JUMAPILI: 19 APRILI 2015 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
Majeshi ya Bwana Morogoro wakiwa na furaha kubwa mbele za Bwana wa Mabwana. |
Kile kitu unachokitafuta kipo, na Mungu alishakupatia hata kabla ya
kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu. Binti au kijana unayetafuta mwenza, au wewe
unayetafuta mtaji wa biashara, au wewe unayetafuta matibabu ya ugonjwa wako, ni
baadhi ya vitu ambavyo tayari
ulishapatiwa na Mungu ingawa hujavipokea kwa sababu ya uwepo wa wazuiaji (watu wasiofaa).
Mfano wa Kibiblia: 1 WAFALME
21:1-10, imeandikwa hivi…[Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli
alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya
Ahabu mfalme wa Samaria. 2 Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba
lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu;
nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda,
nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. 3 Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana
apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. 4 Basi Ahabu akaenda nyumbani
kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na
Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani
pake, akageuza uso wake, akakataa kula. 5
Lakini Yezebeli mkewe akamwendea, akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni
hata usile chakula? 6 Akamwambia, Kwa sababu nimesema na Nabothi Myezreeli,
nikamwambia, Unipe shamba lako la mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa
shamba la mizabibu lingine badala yake. Akajibu, Sitakupa shamba langu la
mizabibu. 7 Yezebeli mkewe akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa
Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la
mizabibu la Nabothi Myezreeli. 8 Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu,
akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye
nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi.9 Akaandika katika
zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele
ya watu, 10 mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia,
kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili
afe.]…Hivi ndivyo wanadamu walivyo: wanapoangalia mafanikio ya watu
wengine (shamba la mizabibu), hujadiliana ama waibe hayo mafanikio unayomiliki au wakuue. Kinachowahangaisha ni
hicho kitu ulicho nacho. Wapo watu
hawalali usiku kwa sababu tu wameona kiti chako ofisini mwako, au wameona watoto wako wanasoma shule
nzuri, au wameona ndoa yako ilivyo na amani n.k. na matokeo yake wanakereka kwa
wivu.
Kikao cha ‘watu wasiofaa’ wanamtumia shetani kama mwenyekiti wao. Mimi
ninaye mwenyekiti wa kikao cha kuwazuia ‘watu wasiofaa’, ambaye ni Mungu
mkuu kuliko miungu yote. Huyu Mungu wangu huweka kikao na watu wake ili kuwazuia ‘watu wasiofaa’, kwa
sababu Mungu wangu anaona vile vya sirini. Mchana wa leo tunawafuatilia wabaya
wote waliokaa vikao na shetani na kuwaharibia mipango yao kwa Jina la Yesu.
Wapo watu wasiofaa kwenye maisha. Hawa hawafanyi kazi, ila hukaa vikao
kutafuta namna gani wataiba mashamba (mafanikio) ya wengine. Ni hao ambao wakiona ndoa za watu ni nzuri
huvizia na kuanza kutaka kuzivuruga hizo ndoa kwa wivu wao. Watu hawa wanasahau
msemo wa Kiswahili usemao, ‘Ukiona
vyaelea vimeundwa’. Jina lako linaweza kujadiliwa kwenye vikao
vya wachawi, na wakafikia maazimio ya kukuharibia, kuanzia kazini,
nyumbani, kwenye biashara zako n.k.
Mungu humpa mwanadamu ushindi wa maisha yake tokea pale mwanadamu anapozaliwa,
lakini wengine wasiofaa wanapoona hayo maisha huyatamani, kama ambavyo Ahabu alilitamani shamba la Nabothi. Yeremia alijulikana hata
kabla ya kuzaliwa kwake. Mungu alishaandaa mazingira yote ya mwanadamu kabla ya
kutungwa mimba, na ndiyo maana Mungu humpa mtu
hatima yake hata kabla ya kuwepo duniani.
Siyo mpango wa Mungu mwanadamu aishi kwa taabu. Maandiko yanasema ‘Adui za mtu ni wale wa nyumbani
mwake’. Ni wale watu anaoongea nao kila siku. Ni wale mnaokutana nao kila siku, na ndiyo maana Biblia inawaita ‘ni watu
wasiofaa’. Mganga wa
Kienyeji na Wachawi ni watu wasiofaa katika
jamii kwa sababu wao ndio wanaokaa vikao hivi na kujadili majina ya wengine
ili wale wanaojadiliwa waishi maisha ya
taabu. Mungu ameniambia, ‘Atanibariki
niingiapo na nitakapo’, sasa iwe je leo hizi Baraka sizioni? Ni kwa
sababu wapo watu waliovuruga mipango yangu.
Katika Mhubiri imeandikwa ‘kuna majira na saa kwa kila jambo’. Saa ya kupita katika ugumu imefika mwisho. Ni saa ya Bwana kutenda. Uliniambia nisubiri nikiwa na miaka
20, hivi sasa imetimia miaka 40, lazima
nipate hicho kitu sasa, siyo wakati wa
kusubiri tena. Lazima aliyezuia hatima yangu aachie kwa Jina la Yesu. Wewe
uliyekaa kwenye njia zangu, jua kuwa naachia mishale ya moto nao ina macho ya
kupiga sawasawa. Imeandikwa ‘Amelaaniwa
yeye azuiaye upanga wake kumwaga damu’ na mimi leo naachilia upanga
wangu kumwaga damu ya wewe unayenizuia kufikia hatima yangu katika Jina la Yesu.
Katika Biblia tunaona kuwa ‘kila mfalme mtata hukumbana na Nabii mtata’.
Akiinuka Ahabu, Mungu humuinua Eliya ili kumdhibiti swasawa na ujeuri wake. Angetokea
Nabii Yeremia, asingeweza kumshughulikia Ahabu kwa sababu Yeremia angelia lia
tu. Lakini mfalme Ahabu kwa ujeuri wake alikumbana na Nabii Eliya, jeuri
mwenzake aliyezuia mvua kunyesha kwa miaka mitatu na nusu. Gideoni alipokumbana
na yule Jemedari, hakumkimbia bali alimuuliza, ‘je wewe upo upande wetu
au upo upande wa adui zetu’.
Maana yake ni kuwa, endapo huyu jemedari angemwambia yupo upande wa adui,
Gideoni angemmaliza pale pale.
Kuna wakati Mungu alichungulia jeshi la Wamisri ili awaangamaize. KUTOKA
14:24-25…[Ikawa katika zamu ya
alfajiri, Bwana akalichungulia jeshi la Wamisri katika ile nguzo ya moto na ya
wingu, akalifadhaisha jeshi la Wamisri. 25 Akayaondoa magurudumu ya magari yao,
hata yakaenda kwa uzito; na Wamisri wakasema, Na tukimbie mbele ya Israeli; kwa
kuwa Bwana anawapigania, kinyume cha Wamisri.]…. Kitendo hiki
cha Mungu kuchungulia hili jeshi, lilisababisha matairi/magurudumu ya magari ya
Wamisri kuachia, na matokeo yake wakaangamizwa. Ni maombi yetu siku ya leo,
kila anayekuonea katika maisha yako, Mungu amchungulie na kumshughulikia kwa
Jina la Yesu.
Kama wewe hujaokoka, kwa kumpa Yesu maisha yako, ni siku nzuri kufanya
hivyo ili Mungu aweze kukupigania kinyume na hao wanavuruga maisha yako.
© Information
Ministry (Ufufuo Na Uzima - Morogoro)
Mtaa wa Nguvu Kazi,
(Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.
/or
Contact our Senior
Pastor:
Dr. Godson Issa Zacharia
(Ufufuo Na Uzima – Morogoro)
Cellphone: (+255) 757
550878 / +255 719798778