Tuesday, September 9, 2014

THIS IS MY STORY: Ushuhuda wa Kichaa cha Naomi

THIS IS MY STORY   -  JUMAPILI  07.09.2014

Mwalimu Malinga na mke wake, wameokoka muda mrefu sana na ni wakazi wa Bigwa Morogoro. Kabla ya tukio hili, Mzee Malinga alikuwa Kiongozi (Mzee wa kanisa) katika Kanisa la TAG - Moria (lililopo Mtaa wa Kola B - Morogoro).


Mzee Malinga (katikati), mkewe (kushoto) na Baba
(SNP Dr. Godson), wakati familia hii  ikishuhudia
matendo makuu ya Mungu kwa mtoto wao Naomi.
Familia hii wana mtoto anayeitwa Naomi, ambaye alifaulu vizuri form 4, na tarehe 27 March 2014 ilikuwa birthday yake. Hata hivyo, Jioni ya hiyo siku ya tarehe 27 March mwanae alianza kuona watu ambao walikuwa wanamfuata sebuleni ingawa baba yake alikuwa hawaoni. 


Katika wale watu aliokuwa anawaona miongoni mwao ni  majirani za familia hii, na ambao watoto wao hawakuwa wamefaulu kama Naomi mitihani yao ya form 4. 


Usiku ule Naomi (mwanae) alikuwa anakimbia kimbia ovyo, na kumgongea mlango baba yake kwani alikuwa akisumbuliwa na wale wachawi. Maajabu Naomi alikuwa na macho ya kuona watu ambao wasioonekana kwa baba yake waliokuwa wanamvizia. Ndiposa Baba yake aliwaza pengine ni malaria imepanda kichwani kwa mwanane. 


Kuna wakati baadae baba alitaka kumsaidia mwanae, lakini looh, Naomi akamwambia baba yake kuwa ameshachelewa kufanya hivyo kwani yupo mtu aliyekuwa anamfuata akimvizia kutaka kumchinja na kisu keshaondoka zake tayari!!!!. Mzee Malinga alimuombea mwanae, na kukemea mapepo, lakini hali ya Naomi haikuonesha matumaini!!!


Mama mzazi wa Naomi alikuwa ameenda Moshi kipindi hiki cha kuanza kwa hili  tatizo. Baba yake Naomi usiku ule ilibidi  ampeleke Naomi kwa Mchungaji wa TAG (Moria) ambapo ndipo anapoabudu, na akafanyiwa maombi, kisha wakazimia kumuacha kwenye hii nyumba ya mchungaji. Hata hivyo mwanane kuanzia siku ile alikuwa halali kabisa usingizi wowote zaidi ya kusumbua na kupiga kelele.


Siku moja Naomi alitoroka na alipopatikana alipelekwa hospitalini, akapimwa malaria, ingawa alikutwa hana tatizo kubwa la malaria, kwani hakuwa na vimelea vya malaria vyenye kuhitaji matibabu. Madkatri walikiri kuwa idadi ya malaria aliyo nayo ni  ya kawaida sana kwa watu wengi na haina madhara. Hata hivyo alimuanzishia dawa ya malaria. 



Siku iliyofuata alipatiwa tiba nyingine ya 'quinine' na kila mara akawa anaongezewa dozi. Madakatari walikiri aina hii  ya malaria haijawahi  kufahamika kwao au kuwepo kwenye taaluma zao za matibabu. Madaktari  walipendekeza pengine Naomi aanzishiwe dozi ya wenye vichaa. 


Dozi hii alianzishiwa kidogo, lakini pia wazazi na madaktari wakapendekeza kuwaona watumishi wa Mungu kwa maombi. Muhimbili ikawa sehemu ya mwisho, na ambapo madaktari walipoisoma ile  historia ya Naomi walishauri kama wazazi wanataka kwenda kwa waganga wa kienyeji sawa, au makanisani kuombewa sawa, wafanye hivyo!!!. 


Wazazi walimpeleka Majumba Sita  Dar es Salaam na akaombewa penye kanisa la TAG, na baada ya maombi, Naomi akawa ametulia na kulala. Walimuacha mwanae mahali pale akiombewa, na huku ile hali ikawa inamrudiarudia kila baada ya  siku. 


Muda wa Naomi kwenda shuleni  ukawadia,  na wazazi wakaenda kumchukua kutoka huko Dar es Salaam. Hata hivyo fujo ziliendelea  kuwa kubwa zaidi, na Naomi alikuwa akitaja majina ya watu wakubwa serikalini (majina yao yanahifadhiwa), na hata wasanii kama akina Marehemu Kanumba n.k. Naomi alipotajiwa kwenda shule,  ndipo aligoma katakata  na kusema hana mpango wa kwenda shuleni tena.


Wapo ndugu waliomshauri Mzee Malinga ampeleke Naomi huko Moshi - Kilimanjaro,  eti kwa sababu kule kuna sehemu inayofahamika sana yenye maombi mazito ya uponyaji. Mzee Malinga kwa kujali hali aliyokuwa nayo mwanae alifunga safari kwenda Moshi na Naomi. Safarini ilibidi amfunge miguu mwanae ili asimtoroke kama alivyokuwa anamtoroka, ukizingatia kuwa endapo Naomi angetimua mbio mzee huyu na umri wake kamwe asingeambulia kumpata. Njiani mzee Malinga alipata shida sana kusafiri na Naomi, kwani kuna wakati Naomi alikuwa anakataa kufuatana na baba yake na hata kunyanyuka kwenye kiti ndani ya basi  na kuanza kucheza nyimbo za TV ya lile basi bila ya aibu, tena mbele ya abiria wote!!!.  


Mbaya zaidi,  Naomi akiwa njiani alikuwa anapiga makelele akiambia abiria wenzake kuwa baba yake  anataka kwenda kumtoa kafara, jambo ambalo lilifanya abiria waingilie kati na kutaka kujua kulikoni!!!!? Mzee Malinga aliwajibu na kujitetea kwa ushahidi wa kimatibabu asije akapata kipigo!!!


Walipofika Moshi, mzee huyu alikodi Guest House na chumba chenye 'double beds' ili kuhakikisha kuwa mwanae hatatoroka usiku ule, lakini  loh, mwanane akagoma kulala mle akipiga makelele kuomba msaada,  akisema kwamba baba yake amefanya hivyo ili apate nafasi ya kumbaka. Baba huyu alijisikia vibaya sana na aibu ikawa inampata. Palepale  Baba yake  alipewa wazo na wahudumu wa ile guest la kwenda kutafuta chumba kwenye hosteli ya masista pale Moshi Mjini na ambapo  mwanane alikubali kulala pale hosteli.


Kesho yake alimpeleka mwanae  kwa 'Yule  Mtu wa Maombi'. Mzee Malinga anakiri kuwa toka amekulia wokovu hakuwahi kukutana na aina hii ya maombi. Kwa nini!!!? Anasema ni aina ya  maombi ambayo mwanae aliambiwa aizunguke madhabahu,  na kisha huyu 'Mtu wa Maombi' akamnywesha maji ambayo hata Mzee Malinga hakufahamu yana kitu gani ndani yake. Hata hivyo maombi yale katu hayakumsaidia mwanae.


Walirudi Morogoro, ikabidi wazazi hawa wampeleke upya Naomi Hospitalini, na ambapo madkatari kwa kujua historia ya Naomi walishauriana kumuanzishia huyu mtoto dozi ya kutuliza watu wenye kichaa.  Pale hospitalini hata hivyo, alikuwepo Dr. Loice wa Hospitali ya Saba saba (Majeshi Majeshi wa Ufufuo na Uzima Morogoro).  Huyu daktari aliwashauri wazazi hawa wampeleke Naomi Kanisani Ufufuo na Uzima Morogoro,  kwani alibaini kuwa tatizo kama hili tiba yake siyo ya Hospitalini, bali ni  kwa 'Kanisa lenye maarifa ya kiroho'. 


Hata hivyo, wazazi walikuwa na 'Taarifa Hasi' dhidi ya Kanisa hili toka zamani. Walijishauri sana juu ya wazo hilo, wakisema endapo makanisa yote waliyokwenda kuanzia Morogoro, Dar es Salaam na kwingineko shida ya Naomi haikutatuliwa,  je, Kanisa la Ufufuo na Uzima, tena lililopo Kihonda watawezaje? 


Kwa shingo upande wazazi hawa walitii na kesho yake wakafika kanisani hapo Ufufuo na Uzima - Morogoro ambapo walipokelewa vizuri na maombi kwa Naomi yakaanza rasmi. Kuanzia siku ile, Naomi alianza kufunguliwa na kuanza kurudiwa na ufahamu wake. Kipindi hiki ni katikati ya Mwezi Julai 2014. Kwa kuona vile, haikuchukua muda, wazazi wakawa wanamleta Naomi kwenye Mkesha na Ibada za katikati ya wiki, na hadi kufikia katikati ya mwezi August 2014, Naomi alikuwa mzima kabisa wa afya na  akaomba apelekwe shuleni!!!.



Baba na Mama wa Naomi Malinga wakitoa sadaka ya
Shukrani na Dictionary ya Biblia kumshukuru Mungu
aliyemponya Naomi kutoka kwenye Maradhi /
Ukichaa wa kutengenezwa  07/09/2014.
Wazazi wa Nomi kwa pamoja  wanakiri kuwa Naomi amepona kabisa na sasa amejiunga na Shule ya Sekondari Mpanda na hata walimu wake wanapiga simu wakisema kuwa Naomi ni mzima kabisa. 


Baba na mama wa Naomi wameamua "mchana kweupe"  kujiunga rasmi na Kanisa la Ufufuo na Uzima Morogoro. Wamehuzunishwa sana na tuhuma na 'Taarifa Hasi'  zilizokuwa zinafanywa dhidi ya Kanisa hili kulichafua zikisema kuwa ni mojawapo ya makanisa ya 'Free Mason'. Wazazi hawa kwa pamoja wamesema kuwa wapo tayari kumtumikia "Mungu wa Ufufuo na Uzima" kwa matendo ambayo wameshuhudia Mungu huyu akifanya, na zaidi sana kwa kumponya Naomi. Sifa na Utukufu - Apewe Bwana wetu Yesu Kristo. Amen.


© Information Ministry (Ufufuo Na Uzima - Morogoro)
==(Cellphone: (+255) 713 45 95 45)==


Share:
Powered by Blogger.

Pages