Sunday, June 15, 2014

SOMO: MADHABAHU YA WACHAWI IMEPASUKA - Na: Pastor Dr. Godson Issa Zacharia (SNP)

JUMAPILI: 15 JUNE 2014 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO

Utangulizi: Somo letu  linaitwa “Madhabahu ya wachawi imepasuka”. Madhabahu ni mahali/ au sehemu /au ni  daraja linalounganisha ulimwengu wa mwili na ulimwengu wa  roho. Katika madhabahu kuna mawasiliano kati  ya ulimwengu  wa mwili na ulimwengu wa roho. Daraja linalounganisha maeneo haya mawili linaitwa MADHABAHU. Vitu vinavyoonekana kwa macho ya kawaida vimo katika ulimwengu wa mwili. 

Katika uumbaji,  Mungu aliumba vitu vinavyoonekana na vile visivyoonekana. Vile viumbe visivyoonekana kama vile bacteria, virus n.k. havionekani kwa macho kwa sababu ya maumbile yao kuwa madogo sana. Ndiyo maana watu hutumia darubini ili kuvikuza viumbe hivi na kisha huweza kuviona kirahisi. Viumbe vingine ambavyo Mungu aliviumba kama vile malaika, havionekani kwa macho ya mwili, si kwa sababu ya udogo wa maumbile yao bali  kwa sababu ni viumbe vya rohoni. Viumbe vya rohoni navyo vimo katika  makundi mawili: viumbe vitakatifu (mfano: malaika wema) na viumbe wachafu (mfano: majini, mapepo, mashetani n.k).


1 WAFALME 13:3…. [Akatoa ishara siku ile ile, akasema, Hii ndiyo ishara aliyoinena Bwana, Tazama, madhabahu itapasuka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.].. 


Abramu / Ibrahimu  alimjengea Bwana Madhabahu: 

MWANZO 12:7… [Bwana akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu Bwana aliyemtokea.]…. 

Baada ya hapo, Ibrahimu akaliitia Jina la Bwana penye ile madhabahu aliyojenga: 

MWANZO 13:4….. [napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu akaliitia jina la Bwana hapo.]. 

Musa pia aliijenga madhabahu:

KUTOKA 17:15….[Musa akajenga madhabahu, akaiita jina lake Yehova-nisi* (Yehova-nisi maana yake ni Bwana ni bendera yangu); akasema, Bwana ameapa; Bwana atakuwa na vita na Amaleki kizazi baada ya kizazi.]…

Gideoni naye pia alimjengea Bwana madhabahu: 

WAAMUZI 6:24…  [Ndipo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu hapo, akaiita jina lake, YehovaShalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri.].  

KILA MADHABAHU INAYOJENGWA,  INAKUWA NA SIFA 5 ZIFUATAZO:-
1.      Madhabahu yenyewe. Madhabahu yaweza kuwa imejengwa kwa ajili ya Mungu wa Mbinguni au ikawa imejengwa kwa ajili ya mashetani na mawakala wake.
2.      Kuhani wa madhabhu. Kwa upande wa kanisa kama hapa,  Mchungaji anakuwa kwenye nafasi ya Kuhani wa madhabahu.  Wachawi nao wanakuwa upande wa pili kwa kufanyika kuhani wa madhabahu ile ya shetani.
3.      Kafara ya madhabahu. Kwa mtu aliteokokolewa hakuna haja ya kufanya kafara yoyote ile kwa sababu Mungu alimtoa Yesu kuwa kafara.
4.      Nguvu ya madhabahu. Kadiri Madhabahu inavyotoa kafara nyingi ndivyo ambavyo nguvu ya madhababhu inavyoongezeka. Wachawi hutofautiana kwa kadiri ya nguvu zao. Wachawi hutoa kafara za wanyama (kuku,  njiwa n.k). hata hivyo wachawi hhuongeza nguvu zaidi hata kutoa kafara ya wanadamu na matokeo yake kafara zao zinakuwa na nguvu zaidi ya wachawi waliotoa kafara ya njiwa.
5.      Mungu wa madhabahu. Mungu baba ndiye Mungu wa Madhabahu kama hii ya kanisa, na shetani  ndiye mungu wa madhabahu zote za kichawi.

1 WAFALME 13:1-10 …. [Na tazama, akatoka mtu wa Mungu katika Yuda kwa neno la Bwana, akafika Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa akisimama penye madhabahu, afukize uvumba. 2 Basi mtu huyo akapiga kelele juu ya madhabahu, kwa neno la Bwana akasema, Ee madhabahu, madhabahu, Bwana asema hivi, Angalia, mtoto atazaliwa katika nyumba ya Daudi, jina lake Yosia; na juu yako atawachinja makuhani wa mahali pa juu, wanaofukiza uvumba juu yako, na mifupa ya watu itateketezwa juu yako. 3 Akatoa ishara siku ile ile, akasema, Hii ndiyo ishara aliyoinena Bwana, Tazama, madhabahu itapasuka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika. 4 Ikawa, mfalme Yeroboamu alipoyasikia maneno ya yule mtu wa Mungu, alipopiga kelele juu ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono wake pale madhabahuni, akasema, Mkamateni. Basi ule mkono wake aliounyosha ukakatika, wala hakuweza kuurudisha kwake tena. 5 Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa Mungu kwa neno la Bwana. 6 Mfalme akajibu, akamwambia yule mtu wa Mungu, Umsihi sasa Bwana, Mungu wako, ukaniombee, ili nirudishiwe mkono wangu tena. Yule mtu wa Mungu akamwomba Bwana mkono wa mfalme ukarudishwa tena, ukawa kama ulivyokuwa kwanza. 7 Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu. 8 Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa; 9 maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la Bwana, kusema, Usile chakula cho chote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia. 10 Basi akaenda zake kwa njia nyingine, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.]… Hapo awali Mungu alitoa maagizo ya jinsi MADHABAHU yake itakavyojengwa. Hata hivyo,  wafalme/viongozi mbali mbali wa Israeli walienda kinyume na neno la Mungu baada ya kuwafukuza makuhani wa Mungu na kuwaleta makuhani wa kichawi ambao waligeuza madhabahu ya Mungu kuwa madhabhu ya miungu wengine, akiwemo Dagoni.

ISAYA 19:19-20 …[Katika siku hiyo itakuwako madhabahu katika nchi ya Misri kwa Bwana, na nguzo mpakani mwake kwa Bwana. 20 Nayo itakuwa ishara na ushuhuda kwa Bwana wa majeshi katika nchi ya Misri; kwa maana watamlilia Bwana kwa sababu ya watu wawaoneao, naye atawapelekea mwokozi mwenye kuwatetea, naye atawaokoa.]… Ni wazi kuwa, unahitaji madhabahu ya kukutetea pale ulipo. Kama vile wachawi wanaendea madhabahu zao za uharibifu, vivyo hivyo wewe na mimi tunahitaji madhabahu ya kutuunganisha na Jehovah Mungu wetu mbinguni. Madhabahu yaweza kuwa mahali kama hapa kanisani. Lakini  pia, madhabahu nyingine ni wewe binafsi.

1 KORINTHO 3:16-17…  [Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? 17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.]… Sin is temporal but its destruction is permanent (Dhambi ni  ya kitambo tu lakini  uharibifu wake ni wakudumu). Acha dhambi. Usikubali kudanganywa na kutenda dhambi. Mungu hawezi kuukaa mahali  pachafu.  Yesu anagonga mlango wa moyo wako ili  aingie kwako. Lakini endapo moyo wako umejaa dhambi, Mungu hawezi kuingia kwako. Kuwa mtakatifu ni jambo rahisi. Kila anayemkubali Yesu Kristo maishani mwake,  Yesu huingia ndani yake na kuwa Mungu wa madhabahu yake.

Ili Mungu aijenge madhabahu yake ndani yako lazima ile iliyopo ibomolewe.  Kawaida ni kuwa, madhabahu mbili hazikai pamoja. Mungu anataka kuijenga madhabahu yake Misri (yaani kwa mataifa).

MAOMBI: Kwa Jina la Yesu, ewe madhabahu ya wachawi na wasoma nyota uliyejengwa ndani yangu, pasuka kwa Jina la Yesu.

UTAJUAJE KUWA MADHABAHU YA WACHAWI IMEJENGWA NDANI YAKO?
1.     Utaota ndoto unaelea angani kama una mbawa. Unaota unakimbia juu kabisa kama vile una mbawa. Hicho ni kituo cha magonjwa ndani yako.

MAOMBI: Kwa Jina la Yesu ewe madhabahu uliyejengwa ndani yangu, bomoka kwa  jina la Yesu.

Kwa nini ijengwe ndani yako? Kwa sababu ni  rahisi wao kuifanya kazi yao kirahisi. Ni rahisi wachawi kutumia kigoda na kukukalia. Ingekuwa imejengwa kwenye mbuyu kwa ajili yako, ingechukua muda kukufuatilia.

2.   Kuharibikiwa na kila unachokifanya. Hata watu huanza kusema, “Ukitaka mambo yako yafanikiwe, usimhusishe mtu Fulani”. Ukipata kazi, inaharibika. Chochote unachokifanya hakifanikiwi.

MAOMBI: Kwa damu ya Yesu, ewe madhabahu, ya uchawi, ewe madhabahu unayevuvia uharibifu ndani yangu. Ewe madhabahu, ewe madhabahu, --- Bomoka.  Ewe madhabahu ewe madhabahu, uliyekaa kwangu, madhabahu ya utasa, ya ugonjwa, ya kukosa kazi--- Pasuka.

Madhabahu ilipopasuka, majivu yake yalimwagika (1 WAFALME 13:3). Madhabahu za wachawi huiba akili,  ufahamu na kuvificha vyote. Mungu anaagiza kwanza madhabahu  hizi za kichawi zipasuke kwanza ili ziteme vibali, afya,  akili  za watu n.k.   

Wapo watu wengine wamekuwa wakitumika kwenye madhabahu za kichawi bila hiari yao. Leo tunataka kuzipasua hizo madhabahu kwa Jina la Yesu. Wachawi waliokutega wakatike mikono na madhabahu zao zipasuke, na majivu yao yawarukie wenyewe kwa Jina la Yesu.

MAOMBI: Kwa damu ya Yesu, nakataa ushirika wangu kwenye madhabahu za wachawi, kwa Jina la Yesu. Kila aliyepanda madhabahu ndani yangu,  mikono yake ivunjike kwa Jina la Yesu, madhabahu yake ipasuke na  majivu ya madhabahu yake yamrukie kwa Jina la Yesu.



==Information Ministry (Ufufuo Na Uzima - Morogoro)==
Share:
Powered by Blogger.

Pages