Tuesday, May 16, 2017

USHUHUDA WA RHODA WILLIAM - KINOLE


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)

KANISA LA UFUFUO NA UZIMA

{MOROGORO}

JUMAPILI: 14 MAY 2017

 

 
Mwanzoni alikuwa anafahamu kusoma vitabu vya elimu ya awali, lakini kufikia darasa la 3 akaugua ugonjwa wa Homa ya Degedege, akazimia kwa wiki 2.  Alizinduka wiki ya 3 muda wa saa 12:00 jioni, na pembeni yake alikuwepo mchungaji  mmoja aliyekuwa akimuombea (ingawa haijulikani ni nani au alikotokea kanisa gani). Kuanzia pale akasahau kabisa kusoma na akili zake zikagoma kuelewa anachofundishwa. Hali iliendelea vile, na alipofika darasa la 5 akaacha shule mwenyewe.


Rhoda akifafanua jambo wakati akihojiwa na SNP Dr. Godson (Kulia) na RP Steven (Kushoto), Jumapili 14/5/2017

 

Huyu tunayemzungumzia ni Rhoda William (Anayehojiwa Pichani), binti  mwenye umri wa miaka 21, anayeishi Kihonda Morogoro. Ni binti aliyechukuliwa msukuleni na bibi mzaa baba (Jina linahifadhiwa) anayeishi kijiji cha Kinole -  Morogoro. Kazi kubwa akiwa msukuleni ilikuwa kumsaidia bibi yake kuua watu kwa kusababisha ajali za barabarani. Anakiri kuua watu wapatao 200 hivi kwa ajali mbalimbali za mabasi ya abiria maeneo ya Morogoro, Mwanza na Marekani. Je, aliwahi kufika Marekani? Rhoda anasema wanaposafiri na bibi yake, ndiye humtajia mahali walipo, ikiwemo huko Marekani!!!

 

Kwa ujumla haya ni maisha ya hofu na mateso  aliyoishi Rhoda tokea achukuliwe msukule. Chakula chake kikuu akiwa huko msukuleni kilikuwa kutafuna matofali ya ujenzi. Na pale anaposababisha ajali, Rhoda alikuwa akipewa zawadi ya lita moja ya damu ya waliouawa ili anywe, na endapo akikataa kunywa bibi alikuwa akimchapa kwa fimbo fulani nyeusi. Kutokana na hali  hiyo, hamu  yake ya kunywa damu za watu  iliongezeka siku  hadi  siku.

 

Alikuwa akiwaua je watu kwa ajali? Rhoda anasema Bibi yake humjia usiku, na kumpaka dawa ya unga mweupe puani, kisha bibi hutoweka, na muda mfupi baadae bibi atarejea upya akiwa na dawa nyingine ya unga tofauti atakayompa mjukuu wake huyu  ili  awarushie usoni madereva wa mabasi yenye abiria wengi.!!!  Dereva atakayelengwa, huona ukungu umetanda kwa mbele barabarani, na ataliyumbisha basi lake, mwishowe litakosa mwelekeo na ajali mbaya itatokea. Hapo penye tukio la ajali, bibi hutokezea mara moja na vibuyu vyake kajifunga kiunoni tayari kujaza damu za watu (ingawa siyo rahisi watu kumuona kwa macho haya  ya  nyama). Rhoda anasema, bibi anacho chombo mithili ya vuvuzela, ambacho huinyonya damu kutoka kwa maiti mmoja hadi mwingine na kujazilia vibuyu vyake hadi vijae. Je, bibi huipeleka wapi damu hiyo? Rhoda anasema hajui kinachoendelea kwa sababu mara zote alikuwa  akizuiwa na bibi yake kuingia huko anakoipeleka hiyo damu. Je, aliwahi kuua watu wa familia au ndugu zake? Rhoda anajibu hapana, hakuwahi kufanya  hivyo.

 

Aliweza je kutoka Kinole hadi mabarabarani ili kusababisha ajali? Rhoda anasema akiwa amelala, Bibi yake humjia na kumpulizia dawa fulani na atajiona kama wapo Rhoda-wawili wanaofanana wakiwa hapo kitandani. Huyo Rhoda mmoja ataondoka mithili ya kivuli na kwenda barabarani kutekeleza mpango  wa kusababisha ajali kama bibi yake atavyomwagiza kufanya. Rhoda mwingine hubaki kitandani akiwa katika usingizi mzito sana.

 

Siku moja bibi yake alimpeleka Rhoda mahali asipopajua na kumtambulisha kikaoni kwa watu fulani ambao pia hakuwafahamu. Rhoda akasimikwa kuwa MALKIA kuanzia pale, na kulazimishwa kuolewa na mwanaume mmoja mwenye ngozi nyeupe (mzungu). Huyu ndiye kila mara alimjia ndotoni na kushiriki naye unyumba nyakati za usiku. Mwanaume huyu alikuwa akipokea maalekezo kutoka kwa bibi wa Rhoda, na kuyaleta kwa malkia Rhoda kwa utekelezaji. Je, alipata watoto na huyu mwanaume?  Kwa hilo Rhoda hakumbuki chochote.

 

Rhoda aliwezaje kutoka huko msukuleni? Rhoda anasema wiki jana aliletwa Kanisani Ufufuo na Uzima Morogoro kuombewa. Wakati anaombewa ilisikika sauti kubwa ya “NJOO KWA JINA LA YESU” iliyomfanya bibi yake amfukuze na kumwambia hiyo sauti ya NJOO inamkera na kumuachia  aondoke  zake. Hata hivyo bibi yake alimkataza asitoe siri ya mambo yake huko aendako.

Rhoda  akihitimisha Ushuhuda wake, Kanisani Ufufuo na Uzima Morogoro hapo Jumapili 14/5/2017


Kwa sasa Rhoda ameokoka, ameamua kuachana na mambo ya uchawi na anamtumikia Bwana Yesu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima Morogoro. Sifa na Utukufu ni kwa Yesu Kristo pekee.
 
 

 

========== AMEN ========
 
KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/
 

 
Share:
Powered by Blogger.

Pages