Sunday, June 25, 2017

VITA DHIDI YA DHAMBI YA UZINZI

GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH (GCTC)
{KANISA LA UFUFUO NA UZIMA → MOROGORO}

JUMAPILI: 18 JUNE 2017

MHUBIRI:  PASTOR DR.GODSON ISSA ZACHARIAH (Snp)

Mch.Dr.Godson Issa Zacharia akifundisha kuhusu "vita dhidi ya dhambi ya uzinzi".

Katika Kitabu cha WAEFESO 5:3 imeandikwa “Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;”. Mtume Paulo anatuasa kuwa kwa watakatifu neno la uasherati au uchafu lisitajwe kamwe.  Neno uasherati au uzinzi kwa mara nyingi hutumika kumaanisha jambo moja. Uasherati ni pale  tendo la ndoa likifanywa na mtu kabla hajaoa au kuolewa. Uzinzi kwa upande mwingine, ni tendo la ndoa likifanywa na mmojawapo wa wanandoa pamoja na mwanaume/au mwanamke asiyehusika katika hiyo ndoa. Hata hivyo Biblia inasema kila dhambi ina mshahara wake ambao ni mauti.


1.      BIBLIA INASEMA JE KUHUSU UZINZI / UASHERATI?
Biblia inautaja Uzinzi/au uasherati kama dhambi ya tofauti kwa sababu ndiyo pekee ambayo “hufanyika ndani ya mwili”. Imeandikwa katika 1WAKORINTHO 6:18-19Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. 19 Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;” Dhambi ya uzinzi siyo dhambi ya kukemea. Unapaswa kuikimbia. Zinaa ni sawa na ibada ya sananu, hupaswi kuikemea bali kuikimbia. Kwa hiyo, fahamu kuwa tendo la ndoa lisilo sawasawa siyo dhambi ya wewe kukaa na kukemea bali unapswa kuikimbia.

Yusufu akiwa katika nyumba ya Potifa, alikumbana na kishawishi cha kufanya tendo la ndoa na mke wa Potifa. Kilichomsaidia Yusufu hata baada ya kushawishiwa kuingia chumbani kwa mama huyu, ni kuwa na Roho Mtakatifu,  na ndipo alijua ni  kosa kufanya jambo kama lile ambalo ni kinyume na neno la Mungu. Huyu mama Potifa alitaka kumbaka Yusufu, kwa maneno na matendo ya ushawishi alioundaa. Hata hivyo Yusufu alikimbia na kuacha vazi lake kwa yule mama Potifa. Ni bora kufungwa gerezani kwa kosa la kukimbia uzinzi kuliko kukubali kutenda dhambi ambayo mwishowe utaishia kupata wadudu (magonjwa).


Watendakazi wakisikiliza kwa makini somo la leo.

Unapswa kuikimbia zinaa. Hapana maombi ya kushindana na uzinzi. Hata kama utafunga kutokula na kunywa, hilo siyo suluhisho, na kabla hujamaliza mfungo huo utakuwa umeshazini. Hayo majina ya kuitwa honey (asali), sweetheart n.k. ni mwanzo tu wa kuingia katika mtego wa uzinzi. Dhambi zingine zote hufanyika nje ya mwili, bali uzinzi ndiyo pekee hufanyika ndani ya mwili. Mwisho wa uzinzi ni uharibifu ndani ya mwili wake mwenyewe…. Cha kufanya “IKIMBIENI ZINAA”.

Mkristo yeyote hapaswi kuikaribia zinaa. Katika maisha yako mambo ya uasherati  na uzinzi vyapaswa kuwa mbali na maisha yako. Ni bahati mbaya kuwa leo hii  usaherati na uzinzi vinatajwa ndani ya kanisa!!! Mungu anasema “uasherati usitajwe kwenu kamwe”. Wapo Wakristo ambao wana nyumba ndogo katika mitaaa mbalimbali wanakoishi. Wengine wanakuja makanisani lakini wameamkia katika nyumba za uzinzi. Yupo mtu umekuja kanisani leo  lakini kumbe hata aliyekupa nauli ya kuja kanisani siyo mumeo bali ni mume wa mtu mwingine. Kinachotokea katika nyumba za kilokole leo hii ni tofauti na matarajio ya  wengi. Wapo watu wanapewa talaka katika makanisa ya waliokoka, tofauti na matarajio ya wengi. Wakristo ni viungo katika mwili wa Kristo.  Ndoa ya  Kiksristo ni ya mume mmoja na mke mmoja,  na hakuna kutalikiana.

Wakristo wengi wa leo hawaeleweki. Nyumba ndogo zipo hadi makanisani. Ndiyo maana Paulo alisema mambo kama hayo yasitajwe kamwe. Imeandikwa katika WAGALATIA 5:19-21Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, 20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.”. Mungu amesema usimwache mwanamke mchawi kuishi. Na kwa kuwa basi, uchawi, uasherati, uzinzi na ibada ya sanamu ni kitu kile kile, basi ni sawa tu  na kusema kuwa “Usimwache  mwanamke / mwanaume mzinzi  kuishi.” Kwa mtu yeyote afanyaye matendo kama hayo, huyaalika mashetani kuukalia mwili wake. Ndivyo ilivyoandikwa katika UFUNUO 18:2-3 (Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza; 3 kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake.). Kumbe kitendo cha mwanaume kulala na mwanamke asiye mke wake au kijana kulala na binti kabla ya muda wa ndoa, maana yake ni kukaribisha mashetani ndani ya mwili wake mwenyewe. Leo lazima tuwaapige waasherati, wazinzi na wachawi wote kwa kuwa jambo lao na mwisho wao ni mmoja!!


Platform ministry wakiongoza kusifu na kuabudu.
Leo imezinduliwa rasmi vita dhidi ya dhambi ya uzinzi hapa  kanisani. Katika vita hii hakuna kuangalia usoni, hakuna kubagua mchungaji au mshirika, hakuna kubagua mtendakazi wa siku nyingi na aliyeokoka hivi karibuni.  Yeyote anayefanya matendo ya uzinzi kanisani ajue kuwa katika kanisa hili hapa siyo sehemu yake. Hata kama itabidi kanisa zima kuhamishwa kwa kuwepo kwa wazinzi wengi, bado itakuwa njema kwa sababu ni afadhali  wawepo watakatifu wachache kweli kweli  kanisani kuliko  kuwepo na idadi kubwa ya waumini wanaoenda kuzimu  na wasio na sifa za kwenda mbinguni. Katika MITHALI 28:13Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema”. Haijalishi wewe ulipokuja kanisani ulikuwa na tabia zipi  hapo  awali. Haijalishi maisha yako ya nyuma yalikuwa mabaya kiasi gani,  kwa sababu Biblia inasema “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.” (2WAKORINTHO 5:17).

Kila mtu anapookoka anapaswa KUACHA mambo fulani-fulani ya hapo awali katika maisha yake. Kuacha siyo kwa sababu huwezi kuyafanya tena. La hasha. Unaamua kuacha kwa sababu wewe ni sehemu ya mwili wa Kristo. Njia ya utakatifu ndiyo pekee iliyo njia ya mafanikio. Paulo ameandika katika 1WAKORINTHO 5:9-11Naliwaandikia katika waraka wangu, kwamba msichangamane na wazinzi. 10 Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang'anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia. 11Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye”. Kwa maandiko haya, Paulo anatumia neno “NDUGU” kumaanisha mtu aliyeokoka na aliyepo kanisani. Wazinzi wa dunia hii hatuwatengi, wala siyo lengo letukuwatenga, bali tutawatenga wale waitwao NDUGU KATIKA KRISTO (Walokole Kanisani) kwa sababu hao ndiyo wanaolinajisi hekalu la Bwana.


2.      MAZINGIRA YANAZOKARIBISHA DHAMBI YA UZINZI.
Yapo mazingira ya yanayoandaliwa na watu wawili hadi kufanyika kwa uzinzi. Namna ya uvaaji wa mavazi, nayo ni njia mojawapo ya kuleta ushawishi wa uzinzi. Kazi kubwa ya nguo ni kuusitiri mwili (wa mwanamke na mwanaume) na pia kumfanya  mtu apendeze. Usipoyakabili mazingira ya dhambi  ujue utakufa tu.

Matembezi ya kijana chumbani kwa binti au binti kumtembelea kijana wa kiume chumbani kwake hilo halikubaliki. Haipaswi kwenda kumfundisha mshirika mpya masomo ya awali chumbani kwake, bali masomo kama haya yafanyikie kanisani. Kijana wa kiume ni  ruksa kutoa huduma ya  maombezi kwa kijana mwenzake wa kiume na vivyo hivyo  kwa vijana wa kike kuhudumiwa na vijana wa kike. Linda sana utakatifu uliopo ndani mwako kwa sababu kitu alichokiweka Yesu ndani mwako ni cha thamani zaidi ya vitu vyote.

3.      BAADHI YA MADHARA YA UZINZI KIBIBLIA
a)     Uzinzi huangamiza nafsi yako mwenyewe. Katika MITHALI 6:32 imeandikwa kuwa “”. Kwa kuwa mtuni roho, inayokaa kwenye nyumba ya udongo ambayo  ni mwili, wenye nafsi. Kwa hivyo mtu yeyote afanyaye uzinzi, unakuwa umearibu  mwili na nafsi kwa wakati mmoja.

b)     Uzinzi hukaribisha mashetani ndani mwako. Imeandikwa katika UFUNUO 18:2-3 (Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza; 3 kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake).

c)     Uzinzi huangamiza mwili wako mwenyewe. Ndivyo ilivyoandikwa katika  1WAKORINTHO 6:18-19 maneno haya (Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. 19 Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;). Ndiyo maana magonjwa ya zinaa humuingia mtu.


Showers of Glory Morogorogo wakicheza mbele za Bwana Yesu.

d)     Uzinzi humfanya mtu kuingia mkataba na shetani na kukufanya uangamie kabisa. (1WAKORINTHO 6:15-16 - (15 Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha! 16 Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.). Kwa kuwa kitendo hicho humfanya mtu kuunganishwa,kinachotokea ni kuwa kunakuwepo na muunganiko wakudumu kabisa na mashetani.



Kanisa lisilo na utakatifu siyo kanisa bali ni kibanda tu. Kanisani ni mkusanyiko wa wenye dhambi wa zamani.

Endapo yupo mtu miongoni mwetu aliyekuwa mtenda uasherarti au uzinzi, leo Yesu anataka kumsaidia mtu wa aina hiyo kwankukubali kutubu dhambi hizo. Imeandikwa katika MITHALI 28:13Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema”. Hii ni fursa pia kwako wewe ambaye hujaookoka ufanye maamuzi ya kuokkoka ili kuwa na ujasiri wa kuikimbia zinaa na tamaa zake kwa kwa Jina la Yesu.

========== AMEN ========

KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI WASILIANA NASI KIPITIA:
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: pastor:dr.godson
TEL: +255 719 798778 (WhatsApp & Sms only)

BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/
Share:
Powered by Blogger.

Pages