Sunday, June 11, 2017

KWA AJILI YA SAYUNI SITANYAMAZA

GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)
{KANISA LA UFUFUO NA UZIMA → MOROGORO}

JUMAPILI: 11 JUNE 2017

             MHUBIRI:  PASTOR STEVEN NAMPUNJU (Rp)


Tunaposoma katika ISAYA 62:1 neno la Mungu linasema “Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo.”. Mji wa Sayuni  ulikuwa umetekwa na maadui na wakaweka vituo vyao hapo.  Adui hawa walijitapa sana, na kuwekeza nguvu  zote hapo ili  kuzuia mtu  yeyote asiweze kuuteka  tena Sayuni  au Yerusalemu. Sayuni ndiyo ulikuwa ngome ya Wayebusi. Mji huu wa Sayuni ulipewa jina hilo kumaanisha ni “ngome iliyoimarika”. Hata wewe leo hii hupaswi kuangalia sana uimara wa dhiki (ngome) uliyo nayo, bali mtazame Yesu Kristo aliye ngome imara, na ngome uliyo nayo na inayokusumbua itaanguka mara moja kwa Jina la Yesu.

Katika ISAYA 65:6-7 imeandikwa (Tazama, neno hili limeandikwa mbele zangu. Sitanyamaza, lakini nitalipa, naam, mimi nitawalipa ujira wao vifuani mwao; 7 maovu yenu na maovu ya baba zenu pamoja, asema Bwana, ninyi mliofukiza uvumba juu ya milima, na kunitukana juu ya vilima; basi, kwa ajili ya hayo nitawapimia kwanza kazi yao vifuani mwao.).  Mungu wetu  hulipa, na siyo  Mungu  anayekopa. Endapo kuna mtu amepanda mabaya, au mauti, au magonjwa juu yako, leo ujue kuwa Bwana atakulipia yote kwa Jina la Yesu. Kuna watu wanayo madeni ya afya, Mungu yupo tayari  kukulipia madeni yako. Kuna watu  wenye  madeni ya ndoa, na leo  Mungu  wetu kwa kuwa huwa analipa ujira pia atakulipia madeni yako hazo kwa Jina la Yesu.

Mungu aliichagua Yerusalemu kama mji wake. Kama unavyoiona Yerusalemu leo hii ikikaliwa na watu ambao ni wenyeji (Wayahudi), ndivyo ambavyo Yerusalemu ya rohoni (yaani wewe na mimi) tunavyopaswa kuishi, kwa kumruhusu Yesu aingie ndani yetu. Ndiyo maana Yesu alisema kwamba yupo mlangoni anagonga, na yeyote atakayefungua mlango, Yesu na Mungu  Baba wataingia ndani mwakena kukaa naye.


Katika YOSHUA 6:1 imeandikwa Basi Yeriko ulikuwa umefungwa kabisa kwa sababu ya wana wa Israeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia.” Kumbe tunajifunza kuwa mji unaweza kufungwa kwa sababu tu ya watu fulani wasiuingie. Yoshua alichagua makuhani na baadhi ya watu kadhaa ambao waliuzunguka mji wa Yeriko kwa siku zote 7 ingawa  kimsingi walihatarisha maisha yao. Unapopigana vita vya rohoni ndiyo njia pekee ya kuwashinda adui zako, ingawa kimsingi unakuwa unahatarisha hata maisiha yako.

Hata hivyo, ngome ya Sayuni ilipigwa na Daudi na baadae ilibadilishwa jina na kuitwa Mji wa Daudi. Tunajuaje haya? Imeandikwa katika 2SAMWELI 5:1-10 (Ndipo kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako. 2 Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli watoke nje, na kuingia ndani. Naye Bwana akakuambia, Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli. 3 Basi wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni, naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za Bwana; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli. 4 Daudi alikuwa amepata miaka thelathini alipoanza kutawala, akatawala miaka arobaini. 5 Huko Hebroni alitawala miaka saba na miezi sita; na katika Yerusalemu alitawala miaka thelathini na tatu juu ya Israeli wote na Yuda. 6 Kisha mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu ili kupigana na Wayebusi, wenyeji wa nchi ile; hao ndio waliomwambia Daudi, wakisema, Usipowaondoa vipofu, na viwete, hutaingia humu kamwe; huku wakidhania ya kuwa Daudi hawezi kuingia humo. 7 Lakini Daudi aliipiga ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi. 8 Naye Daudi alisema siku hiyo, Yeye atakayewapiga Wayebusi, na apande kwenye mfereji wa maji, na kuwapiga viwete, na hao vipofu, ambao roho yake Daudi inawachukia. Kwa sababu hii watu husema, Wako vipofu na viwete hawawezi kuingia nyumbani. 9 Basi Daudi akakaa ndani ya ngome hiyo, akaiita mji wa Daudi. Kisha Daudi akajenga toka Milo na pande za ndani. 10 Naye Daudi akazidi kuwa mkuu; kwa maana Bwana, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye).

Yamkini wapo Wayebusi wa Kiroho wanaokupa wewe masharti kuwa usipofannya mambo kadhaa kadhaa hautafanikiwa.  Unapaswa kuwa kama Daudi katika ulimwengu  wa roho ili kupambana  na wanaokuzia kwa Jina la Yesu. Wanaokuzuia ili usisome, leo kataa maneno yao na hatimaye ubadili jina lako na kuitwa msomi tena kwa Jina la Yesu. Mji uleule ambao Daudi alizuiwa, ndiyo  ambao  baadae ulikuja kuitwa Mji  wa Daudi.

UKIRI
Nazilazimisha ngome zozote zilizokaa kunizuia nisisome, nami naziangusha kwa Jina la Yesu.


Imeandikwa katika 1NYAKATI 11:1-7 … (Ndipo Israeli wote wakamkusanyikia Daudi huko Hebroni, wakisema, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako. 2 Katika zamani za kale, hata hapo Sauli alipokuwa mfalme, wewe ndiwe uliyewatoa na kuwaingiza Israeli. Naye Bwana, Mungu wako, akakuambia, Ndiwe, utakayewalisha watu wangu Israeli, ndiwe utakayekuwa mkuu juu ya watu wangu Israeli. 3 Basi wazee wote wa Israeli wakamjia mfalme huko Hebroni; naye Daudi akafanya agano nao huko Hebroni mbele za Bwana; nao wakamtia Daudi mafuta, awe mfalme wa Israeli, sawasawa na neno la Bwana kwa mkono wa Samweli. 4 Kisha Daudi na Israeli wote wakaenda Yerusalemu, (ndio Yebusi;) nao Wayebusi, wenyeji wa nchi, walikuwamo. 5 Na hao wenyeji wa Yebusi wakamwambia Daudi, Hutaingia humu. Walakini Daudi akaitwaa ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi. 6 Naye Daudi akasema, Mtu ye yote atakayekuwa wa kwanza wa kuwapiga Wayebusi, yeye atakuwa mkuu na jemadari. Naye wa kwanza aliyepanda ni Yoabu mwana wa Seruya, naye akawa mkuu. 7 Basi Daudi akakaa ngomeni; kwa hiyo huuita mji wa Daudi.). 

Unaweza kuwa wewe ni mfanyabiashara katika mji fulani, lakini kuna watu ambao ni wenyeji wa mji huo wanaoamua nani akae au asikae katika huo mji.  Unaweza kujisifia sana kuhusu mwili wako, lakini ujue kuwa yapo majini pia ambayo yanayoweza kuusumbua huo mwili kwa kuutumikisha na kuufanya  kuwa mali yao. Ndiyo maana wapo watu kwa vinywa vyao husema kuwa miili yao ina mashetani, na ambayo yakichachamaa yanakuwa makali kweli kweli.!! Ni kweli wewe unaweza kuwa mwili ulio nao ni wako lakini ufahamu kuwa wapo pia wenyeji wa huo mwili wanaweza kuwemo ndani. Ndiyo maana wapo watu wakitaka kwenda kanisani, kuna sauti huwaambia ndani mwao kuwa hakuna haja ya kwenda.

Tunasoma katika  1WAFALME 8:1  “Ndipo Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila, wakuu wa mbari za mababa wa wana wa Israeli, wamwendee mfalme Sulemani huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la agano la Bwana kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni”. Daudi ndiye aliubadili Jina la Mji wa Sayuni uliokuwa unakaliwa na Wayebusi na kuuita Mji wa Daudi. Ndivyo ilivyoandikwa pia katika 2NYAKATI 5:2Ndipo Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila, wakuu wa mbari za mababa wa wana wa Israeli, huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la agano la Bwana kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni.”.

Katika YOSHUA 15:63 imeandikwa “Tena katika habari ya Wayebusi, hao wenye kukaa Yerusalemu, wana wa Yuda hawakuweza kuwatoa; lakini hao Wayebusi walikaa pamoja na wana wa Yuda huko Yerusalemu hata hivi leo.” Je, na wewe umechanganyika na wenyeji wa kiroho? Yamkini wewe ni mwanamke au mwanaume lakini ndani mwako wapo wanawake/wanaume wa rohoni waliochanganyika na wewe!! Kila Myebusi wa kiroho anayekaa na kukutumikisha maisha yako leo umkatae kwa Jina la Yesu. Yamkini wewe uliwahi kuja kanisani lakini baadae ukawaendea waganga wa kienyeji nao wakakuchanja chale, kwa hali hiyo ujue kuwa umeruhusu Wayebusi wa rohoni kukaa katikati ya maisha yako. Ukimtii Yesu anakuja mwenyewe, lakini shetani ukimpinga katika maisha yako atakimbia mwenyewe. Katika kila mji wenyeji wa mji wapo. Yamkini hawa wenyeji ni wale wanaokupangia cha kufanya katika huo mji. Kipindi cha Yoshua, wana wa Yuda waliwaacha Wayebusi na kukaa pamoja nao baada ya kushindwa kuwaondoa hawa wenyeji. Kitendo hiki cha kuchanganyika na kukaa pamoja na Wayebusi kilimfanya Daudi aanzishe vita hasa baada ya kupewa sharti la kukaa ndani ya huo mji kwa kuambiwa eti awaondoe viwete na vipofu ndani ya mji. Daudi alikataa miiko aliyopewa na Wayebusi, na ndiyo maana akapigana na kuutwaa huo mji na hatimaye kuuita Mji wa Daudi.

UKIRI
Kuanzia leo naulazimisha ufalme wowote wa kishetani uliofunga maisha yangu achia, kwa Jina la Yesu.



Neno  la Mungu katika ISAYA 43:1-9 linasema (Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. 2 Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza. 3 Maana mimi ni Bwana, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako. 4 Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako. 5 Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi; 6 nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia. 7 Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya. 8 Walete vipofu walio na macho, na viziwi walio na masikio. 9 Na wakusanyike mataifa yote, kabila zote wakutanike; ni nani miongoni mwao awezaye kuhubiri neno hili, na kutuonyesha mambo ya zamani? Na walete mashahidi wao, wapate kuhesabiwa kuwa na haki; au na wasikie, wakaseme, Ni kweli.). 

Mungu anapokukomboa anaandaa pia watu wa kukusaidia. Shetani amefunga maisha yako, lakini Mungu amesema hatanyamaza kwa ajili yako. Mungu ndiye aliyekuumba, na ndiye mwenye nyumba, yaani mwili wako. Yesu aliyekuumba anataka awafukuze wapangaji wasiofaa, yaani majinni na mapepo yote ndani ya  huo mwili. Wewe unayetaka kuomba lakini wakati wa maombi ukifika macho yanakuwa mazito ujue tayari kuna mwenyeji wa huo mwili anayezuia usiombe, yaani ni Myebusi wa rohoni. Kuna watu wengine ukiwashauri waokoke hutoa visingizio mbalimbali, au pengine kwa kuomba waruhusiwe wakatoe taarifa kwanza kwa wenzi wao au wazazi wao. Cha kufahamu hapo ni kuwa, ndani ya miili ya watu kama hao kuna wenyeji ambao ni Wayebusi wa rohoni wanaowazuia wasifanye maamuzi ya kuokoka. Ni vyema leo kukataa kutumikishwa na wenyeji wa mwili wako,  kwa sababu itakapofika siku ya mwisho wa maisha yako, hao ndugu uliotaka kuwaomba ruhusa hawatakuwa na wewe katika hukumu ya mwisho.

UKIRI
Enye Wayebusi wa kiroho, leo nawalazimisha achia maisha yangu kwa Jina la Yesu. Amen


Yamkini kuna vitu vingi ulivifanya maishani mwako, vikasababisha ngome ya tatizo lako kuwa imara na kudumu sana. Wapo watu walioenda kwa waganga wa kienyeji, na kupitia yale makombe waliyonyweshwa, tatizo walilo nalo limeimarika kama ngome za Sayuni.  Leo mtazame Yesu na ataiondoa  shida uliyo nayo mara moja katika Jina la Yesu Kristo. Ugonjwa ulio nao usikunyamazishe, taabu uliyo nayo isikunyamazishe, kwa kuwa imeandikwa “kwa ajili ya Sayuni Sitanyamaza”. Mwendee Yesu na kwa sauti yako upaze sauti usikubali kunyamaza.

UKIRI
Waliotumwa kuninyamazisha nawateka nyara. Leo nawateka nyara wachawi wote waliologa maisha yangu. Nawalazimisha wale wote waliojenga ngome kwenye hatima yangu na kwenye mwili wangu, ngome ya utasa, ngome ya magonjwa, nawashambulia kwa Damu ya Yesu. Enyi mnaojiita wenyeji kwenye mwili wangu nawalazimisha wenyeji mapepo, majini, mizimu muachie maisha yangu kwa Jina la Yesu. Amen

Yesu anataka kuwasaidia watu ambao hajaokoka ili ngome za Wayebusi zilizojengwa maishani mwako zikabomolewe zote kwa Jina la Yesu.

========== AMEN ========

KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)

BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/
Share:
Powered by Blogger.

Pages