GLORY OF CHRIST TANZANIA CHURCH
UFUFUO NA UZIMA - MOROGORO
JUMAPILI: 21 AUGUST 2016
Na:
STEVEN NAMPUNJU – (RP MOROGORO)
RP Steven Nampunju akifundisha somo "Vita ya Muota Ndoto" Jumapili 21/8/2016 katika Bonde la Maono - Ufufuo na Uzima Mkundi - Morogoro |
Katika maisha ya kawaida, watu huota Ndoto. Wengine kwa sasa utawakuta ni watu wazima
lakini bado wanaota ndoto eti wanajiona wapo darasani hadi sasa hivi‼‼!. Wengine
wapo mijini lakini ndoto zao huota wakiwa viijini mwao wanatembea na miguu bila
viatu na vitu kama hivyo.
Swali la kujiuliza ni Je, Ndoto ni nini? "Ndoto ni dirisha la muonekano wa
vitu vinavyoendelea katika ulimwengu wa roho". Kweye ulimwengu wa mwili wanadamu
pia hupenda kuangalia taarifa ya habari katika TV ili kujua yale yanayoendelea
katika ulimwengu huu wa mwili. Kwa hiyo Mungu hupenda kumfunulia mwanadamu yale ya
ulimwengu wa roho kupitia ndoto, kama ambavyo redio na TV humuonesha mtu
yanayoendelea katika ulimwengu wa mwili.
Mungu anazijua hatima za kila mtu,na kwamba
alikuumba kwa makusudi gani, na yapin yatakuwa matukio yako hapa duniani. AYUBU
33:14-17 ...(Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu
hajali. 15 Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi
mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; 16 Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia
muhuri mafundisho yao, 17 Ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na
kumfichia mtu kiburi; )... Kumbe ukiona unaiota ndoto mara nyingi ngyini
ikijirudia maana yake wewe haujali.)
MWANZO
41:32
(Na
ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu
amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi.)....Ukiona unaota ndoto
na inayojirudia rudia zaidi ya mara moja ujue
- Hakika ndoto hiyo ni halisi na itakuja upesi
- Uliidharau ndoto ile ulipoiota mara ya kwanza, na sasa unakumbushwa.
KWA NINI WATU TUOTE NDOTO?
Mtu akiwa katika ulimwengu wa mwili, na
akayatazama mambo katika ulimwengu wa mwili
hawezi kamwe kufanikiwa. Ili mtu
afanikiwe, lazima autumie ulimwengu wa roho kikamilifu. Ndoto ni kama bahasha tu
ambayo ndani yake imebeba barua halisi yenye ujumbe kamili. Kama unayo changamoto
yoyote katika maisha yako, ujue majibu yake yapo katika ndoto unazoziota.
Sehemu tu ya Umati wa watu waliohudhuria ibada Jumapili 21/8/2016 katika Bonde la Maono Ufufuo na Uzima Mkundi -Morogoro wakimshangilia Bwana Yesu. |
AINA 3 ZA NDOTO:
Zipo aina nyingi za ndoto, lakini leo
tutazungumzia
1.
NDOTO ZA KIPEPO
Hizi zina lengo la kumtia hofu mtu, au kuharibu maisha ya mtu. Mashetani yanao uwezo
wa kumtoa mtu katika makusudio yake.
YUDA 1:8....(Kadhalika na hawa, katika kuota
kwao, huutia mwili uchafu, hukataa kutawaliwa, na kuyatukana matukufu.)....
Mtu anaweza kuota ndoto na kuanza kuyatukana matukufu. Na njia hii ya uotaji
huutia mwili uchafu, maana yake ni maisha yake kugeuka na kuwa machafu kutokana na ndoto aliyoiota mtu mhusika.
2.
NDOTO ZA KIBINADAMU
MHUBIRI 5:3....(Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya
mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno.)..... Hizi ni ndoto anazoota mtu
kutokana na shughuli zake za kazi zake za kawaida. Hapa
utawakuta watu kama vile makondakta wa daladala wakiota ndoto usiku wakipiga debe,
kuita abiria n.k. Wengine kama ni wauza mitumba wataota ndoto wakipigia debe
mitumba. Ukiwashtua usiku huo huo watu hawa watakwambia walikuwa wanaota wakiwa katika shughuli zao za maisha.
3.
NDOTO ZA KIMUNGU
Hizi ni ndoto zenye malengo ya kumuonya mtu,
kumpa mtu maarifa, kumwelekeza mtu n.k.
HESABU
12:6...(Kisha
akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, Bwana,
nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto.)....
AYUBU
33:17....(Ili
amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi;).... Mungu
anasema na mtu kwa lengo la kumuondoa mtu katika makusudio yake. Mfano mzuri ni
wa Yusufu aliyemposa Mariamu mamaye Yesu. Katika Kitabu cha Mathayo, Biblia inasema Yusufu alikusudia
kumuacha Mariamu kwa siri baada ya kuona kuwa yu mjamzito na hakutaka kumuaibisha mchumba wake. Kwa kuwa ni ngumu kujua siri za mtu na amekusudia kufanya nini kwa
siri, basi njia pekee ni ya Mungu kusema na mtu wa aina hii ni kwa njia ya ndoto.
KWA NINI WATU WANAOTA NDOTO?
Imeandikwa katika AMOSI 3:7...(Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote,
bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.). Tunajifunza kuwa
kumbe Mungu hafanyi jambo bila kuwafunulia watumishi wake. Je, shida uliyo nayo uliwahi kufunuliwa na Mungu?
Jibu ni Ndiyo. Leo ni siku ya kuanza upya kwa kuwa ndoto zako lazima zitimie katika
Jina la Yesu. Watu wengine ni wazuri kuwasifia watoto wao kuwa watakuja kuwa watumishi
wakubwa wa Mungu lakini wanasahau kuanza maandalizi ya kuwafanya hao watoto waingie katika huo
mfumo kwa kuwaombea. Wapo wengine walikuwa wakiota ndoto kipindi cha nyuma lakini kwa sasa
hawaoti ndoto tena na pengine hata wakiota wanasahau walichoota ni nini‼ Hii
inamaanisha kuwa, Mungu aliyekuwa akikuotesha ndoto ameona hakuna umuhimu tena
wa kukupa taarifa hizi kwa njia ya ndoto kila mara kwa kuwa wewe ukipewa hufanyii kazi.
MAMBO MUHIMU YA KUFAHAMU NDANI YA NDOTO
1.
Ndoto yaweza kumtisha
mtu
AYUBU 7:14....(Ndipo unitishapo kwa ndoto, Na kunitia hofu kwa maono;). Ndani ya ndoto vyaweza
kuwepo vitisho. Mungu anaweza kumtisha
mtu katika ndoto na shetani vile vile.
2.
Ndoto yaweza
kumfadhaisha mtu
Ndani ya ndoto inaweza kuwepo siri, ili mtu
anapoiota hiyo ndoto, mtu huyo
afedheheke na asiendelee tena na mpango aliokuwa nao.
Mathalani, endapo ulikuwa unaota ndoto fulani juu ya kazi uliyokuwa
unaifuatilia, unapojikuta unafadhaishwa,
uujue hapo shetani ameingilia kati ili kuacha huo mpango wa mafanikio yako.
3.
Ndani ya ndoto kuna
kipimo halisi cha rohoni cha jinsi mtu
alivyo rohoni
Siri kubwa ipo ndani ya ndoto unapoota, na
ndiyo njia ya kumfanya mtu ajijue yupo je rohoni mwake.
Imeandikwa katika MWANZO 20:2-6....(Ibrahimu akamnena Sara mkewe, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akapeleka watu akamtwaa Sara. 3 Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu. 4 Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee Bwana, Je! Utaua hata taifa lenye haki? 5 Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi. 6 Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse.)... Tunamuona Abimeleki kuwa ni mkamilifu rohoni, na kipimo hiki amekipata kupitia ndotoni. Ni maombi yetu kuwa Mungu akupe uwezo wa kuwashinda maadui zako rohoni na mwilini katika Jina la Yesu. Mathalani endapo unaota ndoto ukiwa unakabwa usiku, ujue hicho ni kipimo tosha kuwa haupo vizuri kiroho.
4. Ndani ya ndoto kuna maelekezo ya usiyoyajua
Ndani ya ndoto ipo siri usiyoijua. Imeandikwa katika MWANZO 28:12-16...(Akaota ndoto; na tazama, ngazi
imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika
wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. 13 Na tazama, Bwana amesimama juu
yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka;
nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. 14 Na uzao wako utakuwa kama
mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini,
na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia
watabarikiwa. 15 Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako,
nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata
nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. 16 Yakobo akaamka katika usingizi wake,
akasema, Kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua). Yakobo
alikuwa anakimbia kuiponya roho yake. Kwa kuwa alikuwa anakimbia, maana yake hakuwa na maandalizi yoyote. Na kile asichokijua ni kuwa Mungu alikuwepo mahali pale.
5.
Ndani ya ndoto zako ipo
siri ya hatima yako
Katika ndoto anazoota mtu, ipo ndoto moja iliyobeba
siri ya hatima yake. Ukiwaona wahubiri,
waimbaji wa Injili na wengineo,
ukiwauliza swali juu yao watakuambia zipo ndoto walizokuwa wakiota nyakati fulani
maishani mwao kabla ya kuwa vile walivyo.
Imeandikwa katika MWANZO 37:1-4...( Yakobo akakaa katika nchi aliyosafiri baba yake, katika nchi ya Kanaani. 2 Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya. 3 Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. 4 Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani.)... Unaweza kuiona familia ambayo mmezaliwa watu 6 au zaidi, na wenzako wote wameungana ila wewe pekee wanakuchukia. Hiyo siyo shida, kwa sababu Mungu anakuwa ameweka makusudi mazuri maishani mwako. Yusufu alipendwa na baba yake kuliko wengine, na huu ukawa mwanzo wa wenzake kumchukia.
MWANZO
37:5....(Yusufu
akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia;).
Chuki zingine hutokea kwa sababu ya ndoto zako. Maadui zako hutiwa hofu na aina ya
ndoto unayoiota. Ni maombi yetu kwa Mungu kuwa maadui zako watiwe hofu kupitia ndoto zako kwa Jina la
Yesu. Kipindi kile cha Gideoni, katika Kitabu cha Waamuzi, adui zake waliota ndoto
wenyewe na kuitafsiri wenyewe na baada ya hiyo wakawa na hofu na kukimbia
hovyo. Ni maombi yetu kwa Mungu kuwa adui zako waote ndoto ziwatie hofu na kukukimbia wakuonapo kwa Jina la Yesu.
Imeandikwa katika MWANZO
37:6-8 ....
(akawaambia,
Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. 7 Tazama, sisi tulikuwa tukifunga
miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda
yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. 8 Ndugu zake wakamwambia, Je!
Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa
ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake). Ndugu za Yusufu waligundua
kuwa ile miganda ni wao wenyewe, na kwa
tafasiri hii waliongeza chuki zaidi.
Maombezi yakiendelea kufanywa kwa watu wenye vita ya muota ndoto |
Imeandikwa katika MWANZO
40:5-22....(
5 Wakaota
ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya
ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa
mfalme wa Misri waliofungwa gerezani. 6 Yusufu akawajia asubuhi, akawaona
wamefadhaika.). Hawa ni wafungwa wamefungwa gereza moja
lakini wakaota ndoto tofauti tofauti. Ukiona
mtu amefadhaika, ujue ipo ndoto
aliyoiota na ambayo hajui tafasiri yake.
6.
Unaweza kuuawa kwa
sababu ya ndoto zako
MWANZO
37:18-20....(Wakamwona toka
mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. 19
Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. 20 Haya, twende,
tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla;
kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.). Mipango miovu inapangwa juu ya mauti ya mtu
lakini chanzo cha yote haya ni zile ndoto anazoziota mtu huyu. Usidhani ni kila mtu
anafurahia ndoto zako. Wanadamu wanaweza kufanya mipango ya kuzuia mafanikio
yako, au kushindana na ndoto zako.
7. Ndani ya ndoto zipo mbinu na namna ya kukabilana na chagnamoto zilizo mbele yako
Unaweza kujiona kuwa una amani, na unakaa
vizuri na familia yako. Hata hivyo Mungu aweza kukuotesha ndoto na namna ya
kukabiliana na yale maovu yaliyopangwa juu yako au ndoa yako.
Ukisoma
Kitabu cha MWANZO 41:1-36 utagundua kuwa, wapo
watu waliomsahau Yusufu baada ya kutolewa gerezani. Zipo hali unazoishi
leo kwa sababu ulimsahau Yusufu uliyekuwa naye gerezani. Wazazi wako wapo
vijijini na wanapata shida, lakini wewe leo hii unaendelea na maisha mazuri
mjini na huku umewasahu wazazi wako.
Umeokoka, na ndugu zako hata hujawahubiria‼!. Yusufu hakupoteza muda wake kumpa
maagizo yoyote yule mfungwa ambaye baada ya siku 3 atanyongwa, bali alimpa maagizo yule ambaye
atakuja kuwa mbele ya Mfalme siku zote kwamba asimsahau!!!!.
Yusufu alikumbukwa tena pale mfalme alipoota
ndoto. Hata hivyo alipotolewa gerezani ilibidi abadilishiwe mavazi yake ya
ufungwa. Wengi wetu leo hii tunataka kumwendea Mfalme Yesu tukiwa bado na
mavazi ya ufungwa. Hii si vyema. Badilisha mavazi uliyotoka nayo gerezani
kwanza, ili uweze kukaa na Mfalme Yesu maishani
mwako.
Imeandikwa katika MWANZO
41:30-36....(Kisha
kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika
nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi. 31 Wala shibe ile haitajulikana katika
nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana. 32 Na
ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu
amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi. 33 Basi, Farao na ajitafutie mtu
wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri. 34 Farao na afanye hivi, tena
akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri,
katika miaka hii saba ya kushiba. 35 Na wakusanye chakula chote cha miaka hii
myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa
chakula katika miji. 36 Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa
ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi
isiharibike kwa njaa.). Zipo njaa zenye kuharibu nchi, njaa zenye kuharibu
vipawa vya watu. Watu wengi hawajifunzi kuweka akiba.
UKIRI
Kuanzia leo,
na kuanzia sasa, Ninawakabili mashetani na majini, yaniache kwa Jina la Yesu. Amen
|
NIFANYE JE NIKIOTA NDOTO
Ndoto ni ripoti apewayo mtu akiwa amelala usingizini.
Unao wajibu wa kushughulikia hiyo ripoti.
Ø
Jambo
la kwanza la kufanya ni kubaini kama ripoti hiyo ni njema au mbaya.
Ø
Jambo
la pili ni kuanza kushughulikia ndoto hiyo haraka sana pindi tu uamkapo.
Kwa nini iwe haraka? Ni kwa sababu baada ya
ndoto tu utekelezaji wa ulichokiota huanza mara moja. Na kwa kuwa ndoto zipo za
aina tatu, ni vyema kufanya haraka. Ndoto zina tafasiri zake. Usiende kwa
wachawi kwa ajili ya kupata tafasiri zake. Mfuate mchungaji wa Mungu na
aliyeokoka mwelezee hiyo ndoto. Kama ndoto ni ya kimungu, ya mambo mazuri
iombee itokee mara moja kwa Jina la Yesu. Endapo ndoto ni ya kishetani (ndoto
chafu ya mambo mabaya), inabidi uiharibu isitokee kwako kwa Jina la Yesu.
Vijana wa Showers of Glory wakicheza mbele za Bwana Jumapili 21/8/2016. |
Endapo mtu hujaokoka hadi leo hii, siyo rahisi kuharibu
ndoto mbaya zinazokuja kwako. Inabidi yawepo mahusiano mema na Bwana Yesu
kwanza ili kukabiliana na ndoto mbaya za maishani mwako kwa Jina la Yesu.
© MEDIA & INFORMATION MINISTRY,
GLORY OF CHRIST (T)
CHURCH
==GCTC==
Tel: +255765979866 / or +255713459545
MOROGORO CHURCH
|