mafuriko yanayoonekana kila mahali hapa nchini siyo kwamba yote ni matukio ya kawaida ya kijiografia. Baadhi ya Mafuriko yameandaliwa na yule muovu shetani, na kupumbaza akili za wanadamu ili wayaone kuwa ya kawaida. Na mbaya zaidi, ni pale baadhi ya Wakristo huyapokea kwa mikono miwili na kujifariji kwa kusema “BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA”. Ni kweli kuwa, Bwana ndiye aliyetoa lakini lazima tuhoji  YULE ANAYETWAA,  tusiamini  amini  sana  anayetwaa, kwa sababu siyo mpango wa Mungu kutwaa kila akupacho.!!

2.      UPEPO  WA KISHETANI
Katika AYUBU 1:1-12 tunasoma simulizi ya Ayubu na matukio mbali mbali yaliyompata. Mfano  ni katika AYUBU 1:18-19 (Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wanao na binti zako walikuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa; 19 mara, tazama, upepo wenye nguvu ukatoka pande za jangwani, ukaipiga hiyo nyumba pembe zake nne, nayo ikawaangukia hao vijana, nao wamekufa; na mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.). Tunaliona tukio la upepo ulioipiga nyumba ya Ayubu pande zote 4 (Mashariki, Magharibi, Kusini na Kaskazini) na kusababisha vifo vingi, wakiwemo watoto 10 wa Ayubu. Kwa kawaida, upepo  hutokea upande mmoja kwenda upande mwigine. Siyo jambola kawaida upepo kutokea pande zote nne. Lakini katika mazingira haya, shetani ndiye aligeuka na kuwa upepo. Ndiyo maana tunasema huu ulikuwa upepo wa kishetani.

Endapo tukio hili la upepo nyumbani kwa watoto wa Ayubu lingetokea leo hii hapa Tanzania, ni dhahiri kuwa vyombo vyote vya habari vingelitangaza kama kawaida  yao, na kuelezea jinsi upepo ulivyokuja na madhara yaliyotokea, na hata pengine Mamlaka  ya Hali ya Hewa wangetupatia  jina la huo upepo (wangeweza kuuita ni tsunami, au torndo n.k.). Siku moja Yesu aliwahi kuukemea upepo walipokuwa kwenye chombo majini na mara moja ile dhoruba ya upepo ikanyamaza kimya. Leo Mungu akupe uwezo wa kunyamazisha pepo zote zinazofuatilia maisha yako, ndoa yako, biashara yako, masomo yako yote kwa Jina la Yesu. Upepo wa kishetani unaweza ukafukuza watu, hata wale waliotaka kukusaidia wasiweze. Pengine kuna mtu alikuwa akusaidie, lakini mara mtu huyo anakufa ghafla na ule msaada uliotegemea kwake unaishia hapo hapo.

Swali la kujiuliza hapa kuhusiana na Upepo wa nyumbani kwa Ayubu ni:- JE, KWA NINI  HUYU MLETA TAARIFA HAKUFA KWENYE HILO TUKIO? Ni wazi kuwa, mleta taarifa naye alikuwa wakala wa shetani, aliandaliwa makusudi kwa ajili ya kupeleka taarifa mbaya. Shetani anaweza kugeuka na kuwa kitu chochote kile apendacho. Ndiyo maana Imeandikwa katika WAFALME 22:20-21 (Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee RamothGileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. 21 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya.). Shetani huyu huyu aliyehudhuria kikao mbinguni na kusababisha matukio kwa Ayubu, ndiye anayehudhuria kikao na kupanga kwenda kumdanganya Mfalme Ahabu.


UKIRI
Ewe mleta taarifa mbaya, taarifa za vifo, taarifa za magonjwa, leo ninakufyeka kwa Jina la Yesu. Amen







Mchungaji Kiongozi Dr. Godson Issa Zacharia, akimfungua  mtu katikati ya Ibada leo Jumapili 14/5/2017.

3.      TUKIO LA  UBUBU NA UZIWI WA KISHETANI
Unaweza kumuona mtu ni bubu au kiziwi ukawaza kuwa hiyo ni hali ya kawaida tu kwa wanadamu, lakini kumbe nyuma yake yupo shetani aliyeesababisha. Imeandikwa katika MARKO 9:14-27 (Hata walipowafikia wanafunzi, waliona mkutano mkuu wakiwazunguka, na waandishi wakijadiliana nao; 15 mara mkutano wote walipomwona walishangaa, wakamwendea mbio, wakamsalimu. 16 Akawauliza, Mnajadiliana nini nao? 17 Mtu mmoja katika mkutano akamjibu, Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo bubu; 18 na kila ampagaapo, humbwaga chini, naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda; nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo, wasiweze. 19 Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu. 20 Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaanguka chini, akagaagaa, akitokwa na povu. 21 Akamwuliza babaye, Amepatwa na haya tangu lini? Akasema, Tangu utoto. 22 Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize; lakini ukiweza neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia. 23 Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye. 24 Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu. 25 Naye Yesu akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena. 26 Akalia, akamtia kifafa sana, akamtoka; naye akawa kama amekufa; hata wengi wakasema, Amekufa. 27 Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua naye akasimama.). 

Hapa tumemuona huyu kijana ambaye ni bubu na kiziwi tokea kuzaliwa kwake. Matukio ya kishetani yaliyompata kijana huyu mara kwa mara ni kama vile:-
·        Kubwagwa chini. Mapepo haya yalikuwa yakimdondosha kijana kwenye  moto na  maji, na lengo likiwa ni kumfanya afe, na baadae akeshakufa watu wataliona hilo tukio kama  la kifo  cha maji au  moto. Yote haya ni mapepo ndani mwake yaliyokuwa yanasababisha haya.
·        Kijana kutokwa povu na kusagasaga meno.
·        Mapepo pia yalisababisha ukondefu kwa huyu kijana, na kumfanya mtu hata kama anakula vizuri tu lakini asiongezeke uzito. Nyakati nyingine unapomuona mtu anatafuna vitu usingizini, fahamu kuwa huyo ni pepo ndani mwake anayemlisha vyakula ndotoni. Unapaswa kuomba kwa bidii na kuyaharibu mapepo ya aina hii kwa Jina la Yesu.
Hata hivyo kwa kuwa Yesu aliliona hilo tukio katika ulimwengu wa roho, tunamuona Yesu akimshika mkono na kumponya.



Showers of Glory Morogoro wakimwimbia na kucheza mbele za Bwana leo Jumapili 14/5/2017



4.      TUKIO  LA UDHAIFU WA KIPEPO KWA MIAKA  18
Katika LUKA 13:10-16 imeandikwa (Siku ya sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo. 11 Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. 12 Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. 13 Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu. 14 Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. 15 Lakini Bwana akajibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je! Hamfungui ng'ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha? 16 Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato?). Huyu pepo wa udhaifu aliingia katika mwili wa huyu mama, na kusababisha mgongo wake kupindana kwa miaka yote 18. Tunamuona Yesu akimfungua huyu mama kwa kuwa aliujua huo ni mpango uliokuwa wa kishetani. Hata katika maisha yako, pengine yapo mambo yamepindisha maisha yako kwa muda mrefu. Unapaswa kuyaona mambo haya katika ulimwengu wa roho, kwa kuwa wapo watu waovu wanaopindisha maisha ya watu wengine. 

UKIRI
Ewe tukio la kichawi lililoandaliwa kuniangamiza mimi nakufyeka kwa Jina la Yesu.  Tukio la kukataliwa, Ng’ooka kwa Jina la Yesu, achia maisha yangu, achia biashara zangu, achia ndoa yangu kwa Jina la Yesu. Amen

 
Endapo katikati yetu yupo mtu hajampa Yesu Kristo maisha yake, kwa maana ya kuokoka, Leo Amua kufanya hivyo ili iwe rahisi kwako kuyaharibu matukio ya kutengenezwa ya kishetani katika Jina la Yesu.


========== AMEN ========

KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:

FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/
Share:
Powered by Blogger.

Pages