GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH
UFUFUO NA UZIMA - MOROGORO
JUMAPILI: 17 APRIL
2016
Na: STEVEN NAMPUNJU (RP)
Katika dunia tunayoishi, zimekuwepo siku
za aina nyingi sana, mathalani siku ya watoto, siku ya akina mama, siku
ya wazee n.k. Kwa kawaida, kwa kila siku za aina hii, jamii hukusanyika na kuadhimisha tukio la
hiyo siku. Siku nzima ni mjumuisho wa saa 24.
Mwanadamu naye anazo siku zake za
kuishi hapa duniani kwa mujibu wa maandiko.
MWANZO
6:1-3.....”Ikawa
wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao,2 wana
wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake
wo wote waliowachagua. 3 Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu
milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na
ishirini.”.....Mungu alipomuumba mwanadamu, hakumwekea ukomo wa maisha
yake. Maasi na dhambi zilipoongezeka, Mungu aliamua kuweka kipimo cha kuishi
kwa mwanadamu huyo aliyemuumba, kwa kuwa hawezi kushindana na mwanadamu milele.
AYUBU
14:1-2...
“Mwanadamu
aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za
kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. 2 Yeye huchanua kama vile ua, kisha
hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala
hakai kamwe”...
Mwanadamu hana siku nyingi za kuishi hata abweteke. Hata hivyo pamoja na uchache wa siku za
mwanadamu, Ayubu anasema zimejaa taabu (magonjwa, mikosi, vifo vya utata n.k.).
Leo Mungu anataka kuuleta ukombozi katika
maisha ya watu kwa Jina la Yesu.
Maandiko yanasema katika ZABURI 103:15...”Mwanadamu siku zake zi kama
majani; Kama ua la kondeni ndivyo asitawivyo.”
AYUBU
10:20.....”Je!
Siku zangu si chache? Acha basi, Usinisumbue, nipate ngaa kutuzwa moyo kidogo.”....Mungu leo anataka alete matumaini kwa uliyepoteza tumaini
kwa Jina la Yesu.
Maandiko mengine yanasema katika ZABURI 144:44....”Binadamu amefanana na ubatili,
Siku zake ni kama kivuli kipitacho..”..
Watendakazi wa Ufufuo na Uzima Morogoro wakiwa wanasikiliza maelekezo kabla ya maombi Jumapili 17/04/2016 |
KWA
NINI TUJIFUNZE KUHUSU SIKU ZA MWANADAMU?
1. Ni kwa sababu Mungu tayari ametupangia muda wa siku za
kuishi, na hivyo ndani ya siku hizi wapo wanaotaka kuzipunguza ili zisitimie
kama ambavyo Mungu wetu amekusudia.
Endapo mtu
anakufa katika kifo cha utata, maana yake mwanadamu huyu ambaye ni roho iliyopanga katika nyumba iitwayo mwili, atakuwa hakuzitimiza zile siku za
kushi alizompangia Mungu. Katika 1WAKORINTHO
15:40...”Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake
ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali.”....
Maandiko yanasema katika KUTOKA 23:25-26...”Nanyi mtamtumikia Bwana, Mungu
wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa
kati yako. 26 Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi
yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza..”.... Kumbe inawezekana
kabisa kwa siku zako kutotimia endapo
haumtumikii Bwana. Siku za mtu kuna uwezekano zisitimie. Hata katika kazi yako, unaweza kujikuta unapunguziwa
siku za ajira yako endapo hujamtumikia Bwana inavyopaswa.
AYUBU
15:20.....”Mtu
mwovu huwa na uchungu siku zake zote, Hata hesabu ya miaka aliyowekewa mwenye
kuonea.”....
Ndiyo maana katika WAEFEZO 6:10-12 imeandikwa ....”Hatimaye, mzidi kuwa hodari
katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu,
mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. 12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si
juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya
pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”...tunafundishwa namna ya
kushindana na siku ya uovu. Hii ni ile
siku ambyo imewekwa ili kumsababishia mtu matatizo ya aina fulani.
MHUBIRI
7:1.....”Heri
sifa njema kuliko marhamu nzuri; Na siku
ya kufa kuliko siku ya kuzaliwa.”........
Maandiko yanasema katika AYUBU 7:1....”Je! Mtu hana wakati wake wa vita
juu ya nchi? Na siku zake, je! Si kama
siku za mwajiriwa?”....... Kila mtu ana wakati wake wa vita. Usimcheke
yeyote unapomuona anapigana vita,
ukasema eti hajui kupigana, kwa sababu kila mtu anao wakati wake wa vita. Na kila mtu ni kana kwamba ni mwajiriwa aliye
kazini, na usipofanya vizuri utaondolewa kwenye ajira yako. Yesu vivyo
hivyo alisema mkulima anapoliona tawi
lisiilozaa, hulikata na kulitupa nje. Msingi wa kuishi hapa duniani siyo ufanye kazi, au biashara au kuoa na kuolewa,
lahasha‼. Hayo yote ni ya ziada, bali lengo kuu la kuwekwa hapa duniani ni KUMTUMIKIA BWANA na hivyo usipofanya vizuri utaondolewa na kutupwa nje.
AYUBU
14:15.....”Kwa
kuwa siku zake zimeamriwa, hesabu ya miezi yake unayo wewe, Nawe umemwekea mipaka yake asiyoweza kuipita;”.....
Kumbe maisha ya mtu yanaweza kuwekewa “mpaka”,
na ambayo huwezi kuuvuka. Hata uwe na
fedha namna gani, huwezi kuuvuka huo mpaka. Maisha ya yule tajiri na maskini
Lazaro yanatufundisha kuhusiana na huu mpaka. Tajiri akiwa kuzimu na Lazaro akiwa kifuani mwa Ibrahimu, na katikati yao ulikuwepo
mpaka.
Vijana wa "Showers of Glory" - wakicheza na kuimba mbele za Bwana katika ibada ya Jumapili 17/04/2016 |
UKIRI
Kuanzia leo, nakuanzia sasa, kwa Jina la
Yesu, wewe uliyekamata idadi ya siku zangu, leo uniachilie kwa Jina la Yesu. Amen
|
2. Ni kwa sababu Tunataka kuzijua idadi ya siku zetu. Ule wakati wa kukaa mashimoni umekwisha kwa Jina
la Yesu. Danieli aliposoma vitabu aligundua idadi ya siku za kukaa utumwani zimekwisha. Na hata
sisi lazima tusome vitabu na kwamba zile
siku za kukaa chini ya utmwa wa shetani zinakoma kwa Jina la Yesu.
Mungu wa dunia hii (ibilisi) naye hupenda
kuweka mipaka ya siku zetu. Endapo mtu
angeweza kuona mbele ya maisha yake na
kuziona balaa zilizoandaliwa juu
yake, hakika hayupo ambaye angesukumwa kuja kanisani ili kumuomba Mungu amuepushie hizo balaa.
3. Ni kwa sababu Tunataka kuzijua siku za mwanadamu ili
tujipime na kujua jinsi gani tumekuwa
dhaifu.
Wakati mwingi hata waajiriwa huchekwa pale wanapostaafu lakini huko mtaani unawakuta hawajajenga hata kibanda cha kuishi.‼ Ni kwanini? Walipokuwa ajirani walijisahau,
wakaacha kujua kuwa siku za ajira zao
zimepimwa.
ZABURI
139:4....”Bwana,
unijulishe mwisho wangu, Na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; Nijue jinsi
nilivyo dhaifu.”.... Mtunga Zaburi anataka kuangalia umri wake wa
kuishi na kazi alizomfanyia Bwana ili
kujua je zinalingana?
Usifungwe na kazi au ndugu katika
kumtumikia Bwana. Kama alivyofanya Yusufu,
vivyo hivyo na wewe ufanye vivyo hivyo, kwa kumuachia joho yeypte
anayekuvuta ili kukurudisha nyuma katika
kumtumikia Bwana.
Imeandikwa katika 1WAKORINTHO 3:9....”Maana
sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la
Mungu.”...... Kuna mwingine ni kama shamba la Mungu, lakini endapo
Mungu anataka kupanda chochote humtumia.
1WAFALME
16:34.....”Katika
siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na
Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na
kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno
la Bwana alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.”.... Katika siku za mtu
ujenzi unaweza kuendelea. Kuna mtu anaishi, lakini kuna ujenzi anaoendeleza kuufanya
ili magonjwa yampate mtu mwingine. Kuna mtu
anaishi lakini ameandaa mpango
mbaya katika maisha ya watu wengine.
Mungu
anataka tuwe na siku nyingi,
katika ndoa, familia, ajira n.k.
Mungu wetu siyo Mungu wa siku chache. Anapoponya uponyaji anaoutoa unakuwa
endelevu.
Katika siku
za mtu fulani, mabaya yaweza kuletwa kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
Imeandikwa katika 1WAFALME 21:29....”Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu?
Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku
zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.”....
Mungu alikuwa ameshaahidi mabaya kumpata Ahabu,lakini kwa kuwa Ahabu alijidhili
Mungu akabadili msimamo wake, ila mabaya
yale yakaelekezwa kwa wana wa Ahabu.
Watendakazi wa Ufufuo na Uzima Morogoro wakiwa wanamwabudu Bwana katika Ibada ya Jumapili 17/04/2016 |
Imeandikwa katika MAOMBOLEZO 5:7....”Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na
sisi tumeyachukua maovu yao.”.... Katika maisha ya mtu, kuna wakati uovu ulitendwa na
waliomtangulia, lakini mateso yanampata mtu mwingine ambaye hakuhusika na yale
maovu.
Ni kweli
Mungu alikusudia uishi miaka 120. Lakini
shetani naye [kama mungu wa dunia hii] anaweza
kuingilia kati ilisiku zako hizi
zisitimie, endapo wewe utakuwa mtenda
dhambi.
UKIRI
Kuanzia
leo, na kuanzia sasa, mtu yeyote aliyekamata maisha yangu ili nisiwe
sawa leo niachie kwa Damu ya Yesu. Amen
|
Baba (SNP) Dr. Godson Issa Zacharia katika ibada ya Jumapili 17/04/2016 |
Kama wewe hujamwamini Yesu,leo ni nafasi yako ya kuokoka ili iwe rahisi kuzitimiza siku zako kwa Jina la Yesu.
UKIRI
Kuanzia sasa wewe uliyesimama kufupisha
siku zangu niachie. Ewe siku uliyejipanga
ili kuleta huzuni kwangu nakukataa, nguvu ya siku iliyoandaliwa kutoka
shimoni, leo niachie kwa Jina la Yesu. Yeyote aliyeanzisha ujenzi wa mateso
kwa siku zangu, au za familia yangu leo achia kwa Jina la Yesu. Nakataa leo
mamlaka za giza kwenye siku zangu.
|
© MEDIA &
INFORMATION MINISTRY,
GLORY OF CHRIST (T) CHURCH
MOROGORO CHURCH
|