Sunday, May 7, 2017

MILANGO YA KUZIMU HAITANISHINDA


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)

{KANISA LA UFUFUO NA UZIMA → MOROGORO}


JUMAPILI: 07 MAY 2017


MHUBIRI:  PASTOR KELVIN MWAIPOPO (SNP NZEGA, TABORA)


Mchungaji Kelvin Mwaipopo akifundisha neno la Mungu, Morogoro.  leo 7. May.2017.

Je hii milango ya kuzimu ni ipi? Kwa kawaida, inapokuwepo nyumba, lazima pawepo pia mlango wa kuingiza vitu ndani na kutoa vitu nje. Hata hivyo, ipo milango ya rohoni pia, ambayo hufanya kazi hiyo hiyo. Kwa maana hiyo yapo malango ya mwilini na malango ya rohoni,  na kwa kuwa Kuzimu ni Roho,  nayo pia ina malango  yake.


1.      MILANGO YA  KIMWILI KATIKA BIBLIA

Katika MWANZO 19:1-2 (Basi, wale malaika wawili wakaja Sodoma jioni; na Lutu alikuwa amekaa mlangoni pa Sodoma. Lutu akawaona akaondoka akaenda kuwalaki, akainama kifudifudi. 2 Akasema, Bwana zangu, karibuni nawasihi mwingie nyumbani mwa mtumwa wenu, mkalale, mkanawe miguu yenu, hata asubuhi mwondoke na mapema mkaende zenu. Wakasema, Sivyo, lakini tutakaa uwanjani usiku kucha.). Hawa ni malaika lakini ili waweze kufanya kazi iliwapasa wavae miili ya kibinadamu na Lutu akaweza kuwaona kimwili. Malaika hawa wanatumia mlango wa kimwili wa mji wa Sodoma. Mlango mwingine ni ule aliotumia Ibrahmu, kama ilivyoandikwa katika MWANZO 18:1 (Bwana akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari.)



baadhi ya makutano wakimsikiliza mchungaji na kuandika neno la Mungu. leo 7. May.2017


Katika KUTOKA 12:22-23 imeandikwa (Nanyi twaeni tawi la hisopu, mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini na kukipiga kizingiti cha juu, na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli; tena mtu ye yote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba yake hata asubuhi. 23 Kwa kuwa Bwana atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, Bwana atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi.). Kuanzia kipindi hiki cha Musa, Yesu alikuwa akitabiriwa hapa kwa kuwa alama ya msalaba iliwekwa kwenye milango hii kwa kutumia damu ili Bwana  atakapopitakuwapiga Wamisri, wana wa Israeli wao wasidhuriwe.


KUTOKA 33:8-10 (Hata Musa alipotoka kuiendea ile hema, watu wote waliondoka wakasimama, kila mtu mlangoni pa hema yake, akamtazama Musa, hata alipokwisha kuingia hemani. 9 Ikawa Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye Bwana akasema na Musa. 10 Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake.). je uliwahi kujiuliza swali kwa nini washirikina huweka mitego yao katika milango? Hii  ni kwa sababu katika mlango ndipo mtu huingia na kutoka. Katika baraka, Mungu ameahidi atakubariki uingiapo na uondokapo. Kwa hiyo ndiyo maana wachawi hutegesha mitego yao milangoni, ili mtu alaaniwe aondokapo na alaaniwe aingiapo. Mchana wa leo Bwana amesimama mlangoni ili kukubariki katika Jina la Yesu.


Katika YOSHUA 6:1-3 imeandikwa (Basi Yeriko ulikuwa umefungwa kabisa kwa sababu ya wana wa Israeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia. 2 Bwana akamwambia Yoshua, Tazama, nimeutia Yeriko katika mkono wako, na mfalme wake, na mashujaa wake. 3 Nanyi mtauzunguka mji huu, watu wote wa vita, mkiuzunguka mji mara moja.Fanya hivi siku sita.). Sisi hatupaswi kuogopa kitu tena. Tayari tumeshaivuka Bahari ya Shamu kwa ushindi, na sasa ni muda wetu kuingia Yeriko  na kuimiliki sawasawa na ahadi za Bwana wetu.

Baadhi ya makutano wakifuatilia kwa umakini mafundisho ya neno la Mungu. leo 7. .May.2017.



Imeandikwa katika WAAMUZI 16:3 (Basi Samsoni akalala hata usiku wa manane, akaondoka katikati ya usiku, akaishika milango ya lango la mji, na miimo yake miwili, akaing'oa pamoja na komeo lake, akajitwika mabegani, akavichukua hata kilele cha mlima ule unaokabili Hebroni). Ndivyo itakavyokuwa kwako siku ya leo. Endapo wachawi watakuzuia, leo uamke usiku na kuyang’oa mageti yao yote ya kuzimu waliyokuwekea katika Jina la Yesu. Mageti ya utasa, mageti ya umaskini, mageti ya magonjwa n.k. yapo katika uwezo wako, kama alivyofanya Samsoni, nawe leo uamue kuyang’oa yote kwa Jina la Yesu.

Lakini wewe unapaswa kujua kuwa MWANADAMU NI LANGO. Katika ZABURI 24:1-10 imeandikwa hivi (Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake. 2 Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari, Na juu ya mito ya maji aliithibitisha. 3 Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake? 4 Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili, Wala hakuapa kwa hila.5 Atapokea baraka kwa Bwana, Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.6 Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao, Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. 7 Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Inukeni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia. 8 Ni nani Mfalme wa utukufu? Bwana mwenye nguvu, hodari, Bwana hodari wa vita. 9 Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Naam, viinueni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia. 10 Ni nani huyu Mfalme wa utukufu? Bwana wa majeshi, Yeye ndiye Mfalme wa utukufu.).  Katika Agano la Kale kabla ya Yesu jkjuzaliwa, mwanadamu alikuwa ni lango ambalo  Mungu laiweza kuingia nakutoka.Mungu aliweza kuingia ndani na kuleta afya, utajiri, mapato, n.k. Kwa upande mwingine wachawi nao kwa kulitambua hili waliweza pia kuingiza magonjwa, umaskini, utasa n.k. kwa mwanadamu.


Katika ISAYA 60:11 Imeandikwa (Malango yako nayo yatakuwa wazi daima; Hayatafungwa mchana wala usiku; Ili watu wapate kukuletea utajiri wa mataifa, Na wafalme wao wakiongozwa pamoja nao.). Malango yako yakiwa wazi Bwana ataingia na kuupitisha utajiri wa mataifa. Je, wewe uliyeokoka, unamiliki biashara gani? Hivi uliwahi kujiuliza swali kwa nini biashara zote kubwa kubwa kama za vituo vya mafuta ya petroli hazimilikiwi na walokole? Ni wakati umefika ili utajiri wa mataifa uje kwetu kwa Jina laYesu pale tutakapoachia milango yetu wazi ili Bwana aingie ndani mwetu.


Imeandikwa katika YOHANA 10:7-9 (Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. 8 Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. 9 Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.). Yesu ametuahidi kwamba atakaeingia katika Mlango ambao ni  Yesu Kristo, atapata MALISHO. Ni mamombi yetu leo kwamba umruhusu Yesu akupe malisho ya ndoa, malisho  ya afya, malisho ya kazi, biashara, elimu n.k. kwa Jina la Yesu.


2.      MILANGO YA ROHONI IKOJE?

Mifano hii ya Kibiblia hapo juu yote inazungumzia malango ya kimwili. Sasa ni wakati pia wa kuyatazama malango ya Rohoni.

Tunasoma katika ZABURI 78:23 tunakutana na neno la Mungu likisema (Lakini aliyaamuru mawingu juu; Akaifungua milango ya mbinguni). Kumbe basi mbinguni nako yapo malango. Kwa hiyo ni sharti ujiunganishe na haya malango ya mbinguni ili upate afya, upate kazi, upate ndoa nzuri n.k. Imeandikwa katika UFUNUO 1:1-2 (Baada ya hayo naliona, na tazama, mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo. 2 Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti;).


Imeandikwa katika 1WAKORINTHO 16:9 (kwa maana nimefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao). Paulo anazungumzia mlango tena mkubwa, siyo wa kimwili, bali wa kiroho ulikuwa mbele yake. Hata hivyo wapo waliompinga ili asiupite.   Katika UFUNUO 3:8 imeandikwa (Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.). Hata sasa, yamkini upo mlango mkubwa sana mbele yako lakini wanaokupinga ni wengi na ambao ni watu kabisa: Pengine ni mashangazi zako, mababu, mabibi, majirani n.k. ndiyo wamkea kukuzuia. Leo tutaomba na kuwafyeka wote wanaotupinga, kwaJina la Yesu.


Tunapoonglea kuzimu, inafaa tufahamu kuwa KUZIMU NI ROHO. Na hivyo  kuzimu ina tumbo, na pia ina kinywa. Ndiyo maana Yona alisema alikuwa katika tumbo la kuzimu  katika zile siku tatu alizomezwa na samaki. Tumbo  la Kuzimu linameza vitu na kuvihifadhi, na ndiyo maana inabidi  tuamuru kuzimu kuvitapika vitu vyetu  vyote ilivyomeza kwa Jina la Yesu. Imeandikwa ISAYA 5:13-14 (Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana. 14 Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo.).


Asili ya kutawala ni yetu sisi wanadamu wala siyo ya shetani. Yesu  aliturudishia tena asili hii  ya utawala iliyokuwa imeibiwa na shetani, na kwa kuanzia ndiyo maana siku  moja Yesu katika kuivuka Bahari, alitembea juu ya maji kinyume na kanuni za kibinadamu. Yesu anatufundisha kuwa tunayo MAMLAKA JUU YA BAHARI na vilivyomo ndani yake. Yesu huyo huyo siku ile alipokufa msalabani alienda kuzimu na kumnyang’anya shetani funguo za kuzimu na mauti. Siku ya tatu Yesu alipofufuka, alidhihirisha kwamba tumbo la kuzimu haliwezi kumzuia, na ndiyo maana akafufuka na kuishinda mauti. Kaburi lilishindwa kumzuia Yesu asifufuke, ili kutufundisha sisi kuwa ardhi tuliyo nayo imeshakombolewa na Bwana Yesu, na tunapaswa KUIMILIKI ARDHI vile vile. Siku 40 baada ya Yesu kufufukailipofika, Yesu alipaa mbinguni na wingu la angani likampokea kudhihirisha kuwa tunayo mamlaka pia ya KULITAWALA ANGA lote, na kwamba hakuna cha kutuzuia.


Imeandikwa katika ZABURI 49:15 (Bali Mungu atanikomboa nafsi yangu, Atanitoa mkononi mwa kuzimu, maana atanikaribisha.). Kumbe tunajifunza kuwa kuzimu  inayo mikono. Kama ndivyo, ujue wazi kuwa mikono ya kuzimu inaweza kuzuia mambo yako yasifanikiwe. Saa imetimia kuizuia mikono ya kuzimu inayotuzuia ili mikono hiyo isifanikiwe kwetu kwa Jina la Yesu.


Katika YONA 2:2 Imeandikwa (Akasema, Nalimlilia Bwana kwa sababu ya shida yangu, Naye akaniitikia; Katika tumbo la kuzimu naliomba, Nawe ukasikia sauti yangu.). Tunaona kuwa kumbe kuzimu inalo tumbo. Na kama hali  ndiyo hiyo tujue kuwa tumbo hili linalishwa vitu mablimbali siku  hadi  siku.


Imeandikwa katika UFUNUO 6:8 (Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi.). Kumbe  tunaona kuwa KUZIMU kwa  kuwa ni roho inaweza kupanda farasi (au  bodaboda, au basi, au gari,  au meli n.k) na ikaongozana na Roho  ya MAUTI,  na  wawili hawa wakaleta uharibifu kwa mwanadamu. 


Pia imeandikwa katika MATHAYO 16:13-17 (Basi Yesu akaenda pande za KaisariaFilipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? 14 Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.15 Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? 16 Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. 17 Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Baryona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. 18 Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.). Sisi kama kanisa tumejengwa katika mwamba ambao ni Yesu Kristo, na malango ya kuzimu haitalishinda kwa Jina la Yesu.






Doughters of Abraham wakicheza kwa pamoja na SNP Dr. Godson Issa Zakaria. leo 7.May.2017.



Katika UFUNUO 1:17-18 imeandikwa (Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, 18 na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.). Leo tuyafungue malango yote ya kuzimu yaliyoficha mali na vitu vyetu vyote kwa Jina la Yesu. Leo tuite viungo vya miili yetu vilivyoibiwa na kuwekwa kuzimu (tuite uso, tuite mikono, miguu, sura iliyoibiwaa n.k), kwa sababu tayari tunazo funguo za mauti na kuzimu mikononi mwetu katika Jina la Yesu.


UKIRI
Baba Mungu katika Jina la Yesu, nakataa, hakuna mchawi, wala mganga wa kienyeji atakayeufunga mlango wangu wa mafanikio. Kuanzia sasa, milango yangu yote naifunua kwa JJina la Yesu. Tumbo la Kuzimu likijaribu tena lipasuke kwa Jina la Yesu. Kuanzia sasa, ninamiliki anga, ninamiliki ardhi na ninamiliki bahari kwa Jina la Yesu. Amen


Hata hivyo hauwezi kumpinga shetani wakati yeye bado ni baba yako. Ni lazima kuhama kwanza kutoka katika ulimwengu wa mashetani na kumjia YESU ili kuwa rahisi kumshinda huyu muovu shetani. Endapo katikati yetu leo yupo mtu ambaye hajaokoka, ni fursa pekee kwako kumpa Yesu maisha yako. 


========== AMEN ========



KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:

FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia

Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson

Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson

TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)

BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/
Share:
Powered by Blogger.

Pages