Sunday, March 8, 2015

FAIDA ZA KUMTOLEA BWANA FUNGU LA KUMI-Na: ADRIANO MAKAZI (RP)


JUMAPILI:  08 MARCH 2015 - UFUFUO NA UZIMA MOROGORO


Utangulizi: Jumapili ya leo, Somo letu linaitwa Faida za Kumtolea Bwana Fungu la Kumi”. Mungu amezungumuzia aina mbalimbali  za sadaka. Zifuatazo ni aina ya hizo sadaka:


 
RP Adriano akifundisha kuhusu "Faida za kumtolea Mungu Fungu la Kumi"
katika Bonde la Maono Morogoro hapo Jumapili 8/3/2015



1.      AINA ZA SADAKA KIBIBLIA

 

                          (i).            SADAKA YA AMANI

KUTOKA 32:6….[Wakaondoka asubuhi na mapema, wakatoa dhabihu, wakaleta sadaka za amani, watu wakaketi kula na kunywa, wakaondoka wacheze. ]… Hizi ni  aina ya sadaka za kusababisha amani ndani ya nchi,familia. Ikikosekana amani mema hayawezi kukujia.

 

                       (ii).            SADAKA YA DHAMBI.

Israeli wakitenda dhambi, sasdaka hii hutolewa. Mnyama (ng’ombe au kondoo) huchinjwa ili  kufanya dhambi za wana Israeli waachliwe kwenye.

 

HESABU 6:13-14 …[Na sheria ya Mnadhiri ni hii, zitakapotimia hizo siku za kujitenga kwake; ataletwa mlangoni pa hema ya kukutania; 14 naye atasongeza sadaka yake kwa Bwana, mwanakondoo mmoja mume wa mwaka wa kwanza mkamilifu, kuwa sadaka ya kuteketezwa, na mwanakondoo mmoja mke wa mwaka wa kwanza mkamilifu, kuwa sadaka ya dhambi, na kondoo mume mmoja mkamilifu kwa sadaka ya amani,]….

 

Media na information Ministries wakiendesha vyombo/mitambo ya sauti na kuchapa Mahubiri
kwenye computer katika Bonde la Maono - Morogoro 8/3/2015



 

                     (iii).            SADAKA YA HATIA

Mtu anakuwa ametenda mambo yenye kumtia hatia, hata akataka kujiua. Yuda Iskariote, kwa mfano, alijisikia ndani mwake hatia kwa kumsaliti Bwana Yesu na mwishowe akajinyonga. Wana wa Israeli pindi wanapojisika hatia ndani ya mmioyo yaowalikuwa wanatoa sadaka ya hatia kwa ajili yao.  Cha muhimu ni kuziacha njia zako mbaya ili hatia ndani yako isiwepo. Yapo mapepo kabisa ya kutia hatia ndani yako. Hayo ndiyo huinon’goneza masikio yako kukuambia kwamba dhambi uliyoifanya ni kubwa na kwamba haiwezi kusamehewa.

 

WALAWI 5:6-7 …[naye atalipa kwa ajili ya hilo alilolikosa katika kitu kile kitakatifu, kisha ataongeza na sehemu ya tano, na kumpa kuhani; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa huyo kondoo mume wa sadaka ya hatia, naye atasamehewa.]…. Kwa hiyo aina hii ya sadaka huleta upatanisho.

 

                     (iv).            SADAKA YA HIARI

Ni sadaka itolewayo kwa Bwana kama hiari,ya kumshukuru  Bwana kwa mambo aliyokutendea. Haulazimiki kuitoa, ila ni kuonesha mapenzi mema kwa Bwana, kwamba unamjali,unapenda aendelee kukuhudumia. Biblia inasema aheri  kutoa kuliko kupokea.

HESABU 29:36….[lakini mtasongeza sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya kusongezwa kwa moto, harufu ya kupendeza kwa Bwana; ng'ombe mume mmoja, na kondoo mume mmoja, na wanakondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu saba;]…

                        (v).            SADAKA YA KINYWA

KUMBUKUMBU 32:38…[Uliokula shahamu za sadaka zao, Na kunywa divai ya sadaka zao za kinywaji?  Na waondoke na kuwasaidia ninyi; Na wawe hao himaya yenu.]…. Baadhi ya makabila wana mila zakumwagapombe ardhini, kama njia mojawapo ya kuwasiliana na mizimu.

2SAMWELI 23:16-17….[Basi hao mashujaa watatu wakapenya jeshi la Wafilisti, wakateka maji kutoka kile kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango, wakayachukua, wakamletea Daudi; walakini yeye hakukubali kuyanywa, akayamimina mbele za Bwana.  17 Akasema, Hasha, Bwana, nisifanye hivi; je! Si damu hii ya watu hao waliohatirisha nafsi zao? Kwa hiyo hakukubali kuyanywa. Hayo ndiyo waliyoyafanya wale mashujaa watatu.]….

 

                     (vi).            SADAKA YA KUINULIWA

KUMBUKUMBU 12:11…[ wakati huo itakuwa kwamba mahali pale atakapopachagua Bwana, Mungu wenu, alikalishe jina lake, hapo ndipo mtakapoleta kila kitu ninachowaamuru; sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu zote teule mtakazoweka kwa Bwana.]…. Mashambani yapo yale mazao ya kwanza kabisakuanza kukomaa, na waisraeli wallikuwa wakito aina hii ya sadaka kwa Bwana (kama Malimbuko) kuwa sadaka ya kutikiswa kwa Bwana. Maana yake, kila  kitui  cha kwanza ni cha Bwana.

 

                   (vii).            SADAKA YA KUNYWEA

Aina hii  ya sadaka hufanywa na watu, wakati mwingine akiwa mzima hakuelezi sababu yake, bali pale akienda bar na kunywa anakuwa na ujasiri wa kuja kwako na kueleza dukuduku  zake. Nyakati nyingine anakuwepo mtu amenuna moyoni mwake  kwa sababu yako. Ni vyema kukaa naye na kuyamaliza kabla ya kutoa sadaka zako mbele za Bwana.

 

Yeyote aliyeninywea mahali popopte,nageuza majeshi yamrudie mwenyewe Kwa Jina la Yesu.

 

EZEKIELI 20:28…[ Kwa maana nilipokuwa nimekwisha kuwaingiza katika nchi ile, ambayo naliuinua mkono wangu kuwapa, wakati huo walipoona kila mlima mrefu, na kila mti wenye majani mengi, walitoa matoleo yao huko, na huko walitoa chukizo la sadaka zao, na huko walifanya nukato la kupendeza, na huko walimimina sadaka zao za kunywewa.]…..

 

 

                (viii).            SADAKA YA KUSONGEZWA

WALAWI  7:30….[ mikono yake mwenyewe itamletea hizo sadaka za kusongezwa kwa moto; mafuta yake pamoja na kidari atayaleta, ili kwamba hicho kidari kitikiswe kuwa sadaka ya kutikiswa mbele ya Bwana.]….

 

                     (ix).            SADAKA YA KUTEKETEZWA

MWANZO 22:1-2…[Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. 2 Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.]….

MWANZO  8:20….[Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.]…

Nuhu aliitoa sadaka ya kutekekzwa juu ya madhabahu.

2WAFALME 3:26-27….[Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki. 27 Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe.]….

Vita ilimlemea Mfalme wa Edomu na ndipo ili ashinde vita ilimlazimu kumtoa mwanae kuwa sadaka ya kuteketezwa. Kuna watu wanatoa sadaka zao ili kuishinda vita. Hata katika taifahili letu, wapo watu wanaowania uongozi (urais, ubunge, udiwani n.k) kwa uchaguzi mkuu mwaka huu  wakitaka kushinda kwa kutoa aina hii ya sadaka.

 

                        (x).            SADAKA YA   KUTIKISWA

WALAWI 10:15….[Mguu wa kuinuliwa, na kidari cha kutikiswa, Watavileta pamoja na dhabihu zisongezwazo kwa njia ya moto, za hayo mafuta ili kuvitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; kisha vitakuwa ni vyako wewe, na vya wanao pamoja nawe, ni haki yenu milele, kama Bwana alivyoagiza.]…

 

                     (xi).            SADAKA YA SHUKRANI

Ni kuonesha shukrani mbele za Mungu.

YEREMIA 17:26…[Nao watatoka miji ya Yuda, na mahali palipo pande zote za Yerusalemu, na nchi ya Benyamini, na Shefela, a na milima, na upande wa Negebu, b wakileta sadaka za kuteketezwa, na dhabihu, na sadaka za unga, na ubani, wakileta pia sadaka za shukrani, nyumbani kwa Bwana]…

 

                   (xii).            SADAKA YA UNGA

KUTOKA 40:29…[Akaiweka madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa mlangoni pa maskani ya kukutania, akatoa sadaka ya kuteketezwa juu yake, na sadaka ya unga; kama Bwana alivyomwamuru Musa.]…

 

                (xiii).            SADAKA YA MALIMBUKO

HESABU 15:21 ….[Malimbuko ya unga wenu mtampa Bwana sadaka ya kuinuliwa, katika vizazi vyenu.]….

 

                 (xiv).            SADAKA YA FUNGU LA KUMI

Ni sadaka yenye mkataba/agano na Mungu. Na mungu ametoa maelekezo kwamba endapo mtu hatatoa aina hii ya sadaka zipo adhabu zitakazofuatia baada ya yake.

MWANZO 14:20…[Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote.]…. Hapa aina hii ya sadaka initwa fungu la kumi.

 

WALAWI 27:30…[ Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya Bwana; ni takatifu kwa Bwana.]… Hapa aina hii  ya sadaka inaitwa ‘zaka’. Ni sadaka ambayo mbele za Bwana ni ‘takatifu’,  kwa ajili  ya matumizi ya kazi ya Bwana.

 

MWANZO 28:22…[Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.]…. Ni sadaka ambayo pia hujjulikna kama fungu la kumi.

 

Kawaida, mtu akila vitakatifu vya Bwana hukumbana na adhabu. Vile uvifanyavyo vyaweza kufa, ikiwemo mifugo, kazi  n.k. 

 
"Bwana Utusamehe kwa kuiba" ni maneno ya watu hawa walioitwa mbele wakiitubia dhambi ya kutokuwa waaminifu katika kulipa fungu la kumi - katika Bonde la Maono Morogoro 8.3.2015
 

2. TARATIBU ZA UTOAJI WA FUNGU LA KUMI

Ni mpango wa Mungu wa Kuwabariki watu waliookoka.

 

MITHALI 15:8…[Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana;  Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake.]…Dhambi ni kikwazo cha kupata majibu kutoka kwa Bwana.

 

EFESO 2:8-9…[Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; 9 wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.]… Mtu hapaswi kujisifu kwamba ameshabarikiwa, kwa sababu ni kwa neema tu. Ndiyo maana baadhi  ya  watu  shida haziishi miongoni mwa waliookoka.

 

YOHANA 3:16…[Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.]… Hata uzimawa milele tulio nao unatokana na utoaji wa Mungu kwa ajili yetu.

 

Ibrahimu alitoa fungu  la Kumi (MWANZO 14:17….[Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme. 18 Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. 19 Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. 20 Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote.]…. Mungu ana uwezo wa kuvaa mwili wa kibinadamu. Melkisededki ni mfano wa aina yake katika Biblia. Tafsiri ya jina la huyu mfalme ndiyo inayotupa uhakika wa kuwa Mungu alijifunua kwa namna ya kipekee.

 

EBRANIA 7:1-3...[Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki; 2 ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani; 3 hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele.]…. Kawaida, tafsiri ya jina la mtu huwa moja, na hayupo  mtu wa kawaida awezaye kuwa na jina lenye  maana nyingi zaidi ya moja.

 

Hata katika Agano Jipya, watu walitoa fungu la kumi.

 

MATHAYO 23:23…[Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.]… Ni mpango wa Mungu kwa watu kutoa fungu  la kumi.

 
Showers of Glory Morogoro wakiimba na kumchezea Bwana Yesu Jumapili 8/3/2105 


 

3. KAZI YA FUNGU LA KUMI

Ni kuhakikisha  kuwa nyumbani mwa Mungu pana chakula.

MALAKI 3:8-9…[Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani?  Mmeniibia zaka na dhabihu. 9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. 10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo,  asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.]… Kwa hiyo mojawapo ya kazi ya fungu la kumi ni kuona kuwa kipo  chakula katika  nyumba ya Bwana.

 

Chakula kwenye nyumba ya Bwana kina maaba gani?  

YOHANA 4:34…[Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. 33 Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula? 34 Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake.]… Chakula katika nyumba ya Bwana ni kufanya kanisani pasiwe ukiwa, bali Injili ya Mungu iweze kusonga mbele.

 

4. FAIDA YA KUTOA FUNGU LA KUMI

Mungu atakaufunulia madirisha ya mbinguni. MALAKI 3:10….[Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo,  asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.]...

 

Mungu atamkemea ibilisi alaye biashara zetu,  afya zetu, ndoa yak n.k. (MALAKI 3:11…[ Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi.])….Ibilisi anakula. Kanuni inasema kuwa, Kama humtolei Bwana fungu la kumi, basi unamtolea Yule alaye. Ndiyo maana, unamkuta mtu

 

Mataifa yatakuita heri. MALAKI 3:12…[Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema Bwana wa majeshi.]… Siyo  kwamba kwa kutoa fungu la kumi,Mungu atakupa  fedha, bali atakaupa vitu vya rohoni, mfano akili nzuri, karama, ujuzi n.k ambavyo vitawafanya watu/mataifa kukuita heri.

 

5. NANI WA KUTOA FUNGU LA KUMI?

Kila mtu ana wajibu wa kutoa fungu la kumi. 1WAFALME 17:10-14…[Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. 11 Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. 12 Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. 13 Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. 14 Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.]… Siri ya kutoa siyo kwa sababu vipo vingi, bali hata katika vidogo ni muhimu kutoa fungu la kumi. Baraka zetu zimeambatanishwa na kutoa,  tena hasa kwa watumishi wa Bwana.

 

6. MSINGI WA UTEKELEZAJI KATIKA KUTOA FUNGU LA KUMI

Kwa wale wafanyabiashara, endapo umechukua mkopo wako benki kwa ajili ya bishara, unapaswa kutoa sehemu ya kumi ya ule mkopo (mfano: mkopo wa sh.100,000 funugu lake la  kumi ni shs. 10,000  na hivyo mtaji wako utakuwa shs. 90,000).  Endapo biashara hii itaongezeka kwa kutoa faida.  Mathalani  mtaji na faida umefikia sh. 150,000, cha kufanya hapo ni kuondoa ule mtaji lakini kwenye faida (sh.60,000) unapaswa kutoa fungu la kumi ambalo ni sh. 6,000. Kawaida mtaji hautolewi fungu la kumi kama awali ulishatolea fungu la kumi.

 

Mke asiye na kazi, hapaswi kuigusa pesa ya matumizi anayoachiwa na mumewe ili  iwe fungu la kumi. Kama mumewe ameshalipa fungu la kumiyatosha. Hata hivyo, mume na mke wakiwa na kazi, kila mmoja anapaswa kutoa fungu la kumi.

 

Mwanafunzi aweza kutoa fungu  la kumi  la ile  pocket money apewayo na wazazi wake. Hata hivyo haipaswi kutoa fungu la kumi la fedha ya ADA upewayo ukiwa mwanafunzi kulipa shuleni.

 
Majeshi ya Bwana Morogoro waisikiliza kwa makini kujua mambo ya kuzingatia wakati wa
kutoa fungu la kumi hapo Jumapili 8/3/2015


7. MAMBO YA KUZINGATIA


Fungu la kumi hutolewa nyumbani mwa Bwana (Kanisani) mahali  ambapo wewe ni  mshirika, unapolelewa. Halitolewi tu kila mahali, bali pale ambapo Bwana ametuelekeza.

Halitolewi kwenye mikutano ya Injili, wala kwa wajane wala kwa masikini na wagonjwa.

 

8. LAANA YA KUTOTOA FUNGU  LA KUMI


ZEKARIA 5:1-4…[Basi, nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, gombo la chuo lirukalo. 2 Akaniuliza, Unaona nini? Nikajibu, Naona gombo la chuo lirukalo; na urefu wake ni dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi. 3 Ndipo akaniambia, Hii ndiyo laana itokayo kwenda juu ya uso wa nchi yote; maana kwa hiyo kila aibaye atatolewa kama ilivyo upande mmoja, na kwa hiyo kila aapaye atatolewa kama ilivyo upande wa pili. 4 Nitaituma itokee, asema Bwana wa majeshi, nayo itaingia katika nyumba ya mwivi, na katika nyumba yake yeye aapaye kwa uongo kwa jina langu; nayo itakaa katikati ya nyumba yake, na kuiteketeza, pamoja na boriti zake na mawe yake.]…. Haijalishi wizi unaofanyika ni wa aina gani, lakini kutotoa fungu la kumi ni wizi kama wizi mwingine. Na adhabu ya mwiiz imeoneshwa hapa katika maandiko ya Biblia siku ya leo.
 

 
UKIRI
Baba Mungu naomba unisamehe, kwa kuwa nimetenda dhambi  ya kutokuwa mwaminifu kwa kutotoa zaka kamilifu,  na laana imeingia katika nyumba yangu. Leo  ninakuomba Bwana unisamehe, nilijihesabia haki kwa kuwa mimi nilikuwa sina, lakini  kumbe siri na njia ya kuwa navyo vingi ni kutoa, kwa mfano wa Yule mama mjane aliyekubali kumtengenezea Nabii Eliya mkate, na kwa kufanya hivyo hakupungukiwa na kitu.
 
Ninatubu leo dhambi ya kutokuwa mwaminifu. Nisamehe Bwana. Kuaznia leo nitakuwa natoa zaka kwa ukamilifu wake. Ponya ndoa yangu, ponya biashara yangu kwa kuwa imeandikwa akusamehe maovu yako yote na kukuponya magonjwa yako yote. Naomba Bwana Yesu unisamehe  katika Jina oa Yesu. Amen
 

 
 
© Information Ministry (Ufufuo Na Uzima - Morogoro)

Mtaa wa Nguvu Kazi, (Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.

 /or

Contact our Senior Pastor:

 Dr. Godson Issa Zacharia

 (Ufufuo Na Uzima – Morogoro)

Cellphone: (+255) 757 550878 / +255 719798778
Share:
Powered by Blogger.

Pages