JUMAPILI: 21 JUNE 2015 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
Utangulizi:
Ili
mtu akusaidie au uweze kuongea nae lazima upate kibali machoni pake. Imeandikwa
katika MWANZO 39:21…[ Lakini Bwana akawa pamoja
na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza.]….
Umuhimu wa kibali upo palepale. Ili
maisha yangu yakae vizuri na sawa, lazima nipate kibali mahali fulani. Hata
kama ninafanya biashara mahali fulani, kama watu hawapati kibali cha kuja kwenye biashara
yangu, hakuna nitakachoweza kukifanya
kikafanikiwa. Kwanza jiulize, Umepata kibali wapi ili ufanye nini? Umepata kibali wapi ili
ufanye biashara wapi? Shetani anao uwezo wa kuibadilisha sura yako ya nje kiasi
kwamba mtu wa pembeni akikuangalia anakuona ukiwa mtu wa ajabu ajabu tu. Wewe
binafsi huwezi kushtukia hilo, ila mtu mwingine anachokiona ndani ya ufahamu
wake anakuona tofauti. Mathalani, endapo unajiona uko safi, lakini mwenzako
anakuona u mchafu, hata kama ungejitetea vipi haitasaidia, kwa sababu mtazamo wa ndani ya ufahamu wake mtu
huyo ni tofauti na wewe. Waswahili husema ‘Uzuri wa mtu upo kwenye macho ya
watu wengine siyo wewe binafsi’. Vivyo hivyo
Uzuri wa bidhaa upo kwenye macho ya mnunuaji wala siyo muuzaji.
Adui anaweza
kuibadilisha sura yako au hata usemi wako.
Maana yake, unapoongea tu inaweza kutafsiriwa tofauti na yule anayesikia
usemi wako. Shetani anafahamu kuwa umeokoka, na hivyo hawezi kukugussa
wewe lakini badala yake atamvuruga mtu yule unayetaka kukutana naye ili akunganishe
na hatima yako. Kumbuka ujenzi wa mnara wa Babeli jinsi ambavyo Mungu mwenyewe alikiri
kuwa kwa namna ile ya kusikilizana kwa wanadamu, asingekuwepo wa kuwazuia mpango wa hawa
wanadamu walivyokuwa katika umoja na sauti moja. Ilimpasa Mungu achafue usemi
wa hawa wanadamu ili kwamba kila anachokiongea kila mmoja wao kieleweke tofauti na mwenzake.
Ndicho anachokifanya shetani hata sasa katika maisha ya wanadamu. Pengine ni
neno dogo tu linazungumzwa kataka maisha yenu ya ndoa lakini kwa neno hilo ndoa
inavunjika. Hii ni kwa sababu shetani anachezea usemi wao ili kupoteza kile
kibali cha ndoa, kwa kuwachafulia semi
zao ndani ya ndoa.
Unapoona kazini kwako unafukuzwa ujue ni kibali chako kimechezewa. Unapoona kwenye
ndoa yako mambo hayaendi vizuri ujue ni
kibali kimechezewa. Unapoona kazini watu wanakusema sema ovyo au
kudharauliwa unapoongea jambo lolote ofisini mwako ujue ni kibali kimechezewa.
Ni lazima leo tuvifuate vibali vyetu kule viliposhikiliwa na adui zetu kwa Jina
la Yesu. Lazima kila nikiongea watu
waseme huyu ni Bwana. Kama wazo langu halishindi maana yake hata mimi mwenyewe
nimeshindwa. Ili kazini kwangu niweze
kusifiwa kwa kile ninanachokifanya lazima nipate kibali. Ukiona mtu asiye na
kibali ujue kwa lugha nyepesi huyo mtu
amelaaniwa. Biblia inasema “kibali cha
mtu humketisha na wakuu”.
Shetani ana uwezo wa kuchezea kibali cha mtu na kukishikilia mahali, na kila
atakachokifanya mtu wa aina hii kinakuwa kigumu na kisichompendeza mtu yeyote. Kibali kinapokamatwa ujue maisha nayo
yanakuwa yamekamatwa.
KUTOKA
33:12…[Musa akamwambia Bwana, Angalia, wewe waniambia, Wachukue
watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini
umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu.]….
Musa alianza kujiuliza maswali kujua ni kwa mamlaka gani atawapeleka Israeli
Kanaani. Ni rahisi sana kusema neno
“neema” bila kujua maana yake. Katika Agano Jipya, Paulo anasema aliwekewa miiba na adui, na baada ya kuomba mara nyingi
iondoke, Bwana akamwambia “Neema yangu
yakutosha”. Katika MWANZO
6:8 imeandikwa…[Lakini
Nuhu akapata neema machoni pa Bwana.].... Kilichomuokoa Nuhu
asiangamie na ile gharika ni neema (yaani Upendeleo wa Kimungu). Neema ya Mungu ndiyo kibali. Ni kwa sababu kupitia neema hii unapata
kibali kisichobishaniwa. Ndiyo maana hata katika Nyaraka za Paulo katika Agano
Jipya, Paulo anamalizia hizi nyaraka kwa kusema ‘Neema ya Bwana wetu Yesu
Kristo ikae nanyi”, akijua kuwa Neema ya Yesu Kristo ndiyo kibali.
YOHANA
1:14…[Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona
utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na
kweli.]… Yesu Kristo alitupa neema isiyobishaniwa. Leo ni siku
ya kulivaa vazi la neema, ili kila nitakapokaa, nipate kibali machoni pa
wengine. Ipo neema ya kuingia popote unapotaka kuingia. Haijalishi umefanyiwa
uchawi wa aina gani, ninachokijua lipo vazi la neema ya Yesu Kristo
nitakapolivaa hayupo wa kunipinga wala kunizuia. Vazi hili alilivaa Musa
nyakati zile kiasi kwamba watu wakamwita
yeye ni Mungu katikati ya wanadamu. Kilichompa Musa kibali ni ile neema.
KUTOKA 33:13-16…[Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata
neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele
zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. 14 Akasema, Uso wangu
utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. 15 Naye akamwambia, Uso wako
usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa. 16 Kwa maana itajulikanaje
kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda
pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa
nchi?]… Kama alivyosema Musa,
hata sisi inabidi tuseme hivyo hivyo. Inakuwaje leo maombi yangu
hayapati kibali machoni pa Bwana? Kuna
vazi (la rohoni) ambalo ukilivaa, afya yako
inakuwa tofauti. Kila ulivaapo vazi hilo, milango yote iliyokuwa haifunguki itafunguka kwa
ajili yako. Tunaihitaji neema ya Mungu ili kanisa liinuke. Tunahitaji neema ya
Mungu ili kuiharibu misingi ya shetani katika taifa hili. Ni saa ya Bwana kunivalisha vazi la neema ili
nikipita popote, milango ikafunguke yenyewe, siyo kwa sababu ya elimu yangu
bali ni kwa sababu ya neema ya wokovu
ndani mwangu. Hilo vazi la aibu ulilo nalo, vazi la kuitwa “msengenyaji”, au “asiyeolewa” n.k. leo ulivue kwa Jina la
Yesu. Ukilivaa hilo vazi la utukufu hata
waliokudharau watakushangaa. Soma habari za Esta, kilichomfanya apate kibali kwa mfalme siyo sura yake, bali ni kwa sababu alikuwa na vazi la neema
ya Bwana.
Musa alimwambia Mungu siwezi kuongea vizuri, lakini tazama
mtu huyo huyo ndiye ambaye Mungu alimtuma aende kwa Farao, ni kwa sababu
kinachomfanya Musa aongee siyo elimu yake wala akili au nguvu zake, bali kwa sababu anayo neema itokayo kwa Baba wa
Mbinguni.
ZABURI
68:7-10…[Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa
wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu.7 Ee Mungu,
ulipotoka mbele ya watu wako, Ulipopita nyikani, 8 Nchi ilitetemeka Naam,
mbingu zilidondoka usoni pa Mungu; Hata Sinai usoni pa Mungu; Mungu wa Israeli.
9 Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu. 10
Kabila yako ilifanya kao lake huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku
walioonewa.]… Daudi anaonesha kuwa wana wa Israeli na safari yao
kutoka Misri hadi Kanaani, haikuwa kwa sababu wanajua sana kutembea, bali ni
kwa sababu ya neema tu. Mungu ndiye aliwavisha Adamu na Eva mavazi yaliyotokana
na ngozi ya mnyama. Wao wenyewe walijisitiri kwa majani, wakasahau kuwa baada
ya muda, jua litayanyausha hayo majani nao watarudia kuwa uchi tena‼!
Katika Biblia, Stefano aliwashinda maadui zake kwa neno, alipoweza kuisoma (kwa ufupi)
Biblia yote kuanzia Mwanzo hadi Ufunuo ndani ya ukurasa mmoja. Hajawahi kuwepo
mtu aliyemtumaini Bwana katika Biblia yote ‘Mwanzo hadi Ufunnuo’ mtu huyo
akakosa neema. Kinachowapa watu mafanikio siyo elimu zao bali ni neema. Usikate tamaa wewe ambaye
watu wanakusema vibaya, bali waambie baada ya muda mfupi tu watasema ‘hakika
wewe ni Mwana wa Mungu’. Hata askari yulee aliyemchoma Yesu mkuki, mwishowe ilimpasa
kukiri ya kuwa ‘hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu’
Imeandikwa KUTOKA
33:17 … [Bwana
akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema
mbele zangu, nami nakujua jina lako. ]…. Mungu anatujua kwa
majina yetu. Je, uliwahi kumuona mfalme bila vazi la kifalme?
Hata wewe, saa yako imefika ya kuvalishwa vazi la kuheshimika, Vazi la Baraka.
Ninachokijua mimi ni kuwa ninalo vazi la kunitoa katika maisha ya shida, na ya kuonewa, nay a kuvuta bangi na kuingia katika maisha
mapya katika Jina la Yesu Kristo wa Nazareti.
Kama mtu hujaokoka huwezi kulivaa hili vazi la neema
ya Bwana. Kuokoka kwa kumpokea Yesu Krsito maishani mwako kuwa Bwana na Mwokozi wako ni hatua ya kwanza ili kuweza kupokea
kibali cha Bwana na kuwashinda adui zako wote.
UKIRI
Ewe vazi la kushindwa, leo ninakukataa kwa Jina la
Yesu. Ninakataa vazi la kichawi, vazi walilonipa wazazi, vazi litokalo
kuzimu nalikataa kwa Damu ya Mwanakondoo. Vazi la kunifanya nionewe, mavazi ya urithi na ya uganga wa kienyeji
nayakataa kwa Jina la Yesu. Leo nayakataa mavazi niliyovishwa ili niwe malkia
wa kuzimu, nakataa mavazi yenu kwa Damu ya
Mwanakondoo. Nakataa vazi la umaskini,
vazi la magonjwa nililovishwa kwa Jina
la Yesu. Vazi la bibi nalipiga.
Nazivua nguo za rohoni walizonivisha
wachawi nyakati za usiku, nayakataa mavazi yao yote kwa Jina la Yesu. Ninakataa
mavazi ya wafu. Nalivua vazi lenu. Vazi la kukataliwa nalivua kwa Jina la
Yesu. Vazi la ukoo la kushindwa nalivua kwa Damu ya Mwanakondoo. Achia maisha yangu ewe
vazi la kuzimu kwa Jina la Yesu.
Nalikataaa vazi lolote nililovishwa kwenye msiba
nililopewa wakati wa msiba. Leo nalikataa kwa Jina la Yesu.kila vazi
linalohusiana na wafu, leo nalivua kwa Jina la Yesu.
Nalivaa vazi la neema ya Bwana, nalivaa vazi la hashima, vazi la upendeleo,
vazi la kuonekana, vazi la kupata kazi, vazi la utajiri, vazi la kusifiwa na
kuinuliwa katika Jina la Yesu. Amen
|
===© Information Ministry ===
(Ufufuo Na Uzima -
Morogoro)
Mtaa wa Nguvu Kazi,
(Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.
/or
Contact our Church
Leadreship:
Bishop Dr. Godson Issa Zacharia
(Glory of Christ (Tanzania) Church inMorogoro)
Cellphone: (+255)
765979866 /or +255 713459545.