Sunday, August 24, 2014

SOMO: ROHO YA KUZAA MAPOOZA-Na: Dr. Godson Issa Zacharia (SNP)

Baba (SNP Dr. Godson) na Mama (RP Happiness) wakimsifu
Bwana Yesu mwanzoni  mwa ibada tarehe 24/08/2014 katika
Nyumba ya Ufufuo na Uzima Morogoro.
Utangulizi: Somo la Jumapili ya leo  linaitwa “Roho ya Kuzaa mapooza”. Kuzaa mapooza maana yake ni kuzaa vitu  vilivyokufa au kisichokuwa na uhai.  Kwa jina linguine ni kutozaa kabisa (barrenness). Ni sawa na kupukutisha.


MALAKI 3:11…[Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi.]…maana ya kupukutisha matunda kabla ya wakati wake ni sawa na  kuzaa mapooza. Tunda pooza ni  tofauti na lile tunda halisia linatazamiwa kuwepo. Unaanzisha mradi wako / biashara na kabla ya kupata kile ulichotarajia huo mradi au biashara inakufa.


2 WAFALME 2:19 …[ Watu wa mjini wakamwambia Elisha, Angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza.]… Ina maana halikuwepo  pingamizi la muonekano wa ule mji, kiasi  kwamba hata Elisha mwenyewe alikuwa shahidi wa kile kinachozungumziwa.

Ifuatayo ni  mifano ya kuzaa mapooza:
1.0.                       “Mtumishi  wa Mungu Elisha, watoto wangu hawa ni wazuri sana kama unavyowaona, lakini  wakifika kipindi cha kuolewa hawapati waume”…. Hili ni pooza.

2.0.                       “Mtumishi  wa Mungu Elisha, hii kazi ni nzuri lakini inabidi ukipewa hii kazi sharti tukutane grand loudge ili ukutane na wenzetu wa freemasonry kufanya nao mazungumzo”…… Hili ni pooza.

3.0.                       “Binti nipo tayari kukupa hii kazi, bila hata kufanya interview, lakini itabidi jioni  tukutane guest house ile karibu na X ili tufanye mazungumzo zaidi”. Kazi ni nzuri sawa, lakini ujue ndani yake kuna mapooza.

MAOMBI: Kwa Jina la Yesu Ninakataa roho ya kuzaa mapooza kwenye maisha yangu, katika Jina la Yesu.

2WAFALME 2:20-22 …[Akasema, Nileteeni chombo kipya, mtie chumvi ndani yake. Wakamletea. 21 Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, Bwana asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza. 22 Hivyo yale maji yakapona hata leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena.]… Kuzaa mapooza na Kufa huenda pamoja.  Nyakati nyingine ni sawa na kuzaa kisicho na uhai.  Mtu aweza kuwa na biashara Fulani, na ghafla ushuru kwa hiyo biashara unapandishwa bila maelezo, na matokeo yake inakuwa ngumu kuendelea na ile biashara.


MP Albano wa Nyumba ya Ufufuo na Uzima Morogoro
akihakikisha maandiko kwenye Biblia kujua "Nini asili ya
kuzaa mapooza
" Jumapili ya tarehe 24 August 2014.
Familia zingine zina kuwa na watoto wenye akili  sana, lakini hakuna hata mmoja anayefika  elimu ya form 4. Maana yake ni kuwa "Mwanzo ni mzuri lakini mwisho wa safari hizi unakuwa mapooza".

NINI  ASILI YA KUZAA MAPOOZA?

Asili yake ni rohoni. Shetani anafahamu kuwa Mungu hapendi mapooza kuwepo. Ndiyo maana hata Elisha alitaka watu wa mji wampeleke hadi kwenye chanzo cha hayo maji yenye kuleta mapooza. Elisha hakuwaambia watu wa mji wamuoneshe mazao yatokanayo na maji ya mapooza. Kila pooza kwenye maisha yako lina chanzo chake, na hicho chanzo ni cha rohoni. Chanzo cha rohoni  huanza na wasimamizi wa rohoni ambao ni mashetani kwa asili  yao.


Baba (SNP Dr. Godson - mwenye shati Jeupe), akimfungua
Mmoja wa watu wenye Roho ya Mapooza tarehe 24/08/2014 
MAOMBI: Leo nimeamua kushambulia kila chanzo cha roho cha kuzaa mapooza kwenye maisha yangu katika Jina la Yesu. Roho  yoyote iliyopandwa kwenye maisha yangu naifuata kwa Jina la Yesu. Ewe roho ya kuzaa mapooza nakung’oa kwa Jina la Yesu.

Kuzaa mapooza kunatafuna muda wako. Wapo wanaosema 'usipokuwa tajiri hadi miaka 40 usahau kabisa'. Hii ni kwa sababu watu  wanajua muda wako  uliobaki  ni mchache, labda wewe uwe mwana wa Ufufuo  na Uzima,  ambao hawafi.

MALAKI 3:7…. [Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande, mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi,   nami nitawarudia ninyi, asema Bwana wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa namna gani?]…. Yeye atiaye uhai ni  Yesu. Kumbuka kufa na kupooza huenda pamoja. Yesu anasema “nirudieni mimi,  mmeniacha toka enzi za babu zenu”. Kitendo cha kutokuwa na Yesu kinamfanya yule alaye apate nafasi ya kupukutisha. Maana yake ni kuwa unakuwa umeshamiri kwa habari ya mapato halafu ghafla kila kitu kinaisha. Unakuwa umeshamiri katika masomo lakini ghafla unaanza kupata sifuri-sifuri kwenye kila somo. Unakuwa na watoto wako wazuri lakini ghafla wanaanza kuugua na kufa mmoja hadi mwingne.

MAOMBI: Leo nimedhamiria kukukimbilia wewe Yesu na kumpinga shetani. Aliyeingia kwenye maisha yangu akala vile nilivyopewa na Bwana namfyeka kwa Jina la Yesu. Roho ya kuanza kitu na kikaharibika, ngo’oka kwa Jina la Yesu.


Kutolipa Zaka ni mojawapo ya mambo ambayo Mungu  ameyataja kama "Laana ya kupukutisha".

Majeshi ya Bwana wakisikiliza kwa makini kujua "Laana ya
Kupukutisha
" itokanayo na kutolipa Zaka (Fungu la kumi)
MALAKI 3:8-10…[Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani?  Mmeniibia zaka na dhabihu. 9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. 10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.]… Kumbe ukileta zaka kamili nyumbani mwa Bwana, unamfanya Mungu azuie laana kutokuwepo katika nyumba yako. Yamkini wapo wanaopata mshahara kiasi  sawa na wewe na wana nyumba zao wamejenga, lakini wewe unaishi nyumba za kupanga tu hadi leo. Kumbe yupo yule alaye mshahara na furaha yako. Hao ndio wanaokutafuna wewe.

Kivipi? Yamkini unapata mshahara kiasi sawa na watu wengine,  lakini ghafla unapigiwa simu kwamba ndugu yako fulani ameugua huko kijijini na pesa inatakiwa haraka. Utakachofanya ni kuzituma hizo  pesa, bila kujua huo ni mtego wa yule alaye ili pesa yako ipukutike.

Kitendo cha kukataa ni kitendo cha  ujasiri dhidi ya roho ya  mapooza. Ni  vyema kukataa kuwa na hizo roho za mapooza. Endapo unaanza mahusiano ya ndoa yanapukutika, kataa. Unapokuwa unaanza biashara nayo inakufa kabla ya kuleta faida,  kataa hilo roho la mapooza.

MAOMBI: Nakataa kupata na kupoteza kwa Jina la Yesu. Ninakataa hasara kwenye maisha yangu. Nakataa kupata kazi na kufukuzwa. Nakataa Roho ya mauti, Nakataa roho ya mapooza, Nakataa kunyanga’anywa kile nilicho nacho kwa Damu ya Yesu, chochote kilichopandwa ndani yangu ili nipooze nakikataa kwa Jina la Yesu.

Kupukutisha maana yake ni kama vile unapokuwa na miti ya matunda na imezaa vizuri, na unakuwa umekadiria faida utakazopata ukeshauza matunda yale. Lakini  ghafla unatokea ugonjwa au upepo na matumaini yote yanaishia papo hapo.

MAOMBI: Ewe upepo wa kisulisuli uliotumwa ili  upukutishe mayai ndani ya tumbo langu, leo nakufyeka kwa Jina la Yesu. Upepo  wa kichawi uliotumwa upukutishe msaada  wangu, leo nakuagiza kwa Jina la Yesu simama. Mganga yeyote wa kienyeji,  uliyetumwa kupukutisha furaha yangu, leo nakushinda kwa Jina la Yesu.

Majeshi ya Bwana Nyumba ya Ufufuo na Uzima Morogoro
wakishangilia baada ya Maombi na kuwekwa huru dhidi ya
Roho ya Mapooza tarehe 24/08/2014.
Bwana anataka akurejeshe kwenye furaha yako kuanzia leo.  Wapo wale wanaokula furaha yako.  Ukipata furaha wiki  hii,  wiki inayofuata  inakuwa yenye huzuni.




MAOMBI: Yeye alaye nakung’oa kwa Jina la Yesu. Mapooza ya kazi,  mapooza ya mahusiano, mapooza ya fura yangu ng’ooka kwa Jina la Yesu.






==Information Ministry (Ufufuo Na Uzima - Morogoro)==
==(Cellphone: (+255) 713 45 95 45)==




Share:
Powered by Blogger.

Pages