Monday, February 29, 2016

Somo: KITABU CHA UKUMBUSHO CHA WANAOMTUMIKIA BWANA


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH

UFUFUO NA UZIMA - MOROGORO

JUMAPILI – 28 FEBRUARI 2016

Na: Dr. Godson Issa Zacharia (SNP)

 

Somo: KITABU CHA UKUMBUSHO CHA WANAOMTUMIKIA  BWANA

 

Mungu kule mbuinguni anatunza kumbukumbu za watu wake kwenye vitabu, na vitabu hivi viko vingi. Kitabu cha ukumbusho cha wanaomtumikia Bwana hiki huandikwa kule mbinguni na kuweka kumbukumbu ya kazi ulizozifanya humu duniani. Hata sasa hivi yapo mambo yako yanayoendelea kuandikwa juu yako. Hakiandikwi ufikapo kule mbinguni, bali huandikwa kabla ya kwenda mbinguni.

 

Imeandikwa katika WAFILIPI 4:5…[Naam, nataka na wewe pia, mjoli wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami, na Klementi naye, na wale wengine waliotenda kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima.]…. Walioandikwa kwenye kitabu cha uzima hiki, ni wale walioishindania Injili.

 

Imeandikwa UFUNUO 20:15…[Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.]….Kitabu hiki cha uzima nacho pia kimeandikwa na Mungu.

 

Imeandikwa katika UFUNUO 21:27…[Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha MwanaKondoo.]…Mtunzaji wa hiki kitabu cha uzima ni Mwanakondooo.  Hii ni kama Diary ya Mwanakondoo.  Kwa nini watu waandikwe humu? Ni kwa sababu watu wanaoandikwa humu ni wale walioikataa dunia na kumfuata Bwana Yesu. Ni watu waliokataa machukizo na aina zote za dhambi, na kuamua kumtumikia Mungu pekee. Siyo kila mtu huandikwa humu bali wale tu waliofanya maamuzi.

 

 

Imeandikwa katika DANIELI 12:3..[ Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.]…. Kumbe ukimtumikia Mungu utang’aa kama nyota ya  milele. Hiki nacho ni Kitabu maalumu kwa wale wanaomtumikia Mungu. Huu ni ukumbusho kwa yale ambayo Mungu atawafanyia watu wa aina hii wakiwa duniani na baadae wakiwa mbinguni.

 

 

JE, KUMTUMIKIA MUNGU MAANA YAKE NINI?

Tafsiri za kumtumikia Mungu ni kama zifuatazo:

(a)  Kumtumikia Mungu siyo kuwa mchungaji, au askofu au  padri  au mwinjilisti n.k. Kumtumikia Mungu pamoja na yote yaliyotajwa ni kumsujudia na kumwamini Mungu  peke yake.

 

Imeandikwa katika KUTOKA 23:25…[Nanyi mtamtumikia Bwana, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako.]…. Kwa maana yake kibiblia, kumtumikia Mungu ni kumsujudia Mungu peke yake, kumwabudu yeye (kwa kuachilia mambo yote na kumtegemea yeye peke yake). Imeandikwa katika MATHAYO 4:10...[Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.]

 

(b)  Tafsriri ingine ya kumtumikia  Mungu ni kumtii Bwana na kumtegemea YEYE PEKE YAKE. Siyo Bwana akuite njoo na wewe uanze kutoa visingizio lukuki.

 

Mfano mzuri ni maisha ya Ibrahimu. Pamoja na kuwa na mwana mmoja tu Isaka,  lakini Ibrahimu hakusita kuitii sauti ya Mungu na kudhamiria kumtoa mwanae sadaka. Kwa sababu ya imani na utii wake, Ibrahimu anaitwa Baba wa Imani.

 

Imeandikwa katika YOSHUA 22:5…[Lakini mjibidiishe sana kuzifanya amri na sheria, ambazo Musa, mtumishi wa Bwana, aliwaamuru, kumpenda Bwana, Mungu wenu, na kwenenda katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na kushikamana na yeye, na kumtumikia kwa moyo wenu wote na nafsi yenu yote.]… Yaani kumtumikia Mungu ni kushikamana naye, na kuenenda na njia zake zote.

 

 

(c)  Tafssiri nyingne ni Kumpenda Mungu. Imeandikwa katika LUKA 10:27…[Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.]….Bila kujali una umri  gani,  umetoka ukoo gani, unaumwa au huumwi,  una fedha au hauna, unapaswa kumependa Mungu jinsi ulivyo. Maadamu upo duniani na una nguvu, unapaswa kumtumikia  Bwana.

 

 

(d) Tafsiri ingine ni kushikamana na Mungu.

 

 

(e)  Tafsiri ingine ni kuzishika amri zake zote. Imeandikwa katika KUMBUKUMBU 10:12-13….[Na sasa, Israeli, Bwana, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche Bwana, Mungu wako, na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote; 13. uzishika amri za Bwana na sheria zake, ninazokuamuru leo, upate uheri?]….Unapozishika amri za Bwana, na kumwamini kwa moyo wako  wote na  nguvu zako  zote,hiyo ndiyo klumtumikia Mungu. Kumbuka kwamba Mungu wetu ni mwenye wivu na haruhusu wewe uabudu  vitu vingine vyovyote isipokuwa Yeye Peke Yake.

 

 

JE, KUMTUMIKIA MUNGU KUNA FAIDA YOYOTE?

Watu wengi wanaosema kwamba hakuna faida ya kumtumikia Mungu wapo. Hii ni kwa sababu watu wa aina hii wanapokumbana na mateso au magumu huanza kujiuliza maswali ya umuhimu wa kuendelea kumtumikia Mungu wa aina hii. Lakini Mungu  huyu huyu ni yule aliyeigawanya Bahari  ya Shamu,  na hivyo hawezi kushindwa kukutana na shida ya mmtu yeyote.

 

Imeandikwa katika MALAKI 3:14-15…[Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi? 15 Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.]… Hawa watu wameyashika maagizo ya Mungu yote, na sasa wanawaza kuna faida gani‼ Hawa waovu wanaoonekana hapa wakiwa wamenawiri, siyo kwamba mali zao hizi hutoka kwa Mungu bali ni kwa sababu ‘wamemtii shetani’, naye akawapa mali za dunia hii.

 

 

Imeandikwa katika LUKA 4:5-7…[Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. 6 Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. 7 Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako.]….Ukiona mtu anakupa kitu maana yake, hicho kitu kipo mikononi mwake. Shetani anazo mali mikononi mwake,  mali zile alizoziiba. Kumbe hata sasa wapo watu waovu wenye mali na miliki za ajabu ajabu nyingi sana kwa sababu wameamua kuinama na kumsujudia Ibilisi. Ndiyo  maana Yesu alimuita shetani kuwa ni “mungu wa ulimwengu huu

 

 

Imeandikwa katika MALAKI 3:16-17…[Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao. 16 Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. Naye Bwana akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake. 17 Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia,kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye.]….  Mungu aliwasikia  wanaomtumikia na akaandika majina ya hawa wamtumikiao kwenye  kitabu. Walioandikwa kwenye  hicho kitabu, watakuwa:

·        Watu wa Mungu

·        Hazina za Bwana.

·        Atawaachilia kama amabvyo  mtu amwachiliapo mwanae

 

NINI KILIMFANYA MUNGU AANDIKE KITABU CHA UKUMBUSHO?

Imeandikwa katika MALAKI 3:18…[Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, na kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia.]…. Mungu alikiandika kitabu hiki ili kutenganisha kati ya waovu na wenye haki. Lazima tofauti zetu ziwe bayana. Ikiwemo balaa lolote, wengine hata kama litawapata lakini wewe unayemtumikia Bwana uwe hai kwa Jina la Yesu. Mungu ukimtumikia, hawezi kukuchanganya wewe na waovu.

                                                           

 

Imeandikwa katika MALAKI 4:1-3…[Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi. 2 Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake; nanyi mtatoka nje, na kuchezacheza kama ndama wa mazizini. 3 Nanyi mtawakanyaga waovu; maana watakuwa majivu chini ya nyayo za miguu yenu; katika siku ile niifanyayo, asema Bwana wa majeshi.].… Mungu anawatazamia hao waovu kuzipata stahili zao kwa Jina la Yesu. Na watu waliomtumikia Mungu kwa uaminifu watafurahi  kwa kucheza cheza kama ndama wa mazizini.

 

Kwa hiyo zipo faida za kumtumikia Mungu. Imeandikwa katika KUTOKA 23:25-27… [Nanyi mtamtumikia Bwana, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. 26 Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza. 27 Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao.]…. Yapo mambo kadhaa ambayo huwezi kuyapata kwa njia ya maombi, bali kwa kumtumikia Mungu tu:

 

 

Mfano wake ni mambo haya, ambayo Mungu atakufanyia pale umtumikiapo:

(a)  Mungu atabariki chakula chako: Maana yake Mungu atakuwa amekupatia chakula. MARKO 16:18-17… [Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; 18 watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya].

 

(b) Mungu atabariki  maji

 

(c)  Mungu ataondoa ugonjwa katikati yetu: Kuna tofauti kati  ya kuponya magonjwa na kuondoa magonjwa. Maana ya kuondoa nikuhamisha. Madaktari wana uwezo wa kuponya magonjwa siyo kuyaondoa. Mungu pekee ndiye anayeweza kuyaondoa magonjwa kwa kuyatupa nje (suppress).

 

Imeadikwa katika KUMBUKUMBU 7:15…[Na Bwana atakuondolea ugonjwa wote; wala hatatia juu yako maradhi yo yote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao.]…Magonjwa ni roho, na Mungu yupo tayari kuyahamishjia maroho haya kwa maadui zako. Kumbuka imeadikwa pia kwamba “Kila pando asilopanda Baba wa Mbinguni yatangolewa”. Kwa hiyo endapo upo ugonjwa kati yako,  Bwana anao uwezo wa kuungoa na kuupeleka kwa wale wakuchukiao kwa Jina la Yesu.

 

 

(d) Hapatakuwepo na mwenye  kuharibu mimba. Kuharibu mimba maana yake,  kile ulichokusudia kizaliwe hakitazaliwa. Ndivyo ilivyo hata katika  masomo, maana yake, utasoma lakini katikati ya masomo  yako unasimamishwa masomo yako.

 

 

UKIRI
Ninakataa vitu vyangu kuanza na kuharibika, ninakataa kuanza na kuharibika uchumba, ninakataa kuanza na kuharibika masomo, ninakataa kuanza na kuharibika elimu,  nakataa kwa Jina la Yesu. Amen
 

 

 

(e)  Hapatakuwepo na mwenye utasa: Kuwa tasa ni kukosa uwezo wa kuzaa. Shetani anapoona kuwa ameshindwa katika hatua ya mimba, hupenda pia kufuatilia ili mtu akose kabisa uwezo  wa kuzaa.  Hata hivyo ukimtumika Mungu, imeahidiwa kuwa hapatakuwepo mwenye utasa.

 

(f)   Mungu atazitimiza siku zako: Hizi siyo siku  za kuishi tu.ikummbukwe kuwa,  Mungu alipokuumba, alikupangia namna ufanisi wako utakavyokuwa ufikapo umri fulani. Mathalani, Mungu anakuwa amekupangia kuwa ufikapo  umri wa miaka 35-70 ufanikiwe, uwe na maisha ya aina fulani lakini shetani akawa  amezuia yote haya yasitokee. Endapo mtu ukimtumikia Mungu,  atakusaidia kuzifanikisha siku zako hizi, na kupata yote kwa wakati, bila kucheleweshwa na shetani.

 

(g)  Mungu atatuma utisho wake ukutangulie: Huu utisho ni wa kibiblia. Maana yake, wasiokutakia mema hata wanapokujadili kwa ubaya,  pindi ufikapo kwenye hivyo vikao watatishwa na uwepo wako na kukupa haki zako.

 

(h) Mungu atawafadhaisha wale utakaowafikilia: Mahali popote utakapofika, utasababisha adui zako  wafadhaike wakuonapo.

 

(i)    Mungu atawafanya adui zako wakuoneshe maungo yao: Kama yupo adui yeyote kwako, maana yake atakimbia mbele zako na kukuacha kwa Jina la Yesu.

 

 

Yoshua alifanya uchaguzi na kusema, yeye na nyumba yake watamtumikia Bwana. Hata wewe leo hii unayo nafasi ya kufanya uchaguzi, wa nani wa kumtumikia. Ni vyema kuchagua kumtumikia Mungu kwa sababu zipo faida za kumtumikia Mungu wetu.

 

 

©  MEDIA & INFORMATION MINISTRY,
GLORY OF CHRIST (T) CHURCH
MOROGORO CHURCH
Share:
Powered by Blogger.

Pages