Monday, July 11, 2016

Somo: VIKAO VYA MAPATANO VYA KUZIMU


GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH

UFUFUO NA UZIMA - MOROGORO

JUMAPILI:  10 JULY 2016

SNP wa Morogoro Askofu Dr. Godson Issa Zacharia 10/7/2016
 

Na: STEVEN NAMPUNJU (RP) &

Dr. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP - MOROGORO)

 

 
Tunapozungumzia VIKAO tunamanisha mikutano inayofanyika iwe ya chama au watu kadhaa wanaojadili jambo fulani. Hata katika jamii zetu, vipo vikao kama vile vya arusi, misiba, vikao vya ofisi n.k. na ambavyo kimsingi watu hukaa kwa ajili ya kujadili jambo fulani linalohusika. Kwa upande wa pili, MAPATANO maana yake ni ulinganifu wa mawazo wa pande mbili au zaidi. Endapo ulinganifu wa mawazo haupo ujue hapo hapana mapatano. Mapatano husababisha mafanikio kuwepo, na hayo yote hutegemea kama ni mapatano ya kimungu au ya kishetani.

 

 

Bibilia inaifananisha kuzimu kama nyumba, kama ilivyoandikwa katika AYUBU 17:13... (Nikitazamia kuzimu kuwa nyumba yangu; Nikitandika malazi yangu gizani) na Imeandikwa Katika ZABURI 139:8.....(Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.). Hapa Mtunga Zaburi anaifananisha kuzimu na kitanda, ambapo mtu aweza kwenda na kulala na maisha yakaendelea tu kama kawaida.

 

RP Steven Nampunju akihubiri Jumapili 10/7/2016

 

Imeandikwa Katika ZABURI 55:15...(Mauti na iwapate kwa ghafula, Na washuke kuzimu wangali hai, Maana uovu u makaoni mwao na katikati yao.). Mtunga Zaburi anazungumzia kuzimu kuwa ipo chini, kwa sababu huwezi kushuka endapo mahali pako kwa juu. ISAYA  14:9...(Kuzimu chini kumetaharuki kwa ajili yako, Ili kukulaki utakapokuja; Huwaamsha waliokufa kwa ajili yako, Naam, walio wakuu wote wa dunia; Huwainua wafalme wote wa mataifa, Watoke katika viti vyao vya enzi.).. Tunamuona Isaya naye anatuonesha kuwa kuzimu ipo chini, wala siyo juu. Imeandikwa katika MITHALI 15:24...(Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu;  Ili atoke katika kuzimu chini.).

 

 

Njia ya uhai haishuki chini, bali huenda juu alipo Bwana kwa Jina la Yesu. kuzimu inatamkwa kama nafsi yenye uwezo wa kusimama na kufanya mapatano. Imeandikwa Katika ISAYA 28:17-18... (Nami nitafanya hukumu kuwa ndiyo kanuni, na haki kuwa ndiyo timazi; na mvua ya mawe itachukulia mbali hilo kimbilio la maneno ya uongo, na maji yatapagharikisha mahali pa kujisitiri. 18 Na agano lenu mliloagana na mauti litabatilika, tena mapatano yenu mliyopatana na kuzimu hayatasimama; pigo lifurikalo litakapopita, ndipo ninyi mtakapokanyagwa nalo.).. Mapatano na kuzimu, yanafanyika, kana kwamba kuzimu na mauti wanakutana na kufanya mapatano: tumepatana kwamba mwaka huu mtu huyu hatazaaa, mtu huyu atakufa, mtu  huyu hataendelea n.k.

 

 

Imeandikwa Katika ISAYA 38:18... (Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu; mauti haiwezi kukuadhimisha; Wale washukao shimoni hawawezi kuitarajia kweli yako.). Anayesifu ni nafsi ya mtu. Kuzimu haiwezi kweli kumsifu Mungu.

 

 

Imeandikwa Katika UFUNUO 6:8...(Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu; mauti haiwezi kukuadhimisha; Wale washukao shimoni hawawezi kuitarajia kweli yako.).... Kana kwamba kuzimu ni nafsi fulani yenye uwezo wa kumfuatilia mtu na kusafirii naye, hata kama utaenda wapi.

 

 

UKIRI
Kuanzia leo, na kuanzia sasa, Ewe kuzimu unayefuatana nami, niachie kwa Jina la Yesu. Amen.
 

 
Mamia ya Washirika wa Ufufuo na Uzima Morogoro wakimshangilia Bwana Yesu 10/7/2016

 

Kuzimu pia husimama kama sehemu (Yaani mahali ambapo watu waweza kukaa na kumjadili mtu). Mpango  wowote hadi  uweze kutokea lazima vikao vya kuujadili vifanyike na mipango ya utekeleza ji wake ikapangwa. Wanadamu waliwahi kuaisi sheria ya Bwana, alivyosema kwamba wazae na kuongezeka na kuijaza nchi. Lakini, wanadamu wakaamua waujenge mnara ili wasitawanyike kama ambavyo Mungu aliwaamuru.  Kikao kilikaa mbinguni kuzuia mpango wa wanandamu, na njia sahihi iliyoamuriwa ni ya kuwachafulia lugha.

 

 

Kuzimu haihitaji upande gari au bodaboda ili kuifuata. Kuzimu ipo rohoni. Katika vikao vya kuzimu, mwenyekiti wao yupo na ambaye ni shetani. Kuzimu huwa haishibi, na mwasisi wake ni  shetani  akitenda kazi na wachawi, majini, waganga wa kienyeji, wasoma nyota n.k. Utambulisho wa watenda kazi hawa ni kama vile hirizi,  chale, ushirikina, dhambi n.k. 

 

 

Kuanzia leo naikataa kadi ya utawala wa giza, na nataka nipewe kadi ya ufalme wa Mungu kwa Jina la Yesu. Amen
 

 

 

ZIPI SIFA ZA MWENYEKITI WA VIKAO VYA KUZIMU?

 

Hizi sifa zmeandikwa katika YOHANA 10:10a...(Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.). Ukiwa mwanachama wa mwivi, malengo ya vikao vyenu itakuwa ni kuchinja, kuiba na kuharibu.

 

  • Watamuua je mtu? Hiyo hufanywa kwa kumfanya mtu asiende kanisani, au kumfanya mtu akose msaada wa aina yoyote ile.

  • Ni Kwa nini Mwivi achinje? Hii ni kwa sababu huwezi kula kitu bila kukichinja. Itakuwa maajabu endapo unataka kula nyama ya kuku halafu unamweka jikoni kabla ya kumchinja. Kazi ya kuchinja ya shetani ni katika   kuichinja familia au ndoa, ili  malengo waliyojiwekea yatimie.

  • Ni Kwa nini Mwivi aharibu? Kwa kawaida anayeharibu kabla ya yote anakuwa na malengo ya kukitumia hicho kitu anachokitamani. Hata hivyo anaposhindwa kukipata huazimia kukiharibu ili asiwepo mwenye kukitumia. Watu hawa huamua kuua ili pande zote mkose hicho kitu.

 
Wachungaji wa Ufufuo na Uzima Morogoro wakimuombea SNP Alphonse (Aliyepiga magoti) ambaye ametumwa rasmi kuliongoza Kanisa katika Wilaya ya Butiama - Mkoa wa Mara

 

UKIRI
Yeyote mwenye malengo ya kuaharibu watoto wangu au familia yangu leo nampiga kwa Jina la Yesu. Amen
 

 

 

Imeandikwa katika LUKA 22:1- 1... (Ikakaribia sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, iitwayo Sikukuu ya Pasaka. 2 Na wakuu wa makuhani na waandishi walikuwa wakitafuta njia ya kumwua; maana walikuwa wakiwaogopa watu.)... Kumbe tukio la kuua lilishapangwa, lakini watamuua je? Wakatafuta njia ambayo wakeshamuua sababu itakuwa rahisi kueleweka.

 

 

Katika LUKA 22:3-5 Imeandikwa.... (Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara. 4 Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao. 5 Wakafurahi, wakapatana naye kumpa fedha.). Ili mauti ije, katika familia yako au kazini, vikao  hufanyika na mmoja wapo. Mapatano ya vikao vya aina hii hufanyika. Yuda Iskaariote alionana na wakuu wa makuhani, kwa ujira wa fedha. Na ndiyo maana walifurahi baada ya ufanya mapatano. Katika mapatano haya, Yuda Iskariote anapatana na wakuu wa mkauhani,  kwa ujira wa vipande 30 vya fedha. Katika mapatano, huyu hujadili na upande wa pili hujadili pia hadi wanapofikia muafaka.

 

 

Imeandikwa katika YOHANA 11:38 - 44.... (Basi Yesu, hali akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango, na jiwe limewekwa juu yake. 39 Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne. 40 Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu? 41 Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. 42 Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma. 43 Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. 44 Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.)... Tunajifunza kuwa, hatupaswi  kukata tamaa. Ijapokuwa umezikwa kaburini, Yesu pia yupo kwa ajili ya kulitembelea hilo  kaburi. Endapo wachawi   wamezika kazi yako, au familia yako, au wameizika afya yako, leo  unga’nga’ne kama Raheli, usikubli kufarijiwa katika Jina la Yesu. Majaribu  uliyo nayo ni  kwa sababu ipo nyota maishani mwako.

 


 





UKIRI
Kuanzia leo, enyi mliokaa vikao vya kuzimu ili niharibikiwe,  leo mniachie kwa Jina la Yesu. Namlazimisha jini wa kila aina aliyetumwa ili ayatese maisha yangu, leo nakuteka wewe, nateka maarifa yako kwa Jina la Yesu. Amen
 

 

 

Watu hawawezi kukaa vikao kama wewe siyo mtu wa hatari kwao. Yesu walipoona kuwa anapata wafuasi wengi zaidi, vikao viliitishwa na sababu ikatolewa. Kuna watu hawataki kuzisikia habari zako. Wanapozisikia habari hizo wao hujisikia  vibaya sana. wapo watu kabisa, na ajenda zao wamezijadili kuhusu maisha yako. Hawa wamepanga njia za uharibifu, na leo lazima tuvikamate vikao vyao na kuwateka nyara. Wawe ni majirani zako, au ndugu n.k. Ndiyo maana unapomuombea mtu mwenye mateso yaliyosababishwa na vikao vya uharibifu, hujitambulisha kuwa wametumwa ili kufanya uharibifu kwa huyo mtu.

 

 

Mapatano yoyote hayafanyiki kama hakuna hatari fulani. Vikao vya aina hii  huwa vya dharura, na ajenda ikishatajwa watu hupewa majukumu ya nini cha kufanya. Hata leo hii, kuzimu huendesha vikao kama hivi ili kujadili maisha ya mtu: "Tuhakikishe ndani ya mwaka huu mtu fulani aharibikiwe". Unapomuona mtu ni mgonjwa ujue kiliwahi  kukaa kikao cha kuleta huo ugonjwa.

 

 

Leo kama yupo mtu ambaye bado hajaokoka, na anayo kadi ya shetani (hirizi, n.k) leo ikabidhi hiyo kadi nasi tutaichoma moto kwa Jina la Yesu. Leo kataa kuwa mwanachama wa Ibilisi. Wala usisseme kwamba utaenda kuirudisha kadi hiyo kwa aliyekupatia kwa sababu leo tunataka umuaibishe ibilisi hadharani kwa Jina la Yesu.

 

Showers of Glory wakiimba na kumchezea Bwana Yesu Jumapili 10/7/2016
 

 

©  MEDIA & INFORMATION MINISTRY,
GLORY OF CHRIST (T) CHURCH
MOROGORO CHURCH

 

 

 

 
Share:
Powered by Blogger.

Pages